• HABARI MPYA

    Friday, October 25, 2013

    AZAM YATOA KIONGOZI WA JUU BODI YA LIGI, TENGA AFUNGUA MOYO KUHUSU UCHAGUZI

    Na Boniface Wambura, Ilala
    HAMD Yahya Juma wa Mtibwa Sugar ndiye Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Ligi Tanzania (Tanzania Professional League- TPL Board) baada ya kushinda katika uchaguzi uliofanyika leo mchana (Oktoba 25 mwaka huu) kwenye ukumbi wa mikutano uliopo Golden Jubilee Tower, Dar es Salaam.
    Juma ambaye hakuwa na mpinzani alipata kura zote kumi za ndiyo zilizopigwa na klabu za Ligi Kuu zilizohudhuria mkutano huo. Klabu ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni JKT Ruvu, Mgambo Shooting, Coastal Union na Rhino Rangers.
    Sheikh Said Muhammad Said Abeid, Makamu Mwenyekiti Bodi ya Ligi Kuu

    Naye Sheikh Said Muhammad Said Abeid ambaye pia hakuwa na mpinzani amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti kwa kupata kura zote za ndiyo.
    Kwa upande wa wajumbe wawili wa Kamati ya Uendeshaji, wote Kazimoto Miraji Muzo wa Pamba na Khatib Omari Mwindadi wa Mwadui wameshinda kwa kura zilizopigwa na klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL).
    Muzo alipata kura 15 za ndiyo wakati mbili zikimkataa, huku Mwindadi akipata kura 16 na moja ilimkataa. Klabu za FDL ambazo hazikuhudhuria uchaguzi huo ni Transit Camp, Burkina Faso, Polisi Mara, Stand United, Toto Africans, Polisi Tabora na Kanembwa JKT. wakati huo huo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) anayemaliza muda wake, Leodegar Tenga amesema amefurahishwa na jinsi kampeni za uchaguzi zinazokwenda kutoka na ukweli kuwa wagombea wamekuwa wakielezea kile wanachotaka kuufanyia mpira wa miguu.
    Akizungumza na Waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF leo mchana, Rais Tenga ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) amesema Watanzania wanataka kusikia ajenda za wagombea.
    “Ombi langu ni kwamba kampeni zimeanza vizuri, watu wanazungumza hoja zaidi. Ni jukumu la wajumbe kupima na kufanya uamuzi. Kwangu mimi nimejitayarisha kumkabidhi Katiba, Rais mpya wa TFF,” amesema.
    Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) amesema kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wake ni kujenga taasisi (TFF) pamoja na kuweka mifumo (structure) inayoainisha majukumu ya kila mmoja.
    “Ajenda yetu wakati tunaingia madarakani mwaka 2005 ilikuwa ni kujenga taasisi. Tayari taasisi ipo, sasa mtazamo uwe kuushughulia mpira wa miguu wenyewe,” amesema.
    Mkutano Mkuu wa TFF unafanyika kesho kwenye ukumbi wa mikutano wa NSSF Waterfront, na tayari wajumbe wa mkutano huo ambao pia utakuwa na ajenda ya uchaguzi siku inayofuata wameshawasili jijini Dar es Salaam.
    Wawakilishi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Ashford Mamelodi ambaye ni Ofisa Maendeleo wa kanda hii, Magdi Shams El Din ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CAF na Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) ni miongoni mwa wageni watakaohudhuria mkutano huo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YATOA KIONGOZI WA JUU BODI YA LIGI, TENGA AFUNGUA MOYO KUHUSU UCHAGUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top