• HABARI MPYA

    Wednesday, June 19, 2013

    TATIZO KIM POULSEN AMETUTAMANISHA YALIYO NJE YA UWEZO WETU KWA SASA

    IMEWEKWA JUNI 19, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
    MARA tu alipopewa majukumu ya kuwa kocha wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars Mei mwaka jana, kocha Mdenmark kim Poulsen alisema dira yake ni kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2015.
    Alisema hivyo wakati anaelekea kwenye kampeni za kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani Brazil na pia Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika za mwaka huu.
    Wakati anasema hayo, Poulsen aliyerithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen alionekana kama anayetufariji tu, kwani Watanzania wengi tulikuwa tumekwishajikatia tamaa na soka yetu, tukiamini ni ya hapa hapa tu.

    Jumapili, Taifa Stars ilifungwa mabao 4-2 na Ivory Coast katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya Brazil mwakani na kupoteza matumaini ya kukata tiketi hiyo.
    Huo ulikuwa mchezo wa kwanza kwa Stars kufungwa nyumbani kwenye Kundi hilo chini ya Kim, baada ya awali kushinda mechi mbili nyumbani, 2-1 dhidi ya Gambia na 3-1 dhidi ya Morocco.
    Ivory Coast sasa wamesonga hatua ya mwisho katika kuwania tiketi ya Brazil mwakani, ambako watamenyana na mmoja wa washindi wengine wa makundi mengine tisa, kusaka nafasi hiyo baada ya kufikisha pointi 13, ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote Kundi C, zikiwa zimebaki mechi moja moja kwa kila timu.
    Lakini baada ya mzunguko wa kwanza Tanzania ikimaliza katika nafasi ya pili kwa pointi zake sita, ikizidiwa kwa pointi moja tu Ivory Coast matumaini ya kwenda Brazil yalikuwa juu kwa Watanzania.
    Yalikuwa juu kwa sababu mbili au tatu kubwa, kwanza ni maendeleo ya timu siku hadi siku tangu Kim aanze kazi, kiwango cha timu kwa ujumla ikiwemo na uwezo wa wachezaji mmoja mmoja, pamoja na matokeo mazuri dhidi ya Morocco katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa kundi hilo.
    Wakati Tanzania inaingia kwenye mchezo dhidi ya  Morocco, wananchi walikuwa hawaamini kama timu yao inaweza kushinda, zaidi kwa kiasi kikubwa walitarajia japo sare, lakini timu ikapata ushindi mnono sambamba na kucheza soka nzuri, kuliko wapinzani wao.
    Na kwa kurejea matokeo ya michezo iliyotangulia nyumbani kuzifunga mfululizo Kenya, Zambia, Gambia na Cameroon imani ilijengeka kwamba uwezo wa timu yetu sasa ni wa kuridhisha na kwenda Brazil inawezekana.
    Tukasahau kuhusu dira ya Kim kwamba ni kucheza AFCON 2015 na tukajenga matumaini makubwa na Fainali za Brazil mwakani.
    Lakini kufungwa mechi mbili mfululizo za Kundi hilo 2-1 dhidi ya Morocco ugenini na 4-2 dhidi ya Ivory Coast Jumapili, kumezalisha hisia tofauti kuhusu timu yetu, na kwa kiasi kikubwa watu sasa wanazungumzia mapungufu ya timu na si udhaifu tena.
    Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwanaspoti ameandika jana kwamba tunahitaji wachezaji watano wanaocheza Ligi Kuu za Ulaya ili kuzifunga timu kama Ivory Coast na wengine wengine kati ya wachambuzi wetu wameandika maoni yao kuhusu timu, lakini si tofauti sana katika mawazo ya jumla.
    Wengi wanaamini tulifungwa na timu ambayo ilitizidi uwezo na uzoefu na tunahitaji kukuza uwezo wetu uzoefu pamoja. Mtu mmoja tu aliniacha hoi kwa pumba zake, aliishutumu Kamati ya Ushindi iliyoundwa eti ilishindwa kufanya kazi yake, ndiyo maana marefa walitoa maamuzi ya kama kutotutendea haki Morocco na Dar es Salaam Jumapili.
