• HABARI MPYA

    Monday, June 03, 2013

    YANGA WAANZA MAFUNZO YA 'VITA YA DARFUR' LEO MABIBO

    Mabingwa; Yanga baada ya kupewa Kombe lao Mei 18
    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 3, 2013 SAA 12:05 ASUBUHI
    MABINGWA wa soka Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC wanatarajiwa kuanza mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam baada ya mapumziko mafupi kufuatia kumaliza msimu.
    Yanga ambayo iliufunga msimu vizuri kwa ushindi wa 2-0 Mei 18, mwaka huu dhidi ya watani wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo itakuwa inaanza maandalizi ya msimu mpya.
    Hata hivyo, katika mazoezi ya leo, Yanga SC itawakosa wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza, ambao wapo kwenye timu zao za taifa.
    Hao ni kipa Ally  Mustafa ‘Barthez’, mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, viungo Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Athuman Iddi ‘Chuji’ walio Taifa Stars ya Tanzania. Wengine ni Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite walio katika timu ya taifa ya Rwanda, wakati Hamisi Kiiza aliye na Uganda, amemaliza mkataba wake na mustakabali wake bado haujawekwa wazi katika klabu hiyo. 
    Kiiza alishindwa kufikia makubaliano na uongozi wa Yanga kuhusu mkataba mpya na akaondoka bila kusaini wiki iliyopita.
    Kocha Mholanzi, Ernie Brandts alitarajiwa kuwasilia jana baada ya mapumziko, lakini hata kama atakuwa hajafika, Kocha Msaidizi, Freddy Felix Minziro ataongoza mazoezi.
    Majukumu ya kwanza ya Yanga katika msimu mpya ni kwenda kutetea taji lao la Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, nchini Sudan kuanzia Juni 18 mwaka huu.
    Yanga ambao ni mabingwa mara mbili mfululizo wa Kagame, wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda
    Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 18 hadi Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
    Mabingwa watetezi, Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAANZA MAFUNZO YA 'VITA YA DARFUR' LEO MABIBO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top