• HABARI MPYA

    Monday, February 23, 2015

    BADI BAKULE ANAPOPONZWA NA MWONEKANO WAKE

    Kuna watu wameumbwa kwa ajili ya mavazi - hata avae kituko cha namna gani bado ataonekana kapendeza, lakini pia wako walioumbwa kinyume chake.
    Badi Bakule ni mmoja wa watu walioumbwa kinyume chake – si aina ya watu wanaopendeza kimavazi hata umpige pamba za bei mbaya kiasi gani bado ataonekana wa kawaida. Hali hiyo imekuwa tatizo kubwa kwa mwimbaji huyu katika bendi nyingi alizopita pengine bila yeye kujijua.
    Mashabiki wengi wamekuwa wakilisema hilo – kwamba Badi ni bonge la mwimbaji lakini mwonekano wake jukwaani unapunguza ladha.

    Badi Bakule ana mapungufu mawili – la kutojipenda ambalo hili linaweza kurekebishika. La pili ni kutopendeza hata pale anapojipenda na kwa hili watu inabidi wamsamehe tu maana kuna vitu vingine ukivichokonoa sana inakuwa kama unahoji kazi ya Mwenyezi Mungu.
    Tukianza kuhoji mtu kukosa mvuto wa sura au umbile jukwaani basi mwishowe tutafikia hatua ya kuhoji uwepo wa wasanii walemavu kwenye majukwaa ya bendi zetu. Mungu atuepushie mbali tusifike huko.
    Mwimbaji bora zaidi wa taarab kuwahi kutokea Afrika Mashariki Siti binti Saad aliyetamba kuanzia mwaka 1911, aliwahi kukutana na kadhia kama hiyo, wapinzani wake wakamkashifu kwa kujaaliwa sura isiyo na mvuto na nyimbo za kumnanga wakamtungia: “Siti binti Saadi kawa mtu lini, Kaja mjini na kaniki chini, Kama si sauti angekula nini?” Ulikuwa ni ujinga wa kupitiliza kutoka kwa wapinzani hao ambao nao wakakutana na majibu yenye hekima kutoka kwake: “Si hoja uzuri, Na sura jamali, Kuwa mtukufu, Na jadi kebeli, Hasara ya mtu, Kukosa akili”. 
    Suala la kutojipenda linaweza kuwa linachangiwa na mambo mengi – kipato kidogo ni mojawapo. Zamani mavazi ya wasanii ilikuwa ni jukumu la bendi, siku hizi msanii anatakiwa ajitose mwenyewe dukani. Kwa mshahara gani? Kwa kipato kipi? Mimi sijui ila tu bado naamini jukumu la msanii kuwa smati jukwaani linapaswa kuanzia kwanza kwa wamiliki wa bendi.
    Badi ni aina ya waimbaji wasiojua kujichanganya kwa watu, si mtu wa kuwa karibu na wafadhili wa bendi au mapedeshee hali inayomfanya aishi kwa kutegemea mshahara tu na hapo ndipo ugumu wa yeye kupigilia pamba za nguvu linapokuwa gumu. Bendi inapaswa kumsaidia kwenye hatua hii.
    Ni kweli kabisa muonekano mzuri ni muhimu kwa msanii hususan anapokuwa jukwaani lakini wakati mwingine huwa najiuliza: “Je kipi ni muhimu zaidi – ubora na uwezo wa msanii au ‘usmati wake jukwaani? 
    Je unapotakiwa kuchagua mmoja kati ya wasanii wawili – mwenye uwezo na ujuzi wa kazi yake lakini hana mvuto dhidi ya msanii smati mwenye mvuto lakini uwezo duni utachagua yupi? Hakika napata kigugumizi.
    Badi Bakule hayupo tena Twanga Pepeta. Mwenyewe ameniambia kuwa kaamua kupumzika kwa muda usiojulikana, uongozi wa Twanga nao unasema umemsimamisha kwa muda usiojulikana kutokana na utoro na utovu wa nidhamu. Najua hizi ni siasa tu kisanii kutoka kwa Badi na mabosi wake lakini habari za chini ya kapeti zinasema mwimbaji huyo amepunguzwa kazi.
    Moja ya sababu za chini kwa chini zinazotajwa ni zile zile za Badi kutokuwa smati pamoja na kukosa mvuto jukwaani.
    Ukitazama kwa haraka haraka kwa waimbaji walioko Twanga Pepeta unaweza ukamkosa wa kulingana na uwezo wa Badi Bakule katika uimbaji na utunzi. Sikiliza vipande vyote alivyotupia Badi Bakule kwenye albam ya “Nyumbani ni Nyumbani” utagundua uwezo wake, wimbo wake wa ‘Mwendapole” ndiyo wimbo bora zaidi katika albam hiyo.
    Ukibahatika kumshuhudia Badi mazoezini utagundua faida nyingine kutoka kwake – anajua kunyoosha nyimbo na kuwaelekeza wenzake, atazungukwa na waimbaji kadhaa wanaohitaji maboresho kutoka kwake. Badi ni aina ya mwimbaji anayehitajika sana kwenye bendi – kama hakufai jukwaani basi atakufaa studio na mazoezini.
    Nimejaribu kupitia nyimbo zote za Badi Bakule kuanzia Tam Tam, TOT hadi Twanga, nimesikiliza kwa makini sana bado sijaona wapi alipoharibu, ni aina ya mwimbaji anayeweza kuendana na kasi ya mabadiliko ya muziki wa dansi lakini kwa bahati mbaya anashindwa kuendana na kasi ya kujipamba katika enzi hizi ambazo watu wanajali zaidi muonekano wa mtu kuliko uwezo wa kazi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BADI BAKULE ANAPOPONZWA NA MWONEKANO WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top