• HABARI MPYA

    Thursday, October 31, 2013

    MABOMU YAMALIZA MECHI YA SIMBA NA KAGERA TAIFA...1-1 HALAFU VITA POLISI NA MASHABIKI MSIMBAZI

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    UWANJA wa Taifa, Dar es Salaam leo uligeuka eneo la vita baina ya Polisi mashabiki wa Simba SC, kufuatia Kagera Sugar kupata bao la kusawazisha dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia kwa dakika 90 za mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, timu hizo zikitoka 1-1.
    Baada ya Salum Kanoni kukwamisha nyavuni mkwaju wake wa penalti, mashabiki wa Simba waliokuwa viti vya Rangi ya Bluu na Chungwa, walianza kung’oa viti na kuvitupia uwanjani.
    Wengine wanang'oa viti, wengine wanakimbia kuokoa maisha yao...hivi ndivyo ilivyokuwa Uwanja wa Taifa leo

    Mara moja, Polisi walianza kupambana na mashabiki hao kwa kuwatupia mabomu ya machozi, ndipo wakaanza kukimbia. Makocha na wachezaji wa Simba kwa pamoja waliwafuata waamuzi kuwalalamikia- hali ambayo ilifanya watolewe kwa kusindikizwa na Polisi.
    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Mohamed Theofile wa Morogoro aliyesaidiwa na Said Mnonga na Charles Chambea wote wa Mtwara, ambao walishindwa kuumudu kabisa, hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0.
    Salum Kanoni akishangilia na Themi Felix kulia baada ya kuisawazishia Kagera


    Ramadhani Singano kulia na William Lucian kushoto wakimpongeza Tambwe baada ya kufunga bao la Simba

    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Amisi Tambwe dakika ya 45 baada ya kupokea pasi nzuri ya Betram Mombeki na kumpiga chenga beki Salum Kanoni, kabla ya kumchambua kipa Hannington Kalyesebula.
    Kagera ilipata pigo mapema dakika ya 22 kipa wake Agathon Anthony kuumia katika harakati za kuzuia shambulizi la Tambwe na nafasi yake ikachukuliwa na Mganda, Kalyesebula.   
    Kwa ujumla timu zote zilishambuliana kwa zamu kipindi cha kwanza, ingawa Simba SC ndiyo waliotengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga.
    Kipindi cha pili, Simba SC iliendelea kusukuma mashambulizi mengi langoni mwa Kagera, lakini washambuliaji wake walikosa umakini wa kutumia nafasi.
    Kagera nayo iliendelea kushambulia na kwa ujumla mchezo ulizidi kunoga kadiri muda ulivyokuwa ukisonga mbele kutokana na ushindani mkali.
    Wakati refa wa akiba, Hussein Kalindo wa Kinondoni, amekwishaonyesha dakika nne za nyongeza, Kagera ikafanya shambulizi langoni mwa Simba na Daudi Jummane akaangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Simba SC, Joseph Owino na refa akaamuru penalti.
    Beki wa zamani wa Simba SC, Salum Kanoni akaenda kumchambua vizuri kipa Abuu Hashimu kuisawazishia Kagera dakika ya 90+2.
    Simba SC; Abuu Hashim, Nassor Masoud ‘Chollo’, Issa Rashid, Joseph Owino, Hassan Khatib, Jonas Mkude, Ramadhani Singano, Said  Ndemla, Betram Mwombeki, Amisi Tambwe na William Lucian.
    Kagera Sugar; Agathon Anthony/Hannington Kalyesebula dk22, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Ernest Mwalupani, Malegesi Mwangwa, Zuberi Dabi/Juma Mpola dk46, Benjamin Asukile/Adam Kingwande dk46, George Kavilla, Themi Felix, Daudi Jumanne na Paul Ngwai.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MABOMU YAMALIZA MECHI YA SIMBA NA KAGERA TAIFA...1-1 HALAFU VITA POLISI NA MASHABIKI MSIMBAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top