• HABARI MPYA

    Saturday, April 04, 2015

    YANGA SC WAFANYA MAZOEZI KWENYE BUSTANI BULAWAYO

    Na Mwandishi Wetu, BULAWAYO
    YANGA SC wamelazimika kufanya mazoezi katika bustani ya hoteli ya Rainbow mjini Bulawayo asubuhi ya leo, kutokana na kukosa Uwanja.
    Hiyo inafuatia timu hiyo kuchelewa kuwasili Bulawayo, ikifika jana majira ya Saa 1 na ushei usiku ikitokea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo wa marudiano, hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, FC Platinum.
    Yanga SC ilichelewa kuondoka Dar es Salaam baada ya kugandishwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) tangu saa 4 asubuhi hadi saa 7 na ushei mchana jana kwa madai uongozi wa klabu hiyo ulikuwa haujalipia ndege.
    Yanga wakifanya mazoezi katika bustani ya hoteli ya Rainbow leo asubuhi

    Yanga SC imekodi ndege ya Serikali kwenda Bulawayo, Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, FC Platinum.
    Hata hivyo, ilidaiwa uongozi wa ndege jana uligoma kuwapakia wachezaji hao hadi malipo yafanyike- na sakata hilo likatatuliwa saa 7 na ushei mchana na wachezaji wakapanda ndege kuondoka.
    Kutokana na kuchelewa kufika, Yanga SC wameshindwa kufanya mazoezi kwenye Uwanja Mandava kwa mujibu wa sheria za CAF jana, kwamba timu ngeni inapaswa kufanya mazeozi kwenye Uwanja wa mechi siku moja kabla.
    Kocha Mholanzi, Hans van der Pluijm aliwaongoza wachezaji wake kufanya mazoezi katika bustani ya hoteli ya Rainbow asubuhi ya leo.
    Yanga SC sasa wataujaribu Uwanja huo baadaye leo, muda mfupi kabla ya mchezo wakati wa kufanya mazoezi ya kuipasha miili ya wachezaji joto.
    Kikosi cha wachezaji 18 wa Yanga SC kimetua salama Bulawayo, Zimbabwe kwa ajili ya mchezo wa marudiano hatua ya 32 Bora Kombe la Shirikisho Afrika.
    Platinum wanatakiwa kushinda mabao 4-0 Uwanja wa Mandava kesho ili kwenda 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, baada ya awali timu hiyo yenye maskani yake Zvishavane kufungwa mabao 5-1 Dar es Salaam.
    Wachezaji waliopo na Yanga Bulawayo ni makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Ally Mustafa ‘Barthez’, mabeki Juma Abdul, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Pato Ngonyani, Rajab Zahir, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kevin Yondan.
    Viungo ni Salum Telela, Said Juma, Nizar Khalfan, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Mrisho Ngassa na washambuliaji Danny Mrwanda, Amisi Tambwe na Hussein Javu.
    Benchi la Ufundi litaongozwa na Kocha Mkuu, Pluijm, Msaidizi wake Charles Boniface Mkwasa, kocha wa makipa Juma Pondamali, Meneja Hafidh Saleh, Daktari Sufiani Juma, mtunza vifaa, Mahmoud Omar ‘Mpogolo’ na Mchua misuli Jacob Onyango.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAFANYA MAZOEZI KWENYE BUSTANI BULAWAYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top