• HABARI MPYA

    Thursday, November 28, 2013

    PONDAMALI: IVO NDIYE TANZANIA ONE KIHALALI

    Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
    KOCHA wa makipa wa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, Juma Pondamali ‘Mensah’ amesema kwamba hawajampa ukipa wa kwanza wa timu hiyo Ivo Mapunda kwa sababu ya jina lake, bali uwezo.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana mjini hapa, Pondamali alisema kwamba kwa sasa Ivo ndiye kipa mwenye uwezo mkubwa kushinda wenzake ndiyo maana amepewa mikoba ya kuwa kipa wa kwanza.
    Juma Pondamali akipanga koni jana Uwanja wa Chuo Kikuu cha Strathmore tayari kuwanoa makip wake na chini ni Ivo Mapunda

    Alisema wamekuwa na utaratibu wa kuwaelezea makipa wote takwimu zao baada ya mazoezi ili kujua makosa yao na pia waweze kujirekebisha.
    “Kwa mfano kila baada ya mazoezi tunamueleza kila kipa alichokifanya, alidaka mipira mingapi, mingapi ilimpita na katika takwimu hizo tangu tunajiandaa na mchezo (wa kirafiki wa kimataifa) na Zimbabwe Ivo alikuwa anawazidi wenzake.
    Anayefuatia ni Dida (Deo Munishi), na kwa sababu hiyo hapa tulipo, Ivo ndiye namba moja na Dida namba mbili, Aishi (Manula) yeye ni kipa wa tatu,”alisema.
    Pamoja na hayo, kipa huyo wa zamani wa Yanga SC, amesema makipa wote wana uwezo mkubwa na ikitokea yeyote kati yao akaanzishwa, lango la Stars litakuwa salama tu.
    Makipa bora kabisa; Kutoka kulia Deo Munishi 'Dida', Ivo Mapunda na Aishi Manula

    “Na kwa ujumla ninajivunia hali hii, kidogo sasa hivi tuna makipa wa kutosha kwa ajili ya timu ya taifa, kwa sababu ukiacha hawa ambao tumekuja nao hapa, bado kule nyumbani tumeacha makipa wengine wazuri sana,”alisema.
    Kili Stars inatarajiwa kuanza kampeni zake za kuwania taji la Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge leo kwa kumenyana na Zambia Uwanja wa Machakos katika mchezo wa Kundi B utakaotanguliwa na mechi nyingine kati ya Somalia na Burundi.         
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: PONDAMALI: IVO NDIYE TANZANIA ONE KIHALALI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top