• HABARI MPYA

    Monday, March 25, 2013

    TAIFA STARS SASA NI STARS KWELI

    Wachezaji wa Stars wakimpongeza Mbwana Samatta

    Na Mahmoud Zubeiry
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, jana imeifunga Morocco mabao 3-1 katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
    Shukrani kwao, washambuliaji wawili wanaochezea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu waliofunga mabao hayo yote.
    Samatta alifunga mawili na Ulimwengu aliyetokea benchi dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula alifunga moja.
    Kwa matokeo hayo, Stars inaendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi C kwa pointi zake sita, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake saba, baada ya juzi kushinda 3-0 dhidi ya Gambia.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa kutoka Angola Helder Martins aliyesaidiwa na ndugu zake, Inacio Manuel na Ricardi Daniel washika vibendera, hadi mapumziko hakukuwa na bao.
    Kipindi cha pili, Stars walianza na mabadiliko, kocha Mdenmark Kim Poulsen akimtoa Kazimoto na kumuingiza Ulimwengu aliyekwenda kubadilisha kabisa mchezo.
    Katika dakika ya 46, mpira wa kwanza kuugusa Thomas Ulimwengu ambao alirushiwa na beki Erasto Nyoni aliunganisha nyavuni na kuipatia Stars bao la kwanza.
    Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwa upande wa Stars na katika dakika ya 67, Samatta alifunga bao la pili akimchambua kipa Nadir Lamyaghri baada ya kupokea pasi nzuri ya Ulimwengu ambaye naye alipasiwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyetokea benchi pia.
    Morocco walionekana kuchanganyikiwa baada ya bao la pili na kuruhusu Stars kutawala zaidi mchezo.
    Zilikuwa zinapigwa pasi zisizo na idadi, ili mradi burudani kwa mashabiki wa soka wa Tanzania waliyokuwa wakipatiwa na wachezaji wa timu yao.
    Lakini katika mtindo huo huo, Stars ilikuwa inatengeneza mashambulizi ya kushitukiza yaliyosababisha kosakosa kadhaa langoni mwa Morocco.
    Hata hivyo, kazi nzuri ya Ulimwengu aliyepambana na beki wa Morocco na kumzidi nguvu hatimaye kufanikiwa kupiga krosi, liliipatia Stars bao la tatu lililounganishwa kimiani na Samatta dakika ya 80.
    Beki Abderrahim Achchakir alipewa kadi nyekundu kwa kumtolea kauli chafu refa baada ya Stars kufunga bao la tatu. Beki huyo alikuwa kama analalamika kuchezewa rafu na Uli wakati akipiga krosi ya bao.
    Burudani iliongezeka baada ya bao hilo, Stars wakigonga pasi nyingi- hata hivyo kosa kidogo la safu ya ulinzi liliipa nafasi Morocco kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Yousef Elarabi aliyetokea benchi. 
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Tanzania, Mdenmark Kim Poulsen alisema kwamba amefurahia matokeo na anawapongeza vijana, lakini bado ana kazi ngumu katika mechi tatu zijazo dhidi ya Morocco na Gambia ugenini na Ivory Coast nyumbani. 
    Jana Poulsen alipanga kikosi chake hivi; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk 63, Frank Domayo, Mbwana Samatta/John Bocco dk 91, Mwinyi Kazimoto/Thomas Ulimwengu dk46 na Amri Kiemba.
    Kutoka kulia Juma Kaseja, Amri Kiemba, Kevin Yondan, Erasto Nyoni na Shomary Kapombe

    SAFU YA ULINZI:
    Utasemaje kuhusu kipa na Nahodha Juma Kaseja jana juu ya kazi nzuri aliyoifanya kama si kusema alikuwa mchezaji bora wa mechi, alitulia mno langoni na kucheza kwa maelewano makubwa na safu yake ya ulinzi.
    Alicheza krosi vizuri, aliokoa michomo kadhaa na aliweza kuitokea vema mipira na kuinyaka. Alikuwa mwepesi wa kuanzisha mashambulizi anapoona timu imekaa katika mwelekeo wa kushambulia. Kwa ujumla alifanya kazi nzuri.
    Beki wa kulia, Erasto Nyoni alifanya kazi yake vzuri. Alikuwa anazuia na kupanda mno kusaidia mashambulizi.
    Nyoni alikuwa akiipeleka mno timu mbele na kutia krosi. Alikuwa akirusha vizuri mipira yake na ndiye aliyetoa pasi ya bao la kwanza baada ya kumrushia mpira vizuri Ulimwengu akaunganisha nyavuni.
    Beki wa kushoto, Shomary Kapombe naye alifanya kazi nzuri ya kuzuia na kusaidia mashambulizi. Kuna wakati alipanda vizuri na kuingia ndani kabla ya kupiga shuti zuri lililokwenda nje sentimita chache
    Alikuwa akipanda kusaidia mashambulizi na kutoa pasi na krosi nzuri kwa washambuliaji, Mrisho Ngassa, Mbwana Samatta na hata Ulimwengu alipoingia.
    Kuna wakati Kapombe alijaribu kuingia mwenyewe kwenye eneo la hatari na kwa ujumla alionyesha ni mchezaji mwenye mustakabali mzuri katika timu ya taifa.
    Mabeki wa kati, Aggrey Morris na Kevin Yondan hao ndio wanastahili pongezi kubwa sana kwa kutulia na kucheza kwa uelewano mkubwa.
    Hakika waliweza kumlinda vema kipa wao, dhidi ya washambuliaji hatari, wenye kila kitu na dakika 90+4 zikamalizika nyavu za Stars zikitikiswa mara moja, tena kwa bao la dakika za majeruhi lililotokana na mabeki hao kujisahau kidogo.
    Amri Kiemba akiwajibika hapa

