• HABARI MPYA

    Saturday, April 04, 2015

    MUDI MATUMLA KUPANDA ULINGO MMOJA NA MAYWEATHER, PACQUIAO LILIKUWA CHANGA LA MACHO, HUYO NDIYE PROMOTA JAY MSANGI

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    ILI kuvutia watu wengi ukumbi wa Diamond Jubilee, ilibidi promota Jay Msangi awadanganye Watanzania, eti mshindi wa pambano kati ya Mohammed Matumla Jr. na Mchina Wang Xin Hua atapigana katika pambano la utangulizi, kabla ya Mmarekani Floyd Mayweather Jr. kuzipiga na Mfilipino, Manny Pacquiao Mei 2, mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani.
    Jay Msangi ambaye ‘uongo’ sasa unaelekea kuwa silaha yake kubwa kibiashara, alisema pambano hilo la uzito wa Super Bantam ni la mchujo kuwania nafasi ya kupigana katika ulingo mmoja na nyota wa mchezo huo, Mayweather na Pacquiao.
    Lakini uchunguzi wa BIN ZUBEIRY umebaini kwamba, Jay Msangi aliwahadaa mabondia hao na Watanzania- kwani tayari utaratibu mzima kuhusu pambano la Mei 2 mjini Las Vegas ulikwishakamilika mapema.
    Mudi Matumla kushoto akimuadhibu Mchina ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam

    Baada ya Matumla kuwafurahisha Watanzania kama alivyoahidi kwa kumshinda kwa pointi Xin Hua Aprili 27, inaelezwa jitihada za kumtafutia pambano la ubingwa wa dunia zimeanza.
    Gwiji wa ngumi, kiongozi wa PST, bondia mstaafu wa kimataifa, Emmanuel Mlundwa kwa sasa yupo Thailand na moja ya mipango iliyompeleka huko ni kumtafutia Matumla mpinzani katika pambano lijalo.
    Matumla Jr. anaweza kurudi ulingoni mwishoni mwa Mei au mapema Juni, iwapo mipango itafanikisha.    
    Matumla alimtandika Mchina bila ubishi, kwani mtoto wa bingwa wa zamani wa dunia WBU uzito wa Super Middle, alimzidi mpinzani wake mwanzo hadi mwisho katika pambano la raundi 10.
    Na haikuwa ajabu majaji wote watatu, Robert Kasiga, Sakwe Mtulya na Francois Botha walipomshinda Matumla Jr.
    Na baada ya pambano, akasema; “Lilikuwa pambano gumu, lakini ninamshukuru Mungu nimeshinda na kuwafurahisha Watanzania ambao walijitokeza kwa wingi kunisapoti. Ushindi huu ni matokeo ya maandalizi mazuri chini ya kocha wangu, baba yangu (Rashid Matumla),”
    Mayweather kushoto na Pacquiao kulia watapigana Mei 2, mwaka huu mjini Las Vegas, Marekani

    Matumla Jr, mwenye rekodi ya kushinda mapambano 12 kati ya 18, aliyocheza tangu aanze ngumi za kulipwa miaka mitatu iliyopita, akiwa amepoteza mawili, yote kwa pointi na sare nne alimvuruga kwa na makonde mfululizo Mchina siku hiyo tangu raundi kwanza na mpinzani wake huyo akaanza kupunguza kasi ya mchezo kwa kusingizia anapigwa chini ya mkanda.
    Awali, alifanikiwa kumrubuni refa Mtanzania, Emmanuel Mlundwa ambaye alimkata pointi Matumla, lakini janja yake ikashitukiwa kaunzia raundi ya tano na ndipo alipoanza ‘kupigwa kama begi’. 
    Promoja Jay Msangi (katikati), ilibidi awadanganye wananchi ili wamiminike kwa wingi Diamond Jubilee

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUDI MATUMLA KUPANDA ULINGO MMOJA NA MAYWEATHER, PACQUIAO LILIKUWA CHANGA LA MACHO, HUYO NDIYE PROMOTA JAY MSANGI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top