• HABARI MPYA

    Saturday, February 28, 2015

    AZAM KATIKA VITA KWELI SUDAN MBELE YA EL MERREIKH LEO

    Na Mwandishi Wetu, KHARTOUM
    MABINGWA wa Tanzania Bara, Azam FC leo watakuwa katika mtihani mzito mjini Khartoum, Sudan wakati watakapomenyana na wenyeji El Merreikh katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali Kombe la Shirikisho Afrika.
    Mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Merreikh, unatarajiwa kuanza Saa 2:00 Usiku kwa Saa za Afrika Mashariki, ingawa hadi sasa hakuna uhakika wa kuonyeshwa na Televisheni yoyote.
    Merreikh imesema haitaruhusu kamera uwanjani na uongozi wa Azam FC, chini ya Mtendaji wake Mkuu, Saad Kawemba ulikuwa unapambana kuzuia mpango huo, ikiwemo kuwasiliana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
    Kila la heri Azam FC katika mchezo wao na El Merreikh leo Sudan

    Azam FC ilishinda mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam maana yake leo watahitaji sare ili kusonga mbele.
    Kikosi cha Azam FC kilitua Khartoum usiku wa Jumanne na kukumbana na usumbufu wa hapa na pale kutoka kwa wenyeji, mambo ambayo yalilenga kuwavuruga kisaikolojia.
    Waliwekwa kwa muda mrefu Uwanja wa Ndege wakisumbuliwa kwa mambo tofauti ikiwemo kugongewa visa za kuingia nchini humo- na baada ya hapo wakapewa basi chakavu, ambalo walilikataa na kutumia la kwao wenyewe walilokodi.
    Azam FC waliweka kambi katika majengo maalum, si hoteli wakiwa wamesafiri na vyakula na wapishi wao, kuepuka hujuma za wenyeji. Walikuwa wakifanya mazoezi katika Uwanja wa jeshi la nchi hiyo, kabla ya jana kuingia Uwanja wa Merreikh kuujaribu kuelekea mchezo wa leo.
    Wakati wanaingia Uwanja wa Marreikh walipigwa na mayai na mashabiki wa Merreikh pamoja na kuzomewa, lakini kwa kuwa tayari wachezaji wa klabu hiyo wamekwishaandaliwa kisaikolojia, hilo halikuwasumbua.
    Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Kawemba anasema wamejipanga vizuri kwa ajili ya mchezo huo na kila kitu kipo sawa, wakati Kocha Mkuu, Joseph Marius Omog naye anasema vijana wake wako tayari.
    Hakuna majeruhi katika timu na bila shaka mlinda mlango Aishi Manula ataanza pamoja na mabeki, Shomary Kapombe kulia, Erasto Nyoni kushoto, Aggrey Morris na Serge Wawa katikati.
    Safu ya kiungo inatarajiwa kuongozwa na Kipre Michael Balou chini, wakati juu watacheza Frank Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ huku washambuliaji wakiwa ni Didier Kavumbangu, Kipre Herman Tchetche na Brian Majwega.
    Mfungaji wa bao la pili katika mchezo wa kwanza Dar es Salaam, John Bocco anatarajiwa kutokea bechi na leo pia, hiyo ikiwa ni mipango ya kocha Omog kutotumia silaha zake zote za maangamizi kwa wakati mmoja uwanjani. 
    Washambuliaji Mkenya, Alan Watende Wanga na Mmali Mohammed Traore wanatarajiwa kuwa tishio upande wa Marreikh leo, haswa wakicheza mbele ya mashabiki wao leo. 
    Kila la heri Azam FC. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM KATIKA VITA KWELI SUDAN MBELE YA EL MERREIKH LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top