    SAFU YA KIUNGO:
    Jambo la kufurahisha zaidi, mbele ya walinzi jana walikuwa wakicheza viungo wawili, Frank Domayo na Salum Abubakar 'Sure Boy' kama viungo wa ulinzi, ambao walifanya kazi nzuri mno.
    Walikuwa wakisaidia mno ukabaji, na wakati huo huo wakiipandisha timu kwa haraka wakishirikiana na viungo wenzao Mwinyi Kazimoto na Amri Kiemba, ambao walikuwa wachezeshaji jana.
    Mfumo wa sasa Stars ni sehemu nyingine ya burudani, iliyobeba matumaini ya timu ya taifa, kucheza kitimu na kwa uelewano wa hali ya juu.
    Uchezaji wa aina ile, wa kila mchezaji kuwajibika uwanjani, timu inapokuwa ina au haina mpira ndiyo maana ya nidhamu ya kiuchezaji na kama timu itaendelea hivyo, kuna uwezekano wa ndoto kutimia.
    Viungo hawa wote walikuwa wakichezesha timu na wote walikuwa wakikaba na hilo lilisaidia sana Stars jana kutoingia kwenye makucha ya Simba wa Atlasi.
    Pasi muruwa walizokuwa wakipiga zilikuwa mtihani mzito kwa wachezaji wa Morocco, ambao pamoja na kujitahidi kuibana Stars kwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza, lakini kipindi cha pili walichemsha.
    Walichemsha na kuwaacha vijana wa Tanzania wakiwarusha mashabiki wao kwa shangwe za burudani ya kandanda safi yenye kupendeza na kushangilia mabao ya kiwango cha juu.
    Thomas Ulimwengu akiwatoka mabeki wa Morocco

    SAFU YA USHAMBULIAJI:
    Morocco hawakuwa wabaya katika safu yao ya ulinzi na ndiyo maana kwa dakika zote 45 za kipindi cha kwanza waliwabana Stars. Mashuti mengi yalipigiwa nje ya eneo la hatari.
    Lakini bado wachezaji wa Stars waliendelea kupambana kuhakikisha kipyenga cha kuhitimisha mchezo hakilii kabla hawajapata bao.
    Ni ukweli usiopingika ushindi wa jana, ulitokana na kazi nzuri ya Ulimwengu- kama si Kaseja basi huyo ni mtu mwingine unayeweza kusema alikuwa mchezaji bora wa mechi. Aliingia uwanjani akiwa tayari amekwishaisoma vyema safu ya ulinzi ya Morocco.
    Alikwenda kuwanyanyasa mno wale mabeki wa Morocco hadi wakamchukia na kuanza kumsukuma na kumtolea maneno kila alipowashinda. Lakini dogo anaelewa sasa, alikuwa akiachana nao na kuendelea kufanya kazi ya taifa.
    Tazama alivyofunga bao la kwanza- yale ni mabao ambayo yanafungwa na wachezaji bora sana Ulaya. Alirushiwa mpira akiwa amebanwa, lakini akaumiliki na kugeuka nao kabla ya kufumua shuti lililotinga nyavuni.
    Cheki alivyopambana na yule beki wa Morocco hadi akamuacha na kumfunga tela kabla ya kutoa mkrosi ya bao la tatu. Lakini pia vipi kuhusu uamuzi wa haraka wa kumpa pasi Samatta ya bao la pili, baada ya kupewa mpira na Athumani Iddi ‘Chuji’.
    Na vipi kuhusu krosi zake zenye mikato makini, zinazokwenda kwa mlengwa. Thomas Emmanuel Ulimwengu kijana aliyeibuliwa katika akademi ya TSA sasa anatufaa na haya ndio matunda ya uwekezaji.   
    Benchi la Ufundi kwa pamoja na wachezaji wa akiba

