• HABARI MPYA

    Wednesday, March 20, 2013

    MALKIA WA NYUKI ATOA MSIMAMO WAKE MZITO SIMBA SC

    Kulia kikosi cha Simba SC, kushoto Malkia wa Nyuki

    Na Mahmoud Zubeiry
    MFADHILI wa Simba SC, Rahma Al Kharoos maarufu kama Malkia wa Nyuki amesema kwamba hatambui uteuzi wake katika Mkutano ulioupindua uongozi kwa sababu anafikiria zaidi vita ya kuinusuru timu katika wakati huu mgumu.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY leo, Malkia ambaye alisema alikuwa safarini wakati mapinduzi hayo yanafanyika mwishoni mwa wiki, alisema haelewi nini dhamira ya kutajwa kwake katika mkutano ule uliotishwa kinyume cha Katiba ya Simba SC.
    “Hawa watu kama wangekuwa wana nia nzuri na Simba au mimi, wangenihusisha katika mambo yao, lakini hawakunihusisha na wanakwenda kutaja jina langu bila kuwasiliana na mimi. Kwa kweli sijapenda,”alisema.
    Malkia wa Nyuki
    Hata hivyo, Malkia alisema hataki kuzungumzia zaidi mambo hayo kwa sasa, kwa kuwa kichwa chake kimetingwa na majukumu ya kuinusuru timu.
    “Hapa najipanga kwa mechi za Kanda ya Ziwa, nataka tuchukue pointi sita za Kanda ya Ziwa tujiweke sawa. Hata kama hatuwezi kupata ubingwa, lakini lazima tupate nafasi ya pili,”alisema.
    Aidha, Mama Al Kharoos amesistiza huu si wakati mwafaka kwake kuzungumzia siasa za klabu au migogoro, bali anataka asikie kuhusu kuiwezesha Simba kutetea ubingwa au kushika nafasi ya pili.
    Jumapili wanachama 698 wa  klabu ya Simba walifikia uamuzi wa kuuondoa madarakani uongozi wa klabu yao na kuunda Kamati Maalum ya Muda, wakiwateua Zacharia Hans Poppe na Malkia wa Nyuki kuiongoza.
    Katika Mkutano uliofanyika kwenye ukumbi maarufu wa Star Light Cinema, Dar es Salaam, wanachama hao walifikia uamuzi wa pamoja kuuondoa madarakani uongozi huo, kutokana na kile kilichoelezwa kushindwa kutekeleza majukumu yao na kuifikisha timu pabaya.
    Pamoja na kuikabidhi timu kwa Hans Poppe, wanachama hao wamesema watakuwa bega kwa bega na viongozi hao wateule kuhakikisha wanafanikisha azma ya kurejesha hadhi na makali ya timu.
    Lakini uongozi wa Simba SC unaukana Mkutano huo kwamba ni batili na Mkutano Mkuu halali wa klabu hiyo, utafanyika baada ya Mwenyekiti wa klabu, Alhaj Ismail Aden Rage kurejea kutoka India anakotibiwa.
    Lakini wanachama hao walisema wameamua kufanya Mkutano huo kwa sababu uongozi umekuwa ukipiga chenga kufanya Mkutano na kulingana na hali ilivyo mbaya ndani ya klabu, wamechukua hatua hiyo ili kuinusuru klabu.
    Kwa upande wake, Hans Poppe, kwanza alisema hana taarifa za Mkutano huo wala yaliyofikiwa.
    “Sina taarifa na wala siafiki, kwa sababu hakuna mtu aliyeshauriana na mimi kabla, na pia wamefanya mambo kinyume na Katiba,”alisema Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
    “Lazima wanachama wawe na subira, wasubiri Mwenyekiti arudi aitishe mwenyewe Mkutano, yeye mwenyewe (Mwenyekiti) alikwishasema ataitisha Mkutano, sasa kitu gani kinachowafanya wao wanakosa subira,”.
    “Mbaya zaidi wamekwenda kufanya Mkutano wao na kufikia maamuzi yao, bila hata kunitafuta kuniuliza kwanza, sasa hii si ni dharau? Ina maana wao wanataka mimi nifanye wanavyotaka wao, mimi sitaki kuwa sehemu ya migogoro katika Simba,” alisema Hans Poppe. 
    Kwa ujumla, hamkani si shwari sasa ndani ya Simba SC, kufuatia viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Hans Poppe aliyekuwa pia Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili  kujiuzulu wiki mbili zilizopita.
    Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Rage yuko India kwa matibabu na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Joseph Itangare ‘Kinesi’ aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, sasa ndiye anakaimu Uenyekiti wa klabu.
    Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Malkia wa Nyuki.
    Malkia wa Nyuki alianza vyema jana baada ya kuiongoza Simba SC kuilaza 2-1 Coastal Union na sasa anajiandaa kwenda kucheza mechi ya pili, dhidi ya Kagera Sugar mjini Bukoba Jumatano ijayo.
    Simba SC ambao ni mabingwa watetezi, kwa sasa inazidiwa kwa pointi 14 na Yanga SC, inayoongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 48, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 37. Simba ya tatu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MALKIA WA NYUKI ATOA MSIMAMO WAKE MZITO SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top