• HABARI MPYA

    Tuesday, October 22, 2013

    MACHUPPA AMUAMBIA KIBADENI; "UMEZIDI KUSAKAMA WACHEZAJI, ZUNGUMZIA SOKA, TATIZO NI VIONGOZI WAKO:

    Na Princess Asia, Dar es Salaam
    MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania na klabu ya Simba SC, Athuman Machuppa ameonekana kukerwa na shutuma za kocha wa klabu yake hiyo ya zamani, Abdallah Kibadeni kwa wachezaji wa timu hiyo na kusema; “zimezidi, inatosha sasa, ongelea soka”. 
    Mshambuliaji huyo aliyehamia Sweden kucheza soka ya kulipwa baada ya kuondoka Simba SC, ameandika kwenye ukurasa wake wa fecebook; “King Kibaden Dah Too Much About Players!!!ongelea soka sio wachezaji tatizo ni viongozi wako ndio chanzo!!!usilaumu wachezaji Only,”.
    Machuppa alikuwa anamaanisha Kibadeni amezidisha kuwashutumu wachezaji na bora sasa aanze kuzungumzia soka, badala ya wachezaji na kwamba tatizo ni viongozi wa klabu.
    Umezidi kusakama wachezaji; Machuppa amemuambia Kibadeni sasa azungumzie soka

    Kauli ya Machuppa inafuatia shutuma za King Kibaden baada ya mchezo dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga SC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambao Simba SC ilitoka nyuma kwa mabao 3-0 hadi mapumziko na kupata sare ya 3-3. 
    Baada ya mchezo wa juzi, kocha wa Kibaden alisema kwamba kambi yao ya kujiandaa na mchezo huo ilivamiwa na vijana wakarubuniwa, ndiyo maana timu yake ilicheza ovyo kipindi cha kwanza na kulala 3-0 kabla ya kuzinduka kipindi cha pili na kupata sare ya 3-3.
    Kibaden alisema kwamba anashukuru kupata sare na anawaheshimu, Yanga kwa kucheza vizuri kipindi cha kwanza na vijana wake kwa kucheza vizuri kipindi cha pili. 
    Hata hivyo, Kibadeni alisema mechi ya juzi ilikuwa ashinde yeye zaidi ya mabao matatu, lakini kwa kuwa kipindi cha kwanza wachezaji wake waliwaachia Yanga mabao matatu, wakamvurugia mipango.
    “Wamewaachia, mimi nasema timu imewaachia wale wamefunga goli tatu. Si timu ya kutufunga goli tatu sisi Yanga namna ile. Lakini waliwaachia. Nikarudi mapumziko nikawaambia sawa, mlitaka kuwaachia tatu, basi zinatosha, mimi niliwaambia hivyo, msiwape nyingi, hizo zinwatosha. Na kweli zimewatosha, tumerudisha goli tatu,”alisema Kibaden na kuongeza; “Wala sijafanya kazi nyingine, nimewaambia tatu mlizowapa wachezaji zinawatosha kwa kutufunga sisi, lakini nyinyi sasa kachezeni mpira,”.  
    “Nachozungumza, tumepata sare mimi nashukuru. Wenzetu walitangulia kipindi cha kwanza, sisi tukazinduka kipindi cha pili, lakini najua, mimi nimezaliwa Tanzania, mpira wa Tanzania naujua, mpira unachezwa ndani, mpira unachezwa nje,”.
    Tatizo ni viongozi; Machuppa amesema tatizo Simba SC ni viongozi

    “Kuna kazi kubwa sana kuangalia watu wanaovamia kwenye kambi zetu, kwenye timu zetu, kutaka kuharibu kuwadanganya watoto, hawa watoto bado wadogo mimi nasema, sasa hivi wanacheza mpira wa kushinikizwa na watu, ndiyo maana unakuta matatizo tunayoyapata haya,”.
    “Sasa wengine hawajui, lakini mimi nazungumza kwamba matatizo yapo, timu mliiona kipindi cha kwanza ilifanya vibaya, lakini si kwa kupenda, nimetoka mapumziko nimeongea maneno machache tu nimebadilisha timu, wale wamekuja kucheza mpira sasa, kwa hiyo nataka muwaelimishe watu, wachezaji kucheza mpira ni kazi yao, wawafurahishe wanachama wao, wawafurahishe wapenzi wao,”. 
    “Sasa wakitumiwa na watu wengine kuja kuvuruga hilo ni tatizo. Sasa kuna vitu mtavisikia baada ya wiki moja au wiki mbili, mimi kila mwenye matatizo natoa, najua mwisho nitapata timu safi, lakini nashukuru matokeo, nawaheshimu Yanga wamecheza mpira mzuri kipindi cha kwanza na mimi nimecheza mpira mzuri kipindi cha pili,”alisema.
    Mzee zungumzia soka; Kibadeni ameambiwa na Machuppa sasa azungumzie soka aache kusakama wachezaji

    Simba SC iliingia kwenye mchezo wa jana ikitokea Bamba Beach Kigamboni, Dar es Salaam ambako imekuwa kambi yake tangu wakati wa maandalizi ya msimu, wakati wapinzani wao, Yanga SC walihamia Pemba kwa ki moja kujiandaa na mchezo huo kutoka makao makuu yao, Jangwani.
    Hadi mapumziko, tayari Yanga walikuwa mbele kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza mawili, lakini kipindi cha Simba SC ikasawazisha kupitia kwa Betram Mombeki, Joseph Owino na Gilbert Kaze.
    Matokeo hayo yanaifanya Simba SC ibakie nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu kwa kutimiza pointi 19, huku Azam FC ikiendelea kuongoza ligi hiyo kwa pamoja na Mbeya City kwa pointi zao 20 kila timu.
    Simba SC iliondoka jana Dar es Salaam kwenda Tanga kwa ajili ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani, kesho.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MACHUPPA AMUAMBIA KIBADENI; "UMEZIDI KUSAKAMA WACHEZAJI, ZUNGUMZIA SOKA, TATIZO NI VIONGOZI WAKO: Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top