    Kila mtu ana upeo wake katika masuala ya soka kwa ujumla, lakini kikubwa ni kujitambua na kutambua katika kuielezea soka kisayansi zaidi badala ya kufikiria fitina zituvushe popote. Ni kupotosha watu wanaokusoma na kuwajaza fikra mbovu Watanzania.
    Mawazo kama hayo unaweza kuzungumzia baa na walevi wenzako, lakini si kwenye gazeti lenye heshima zake- watu wanataka kusoma sababu za msingi za kufungwa katika michezo tuliyotarajia kushinda na kupata maoni yako mbadala nini kingefanyika kuepuka matokeo yaliyotokea. 
    Mechi zote mbili zilizopita za Kundi C tulifungwa kwa sababu ya kujiamini tunaweza kushindana na yoyote bila woga na kuachana na ule mchezo wa kujihami zaidi tukitegemea kufunga kwa mabao ya mashambulizi ya kushitukiza.
    Mechi zote tano ambazo Kim alishinda mfululizo nyumbani dhidi ya Gambia, Kenya, Zambia, Cameroon na Morocco alikuwa anaanzisha mshambuliaji mmoja na kulundika viungo wengi- lakini baada ya hapo akawa anatumia mfumo wa kushambulia zaidi na kupunguza kujihami, unaweza kusema alikuwa anatengeneza uwiano sawa katika timu kuanzia ulinzi hadi kushambulia. 
    Na hiyo ilitokana na yeye pia kujiamini juu ya maendeleo ya kazi yake na taratibu akawa anajaribu mambo zaidi na mengi ndiyo yaliyomuangusha- kwa mfano Jumapili baada ya kuona yupo nyuma kwa mabao 3-2 hadi dakika ya 85, akamtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza winga Vincent Barnabas kwa lengo zuri tu kuongeza kasi ya mashambulizi, lakini matokeo yake timu ikafa tukafungwa bao la nne.    
    Mechi ya Jumapili ingeweza kwisha kwa sare ya 2-2 kama si madudu ya refa kuwapa penalti ya utata Ivory Coast na pia Kim kutofanya mabadiliko yaliyomuangusha dakika za lala salama.
    Wengine wanasema mabeki wa pembeni ni tatizo, kwa nini Shomary Kapombe achezeshwe kushoto wakati ni kiungo, hakuna mabeki?
    Wengine wanasema Erasto Nyoni ni uchochoro, lakini hawawazungumzii aina ya wachezaji wanaokabiliana nao ubora wao ukoje. Lakini yote haya yanakuja kwa sababu, ya kazi nzuri ya Kim mwenyewe, kututengezea timu bora ya ushindani.
    Kutoka tuliojikatia tamaa kwamba hatuwezi hata kucheza AFCON 2015 hadi kulia kilio cha kusaga meno kwa kukosa tiketi ya Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil- dhahiri kuna kazi Kim ameifanya.
    Tumefungwa 4-2 na Ivory Coast, lakini kesho Stars ikiingia uwanjani hata na Nigeria, watu wataitikia kwa wingi, kwa sababu tayari wana imani na timu na kocha pia, kwamba siku hadi siku inaimarika.
    Wakati Ivory Coast wanakwenda kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 Afrika Kusini walipita hapa tukacheza nao mechi ya kirafiki wakatufunga bao 1-0, lililotiwa kimiani na Didier Drogba. Lakini ukirejea mechi hiyo ya kufungwa 1-0 na iliyopita ya Jumapili ya kufungwa 4-2, unaona kabisa ni Juni 16, 2013 ndiyo tulicheza soka nzuri ya kusisimua na ya ushindani.
    Kufungwa mabao mengi hakumaanishi udhaifu, wakati mwingine ni mipango tu kukataa. Rejea mchezo wa juzi, Kim alimtoa Mwinyi akataka abakize viungo watatu katikati, Amri Kiemba, Frank Domayo na Salum Abubakar ili Barnabas akawasaidie Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta kushambulia, lakini ikawa tofauti timu ikafungwa bao la nne.   
    Mengi tunayoyazungumza na kujadili leo kuhusu Stars ni kwa sababu Kim amefanya kazi nzuri ya kuboresha kiwango cha timu, kiasi cha kututamanisha hata yale ambayo bado yako nje ya uwezo wetu, kama kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani. Tukijaaliwa Jumapili Inshaallah. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TATIZO KIM POULSEN AMETUTAMANISHA YALIYO NJE YA UWEZO WETU KWA SASA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top