• HABARI MPYA

    Sunday, November 03, 2013

    SIMBA SC INAELEKEA WAPI?

    ZACHARIA Hans Poppe anasema anaipenda sana Simba SC na hayuko tayari kushiriki mpango wowote wa mabadiliko katika uongozi. Lakini yeye ndiye Mwenyekiti wa kundi la Friends of Simba, ambalo haliridhishwi na uongozi wa timu kwa sasa pamoja na benchi la Ufundi.
    Mwenyekiti, ‘Kaka wangu’ Alhaj Ismail Aden Rage kwa kweli ametingwa na majukumu mengi aliyonayo yakiwemo ya kisiasa na ili mambo yawe mepesi Simba SC, lazima watu wa chini yake katika Kamati ya Utendaji na Sekretarieti watekeleze majukumu yao ipasavyo katika kiwango cha ‘A+’.
    Hakuna siri, Hans Poppe anatumia fedha zake nyingi kuisaidia Simba SC  kutokana na mapenzi aliyonayo katika klabu hiyo, lakini kwa msimu wa pili mambo yanakwenda kinyume cha matarajio. Lazima itakuwa inamuumiza.
    Lakini Hans Poppe anapaswa kutambua kwamba, anaumizwa na kitu ambacho kinatokana na matakwa ya nafsi yake. Hana budi kuvumilia, kwanza na pili ufike wakati autazame mara mbili msimamo wake.
    Pale Simba SC pana matatizo. Tena sana. Wachezaji wazuri wanasajiliwa, baada ya muda mfupi wanaonekana hawafai. Waalimu wazuri wanaajiriwa, lakini nao  baada ya muda mfupi wanaonekana hawafai.
    Ilifika wakati msimu uliopita wanachama wakajaribu kutaka kufanya mapinduzi, lakini hawakufanikiwa mbele ya Rage na zaidi aliyekuwa Makamu wake Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ akapeperushwa na upepo wa zoezi hilo kwa kujiuzulu yeye mwenyewe.
    Mamilioni ya wana Simba SC kwa sasa wanaumizwa na mwenendo wa timu yao, lakini watu wasiozidi 40 maarufu kama Makomandoo wanakuwa chanzo cha matatizo ya timu.
    Wanaulinda uongozi ambao unashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo, umeweka maslahi binafsi mbele na haujali kabisa kuhusu ustwati wa timu- sasa hali si  nzuri Simba SC.
    Unaweza kufanya vibaya leo, lakini ukawa na matumaini ya kuzinduka kesho na kufanya vizuri, lakini kwa hali halisi ndani ya Simba SC kwa sasa, ikifanikiwa kushika nafasi ya nne mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, itakuwa kile kitu ambacho watu wanaita; “MIUJIZA”.
    Tanzania ya leo, siyo ile Tanzania ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Tanzania ya leo haina uzalendo tena na watu hawana mapenzi na nchi yao, zaidi kilichobaki wengi wetu kila mmoja ameweka maslahi yake binfasi.
    Unaposema Tanzania, hilo ni jina, lakini Tanzania ni nchi. Na nchi, zaidi ya mipaka yake, ni vitu vilivyomo ndani yake- hivyo basi kama hatutapenda na kujivunia vitu vyetu pamoja na kuvilinda, maana yake tunaibomoa nchi yetu ama kwa kujijua, au kwa kutojijua. 
    Simba na Yanga zina maana kubwa sana katika nchi yetu, pengine ndizo hizo zinasababisha hatupigani kwa makabila au kwa dini zetu, kwa sababu makabila yote, dini zote zinakutakana na kushangilia pamoja katika jezi nyekundu au ya njano.
    Sasa ukiona mtu anataka kuvuruga umoja mkubwa wa Tanzania, huyo haitakii mema nchi yetu. Kama hatutobishana kwa Simba ajili ya Yanga, tubishane kwa dini zetu au makabila?
    Jumatatu wiki hii, mashabiki wa Simba SC walibomoa viti na kufanya fujo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya Kagera Sugar kupata bao la kusawazisha dakika za majeruhi na kupata sare ya 1-1.
    Makocha wa Simba walianza kumfuata mwamuzi wa akiba mapema tu baada  kuonyesha dakika nne za nyongeza wakilalamikia muda huo kuongezwa. Lakini siku hiyo wachezaji zaidi ya watano walianguka uwanjani na kutibiwa hapo hapo, haikuingia machela kutokana na udhaifu wa refa.
    Simba SC haijashinda mechi tangu itoke sare ya 3-3 na wapinzani wa jadi, Yanga wakitoka nyuma kwa 3-0. Baada ya hapo, ilitoka sare ya 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, ikafungwa 2-1 na Azam kabla ya sare ya 1-1 na Kagara.
    Baada ya mechi ile, niliandika wazi, Yanga wangeweza kuifunga Simba SC tena mabao mengi tu, kama si uzembe wa wachezaji wake kucheza mpira wa ‘kibishoo’ baada ya kuwa wanaongoza 3-0.
    Kocha Mkuu wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ aliwatupia lawama wachezaji kwamba, walicheza chini ya kiwango kipindi cha kwanza ili kuipa mabao Yanga- na baada ya kuwatoa kipindi cha li, wakapata sare.
    Siku moja baada ya mechi, wachezaji wawili, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’ na Haroun Chanongo wakapelekwa timu B wakapandishe viwango vyao, lakini ukweli ni kwamba, wameshukiwa kuhujumu timu ndiyo maana wamepewa adhabu hiyo.
    Kinachoonekana hapa, sasa unaweza kuamini viongozi wanawatoa kafara wachezaji ili kujikosha kwa wapenzi wa timu yao- maana yake msimu uliopita pekee wameondolewa wachezaji wengi na muhimu katika timu, wakiwemo ambao walisajiliwa kwa fedha nyingi.
    Jiulize, kutoka kusawazisha mabao matatu kipindi cha pili dhidi ya Yanga hadi kushindwa kulinda bao moja katika mechi na Kagera, hii inakuwaje?
    Lakini mashabiki wa Simba SC waliofanya vurugu katika mechi hiyo, walizingatia na kiwango cha timu yao siku hiyo? Yote kwa yote, mzizi wa haya ni uongozi ambao siwezi kuuita mbovu, bali ambao umeshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Sasa kwa mtaji huu, jiulize Simba inaelekea wapi?      
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC INAELEKEA WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top