    BENCHI LA UFUNDI:
    Soka iliyochezwa na Stars jana, pekee ni kielelezo cha kazi nzuri ya benchi la ufundi. Mabadiliko yaliyofanywa na Stars jana, kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza mshambuliaji Thomas Ulimwengu kwa kiasi kikubwa yalichangia kupatikana kwa ushindi wa jana.
    Na kutokana na Ulimwengu kwenda kushambulia zaidi akitokea pembeni, akatolewa Ngassa na kuingizwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ ili kutengeneza uwiano sawa. Chuji alikwenda kucheza nafasi ya Mwinyi Kazimoto na alikuwa ana mchango wake katika bao la pili. 
    Ilionekana ni mipango, ambayo kocha Mdenmark Kim Poulsen na wasaidizi wake, Sylvester Marsh na Juma Pondamali waliingia nayo uwanjani.
    Kwanza, kulundika viungo wengi ili wakazibe njia za Morocco kuipitisha mipira, lakini baadaye kabisa, kupunguza kiungo na kuongeza mshambuliaji, ili kuzidisha nguvu ya mashambulizi na hatimaye kupatikana kwa japo bao kama si mabao.  
    Kikosi cha Stars jana

    STARS INATIA MATUMAINI:
    Kwa ujumla Stars imebadilika kwa kiasi kikubwa, jana ikishinda mechi ya nne kati ya tano ilizocheza ndani ya miezi minne iliyopita.
    Novemba, iliifunga Kenya 1-0 mjini Mwanza, Desemba ikaifunga Zambia 1-0 mjini Dar es Salaam na Januari ikafungwa 2-1 ugenini nchini Ethiopia kabla ya kuifunga Cameroon 1-0 mwezi uliopita.
    Kwa waliokuwa wakibeza kampeni za Stars kuelekea Brazil 2014, bila shaka sasa wako vichwa chini. Stars itaikaribisha Ivory Coast hapa Juni 14, baada ya kurudiana na Morocco Juni 7 ugenini. Mechi na Morocco lolote linaweza kutokea lakini ‘Mungu akijaalia’ hata sare itatufaa. Na inawezekana.
    Lakini mikakati madhubuti ikiwekwa, Tembo auawe hapa Dar es Salaam na kwa kuwa huyo ndiye mpinzani wetu mkuu kwenye kundi letu, tutazungumza lugha nyingine wakati huo ukifika. Gambia ambaye amekwishajikatia tamaa kumfunga kwake inawezekana.
    Picha ndogo kushoto juu, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, na picha kubwa ni basi la kisasa la Taifa Stars

    HAYA NI MATUNDA YA UDHAMINI WA TBL
    MEI 9, mwaka jana, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilisaini mkataba wa udhamini na TBL wa miaka mitano, ambao kila mwaka zinatoka zaidi ya dola za Kimarekani Milioni 2 kwa ajili ya Taifa Stars.
    Ni kiasi kikubwa cha fedha kutoka huko tulipotoka, ambacho kwa hakika kimebadilisha kabisa taswira nzima ya Taifa Stars.
    Hadhi ya timu ya taifa imebadilika mno. Timu sasa wachezaji wanaweka kambi katika hoteli ya hadhi kwa muda mrefu. Wanapatiwa posho nzuri. Timu imepatiwa basi zuri la kisasa. Hadi ya Taifa Stars iko juu sana.
    TBL inajihusisha kikamilifu katika masuala ya kila siku kuhusu timu ya taifa. Na kwa sababu hiyo, mafanikio ya Stars hivi sasa ni matunda ya udhamini mzuri wa TBL, kupitia bia yake ya Kilamnjaro.  
    Kila la heri Taifa Stars katika kampeni za kuwania tiketi ya Kombe la Dunia Brazil 2014 na shukrani kwao wadhamini wa timu yetu, Kilimanjaro Premium Lager kwa kufanikisha furaha ya Watanzania.

    MSIMAMO WA KUNDI C ULIVYO SASA:
                         P W D L GF GA GD Pts
    1 Ivory Coast 3 2 1 0 7 2 5 7
    2 Tanzania    3 2 0 1 5 4 1 6
    3 Morocco     3 0 2 1 4 6 -2 2
    4 Gambia 3 0 1 2 2 6 -4 1

    REKODI YA STARS CHINI YA UDHAMINI WA KILIMANJARO PREMIUM LAGER:
    Mei 26, 2012
    Tanzania 0 – 0 Malawi (Kirafiki)
    Juni 2, 2012
    Ivory Coast 2 – 0 Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 10, 2012
    Tanzania 2 – 1 Gambia (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 17, 2012
    Msumbiji 1 – 1 Tanzania (Tanzania ilitolewa kwa penalti kufuzu Mataifa ya Afrika)
    Agosti 15, 2012
    Botswana 3 – 3 Tanzania (Kirafiki)
    Novemba 14, 2012
    Tanzania 1-0 Kenya (Kirafiki)
    Desemba 22, 2012
    Tanzania 1-0 Zambia (Kirafiki)
    Januari 11, 2013
    Tanzania 1-2 Ethiopia (Kirafiki)
    Februari 6, 2013
    Tanzania 1-0 Cameroon (Kirafiki)
    Machi 22, 2013
    Tanzania 3-1 Morocco (Kufuzu Kombe la Dunia)

    MECHI ZIJAZO:
    Juni 7, 2013
    Morocco Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Juni 14, 2013
    Tanzania Vs Ivory Coast (Kufuzu Kombe la Dunia)
    Septemba 6, 2013
    Gambia Vs Tanzania (Kufuzu Kombe la Dunia)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TAIFA STARS SASA NI STARS KWELI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top