• HABARI MPYA

    Wednesday, October 30, 2013

    HIZI NI CHANGAMOTO ZA AWALI KWA UTAWALA WA MALINZI TFF

    MASHABIKI wa Mbeya City wamerudia tena kufanya vurugu, kupiga, kujeruhi na kuharibu mali jana katika mchezo dhidi ya wapinzani wao wa Jiji la Mbeya, Prisons Uwanja wa Sokoine mjini humo.
    Imeripotiwa wachezaji wa Prisons wamefanyiwa fujo, basi limepasuliwa vioo na baadhi ya mashabiki wamejeruhiwa na mashabiki wa Mbeya City.
    Mwezi uliopita mashabibiki wa timu hiyo walifanya mambo kwa hayo kwa Yanga, walipasua kioo basi la timu hiyo na kumjeruhi dereva wake katika mechi baina ya timu hizo. 

    Tukio la jana linakuwa tukio la tatu kubwa la vurugu katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya awali mashabiki wa Yanga kushambulia basi la Coastal Union, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kujeruhi mmoja wa wachezaji wa timu hiyo.
    Baada ya vurugu za kwenye mchezo wa Yanga na Coastal na Union, Kamati ya Ligi Kuu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliitoza Yanga faini ya Sh. Milioni 1, yaani Sh. 500,000 kwa kila kosa, kutokana na washabiki wake kuwarushia waamuzi chupa za maji baada ya Coastal Union kusawazisha bao katika mechi hiyo na kuwarushia chupa waamuzi hao wakati wakirejea vyumbani baada ya pambano hilo.
    Suala la kushambuliwa kwa basi la Coastal halikuchukuliwa hatua na sababu hazikuelezwa. 
    Ajabu kocha wa makipa wa Coastal Union, Juma Pondamali aliyewakejeli tu mashabiki Uwanja wa Taifa, alipewa adhabu kubwa kuliko Yanga SC, kwa kupigwa faini ya Sh. Milioni 1 na kufungiwa miezi mitatu.
    Marefa waliochezesha mechi hiyo, Martin Saanya na msaidizi wake namba moja, Jesse Erasmo nao wamefungiwa mwaka mmoja kila mmoja kwa kutoimudu mechi hiyo.
    Baada ya yaliyotokea katika mchezo wa Yanga na Coastal niliandika; Samaki mkunje angali mbichi na ni bora kuchukua tahadhari kabla ya hatari. TFF, imekuwa ikinyamazia matukio yenye dalili za kuleta athari kubwa zaidi mbele, jambo ambalo hakika si zuri.
    Haikuwa mara ya kwanza kwa mashabiki wa Yanga kufanya fujo uwanjani na kusababisha uharibifu wa mali na hata kujeruhi na kwa ujumla kuhatarisha amani. Wenye soka yao, FIFA wanauita mchezo wa kiungwana- hawataki uhuni hata kidogo na TFF kama wasimamizi wakuu wa soka nchini, wanapaswa kulizingatia hilo.
    Lakini tatizo kubwa, TFF wanashindwa kuchukua adhabu ambazo zitakuwa fundisho kwa mashabiki wa Yanga na wengine wote, kwa sababu wameweka mbele fedha kuliko utu na thamani ya mchezo wenyewe.
    Nilisema, wakati umefika sasa, Yanga ipewe adhabu ya kucheza mechi bila mashabiki uwanjani, japo mechi tatu tu na bila shaka baada ya kukosa fedha, viongozi wake wataona umuhimu wa kuwasihi mashabiki wao wawe wastaarabu. Lakini kama tutaendelea na ile desturi ya faini Sh. 500,000 na kutakiwa kufidia gharama za uharibifu na tiba za waliojeruhiwa, hakika iko siku litakuja kutokea kubwa.
    Nilisema, ni wazi kama tunataka kuivusha soka yetu katika hatua nyingine, lazima kwanza tukubali kujivua ushabiki na kuchukua hatua ambazo moja kwa moja zitalenga maslahi na ustawi wa mchezo huu nchini. Wakati umefika sasa, tuondoe dhana kwamba Simba na Yanga haziwezi kupewa adhabu kali, kisa ni timu kubwa na zinazalisha mapato mengi. Si sahihi.
    Sasa matokeo yake na mashabiki wa mikoani nao wanaiga vurugu, tena wanazifanya kisawasawa na kuhatarisha amani kabisa. Bado najiuliza, kama mashabiki wa Yanga baada ya vurugu zote walizofanya dhidi ya Coastal, timu yao ingepewa adhabu ya kucheza bila mashabiki japo mechi moja tu, je na mashabiki wa Mbeya City jana wangefanya walichokifanya? 
    Mfano mdogo tu; wakati fulani mashabiki wa Ashanti walifanya vurugu katika mechi dhidi ya Yanga SC na wakafungiwa kucheza Uwanja wa Taifa na sasa timu yao imerejea Ligi Kuu wamekuwa na nidhamu ya hali ya juu, wakikumbuka adhabu waliyowahi kupata. 
    Sasa Mbeya City warudia tena jana, kwa sababu hata tukio la kwanza hawakupewa adhabu ya kuwafanya waogope kufanya hivyo tena. Vema mwishoni mwa wiki soka ya Tanzania imepata viongozi wapya, chini ya Jamal Malinzi (Rais) na hizi zinakuwa changamoto za awali kwao.
    Inaweza kuchukuliwa kama changamoto ndogo, lakini ukweli ni kwamba hii ni changamoto kubwa, ambayo kwa hakika chini ya utawala mpya wa Malinzi vema ikafanyiwa kazi na kupatiwa suluhisho la kudumu, ili soka iendelee kuwa mchezo wa amani na kujenga urafiki. Kila la heri.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HIZI NI CHANGAMOTO ZA AWALI KWA UTAWALA WA MALINZI TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top