• HABARI MPYA

    Monday, March 11, 2013

    MPYA SIMBA SC; BABU MFARANSA MIEZI MIWILI HANA MSHAHARA, HALI TETE

    Maji ya shingo; Kocha Patrick Liewig

    Na Mahmoud Zubeiry
    KOCHA Mfaransa wa Simba SC, Patrick Liewig anaweza kuondoka wakati wowote bila hata kufukuzwa, baada ya maji kumfika shingoni, imefahamika.
    Habari za ndani, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zimesema kwamba Mfaransa huyo ana miezi miwili hajalipwa mishahara na hapo hapo kwa takriban wiki sasa amepokonywa gari.
    Gari alilokuwa anatumia kocha huyo ya GX110 linashikiliwa na uongozi wa hoteli ya Spice, iliyopo Kariakoo, Dar es Salaam ambao unaidai klabu hiyo kiasi cha Sh. Milioni 28.
    Spice ndiyo kambi kuu ya Simba SC mwaka jana, lakini baada ya deni kuwa kubwa, wakahamia katika hoteli ya Sapphire Court, iliyopo Kariakoo pia ambako nako walifukuzwa jana baada ya deni kuwa kubwa. 
    Habari zinasema kocha Liewig amekuwa akilalamikia kufanya kazi katika mazingira magumu na hana matumaini ya kutimiza ndoto zake katkka klabu hiyo.
    “Nidhamu ya wachezaji ni mbovu, huo ni mtihani mkubwa wa kwanza alionao, bado na matatizo mengine kibao, usimuone vile yule babu, ni mvumilivu sana kwa kweli,”kilisema chanzo chetu kutoka Simba SC.
    Tayari benchi la Ufundi la Simba SC nalo limeanza kumeguka, baada ya aliyekuwa Mtunza Vifaa, Kessy Rajab kuandika barua ya kujiuzulu.
    Inadaiwa Daktari Cossmas Kapinga naye ameachia ngazi na jana hakuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati timu hiyo ikimenyana na Coastal Union ya Tanga.
    Meneja Moses Basena kutoka Uganda, amekuwa akiambiwa na wafanyakazi wenzake Simba SC kwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa klabu, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliyemleta amejiuzulu, naye bora angendoka.     
    Lakini Basena amekuwa akiwajibu yeye ana mkataba na Simba SC na si mtu na aliletwa mtu basi alifanya kwa niaba ya klabu kutokana na dhamana aliyopewa na wanachama.
    Jana usiku Basena, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde, wote raia wa Uganda, walifukuzwa kwenye hoteli ya Spice, Kariakoo, Dar es Salaam kutokana na klabu hiyo kulimbikiza deni la Sh. Milioni 27.
    Pamoja na kufukuzwa kwa Waganda hao usiku huo, uongozi wa Spice Hotel unashikilia magari mawili ya Simba SC, basi dogo na gari la kocha, aina ya GX110 hadi ulipwe fedha zake.
    Kutokana na kufukuzwa Spice, Waganda hao walikwenda kuomba hifadhi katika hoteli ya Sapphire, ambako walipokelewa na kupewa vyumba vitatu. Kocha Mfaransa, Patrick Liewig pekee ameachwa aendelee kuishi katika hoteli ya Spice. 
    Mapema jana mchana, uongozi wa hoteli ya Sapphire Court, iliyopo Kariakoo pia, uliwazuia hotelini wachezaji wa Simba SC waliokuwa kambini hotelini hapo, ukishinikiza kulipwa deni la Sh. Milioni 25.7.
    Simba SC ilizuiwa ikiwa inajiandaa kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Coastal Union ya Tanga katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Hata hivyo, baadaye kaimu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itangare ‘Kinesi’ alikwenda kuzungumza na wamiliki wa hoteli hiyo na kufikia mwafaka wa kulipa baada ya mechi ya Coastal.
    Katibu wa Simba SC, Evodius Mtawala amesaini hati ya kuahidi kulipa deni hilo baada ya mechi ya jana. Bado Menejimenti ya Sapphire inasistiza kulipwa fedha zake, vinginevyo itachukua hatua za kisheria dhidi ya klabu hiyo.   
    Hamkani si shwari sasa ndani ya Simba SC, kufuatia viongozi wawili wa Kamati ya Utendaji, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Zacharia Hans Poppe kujiuzulu wiki iliyopita.
    Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage yuko India kwa matibabu na Kinesi aliyeteuliwa kukaimu Umakamu Mwenyekiti, sasa ndiye anakaimu Uenyekiti wa klabu.
    Aidha, Baraza la Wazee kwa pamoja na Baraza la Wadhamini, wameunda Kamati Maalum ya kusimamia timu kuhakikisha inafanya vizuri katika wakati huu mgumu, chini ya Mwenyekiti, Rahma Al Kharoos, maarufu kama Malkia wa Nyuki.
    Malkia wa Nyuki alianza vyema jana baada ya kuiongoza Simba SC kuilaza 2-1 Coastal Union.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MPYA SIMBA SC; BABU MFARANSA MIEZI MIWILI HANA MSHAHARA, HALI TETE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top