• HABARI MPYA

    Monday, June 03, 2013

    KOCHA YANGA AKWAMA ULAYA, TIMU YAANZA KUJIFUA CHINI YA MINZIRO MABIBO

    Yanga SC
    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JUNI 3, 2013 SAA 8:00 MCHANA
    MABINGWA wa soka Tanzania Bara na Afrika Mashariki na Kati, Yanga SC leo asubuhi wameanza mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam baada ya mapumziko mafupi kufuatia kumaliza msimu.
    Yanga ambayo iliufunga msimu vizuri kwa ushindi wa 2-0 Mei 18, mwaka huu dhidi ya watani wa jadi, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeanza maandalizi ya msimu mpya bila ya Kocha wake Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts.
    Beki huyo wa kimataifa wa zamani wa Uholanzi alikosa ndege ya kumleta Dar es Salaam jana kutoka kwao, Uholanzi na sasa anatarajiwa kuwasili kesho usiku.
    Katika mazoezi ya leo, Yanga SC imewakosa wachezaji wake wengi wa kikosi cha kwanza, ambao wapo kwenye timu zao za taifa.
    Hao ni kipa Ally  Mustafa ‘Barthez’, mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, viungo Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Athuman Iddi ‘Chuji’ walio Taifa Stars ya Tanzania. Wengine ni Haruna Niyonzima na Mbuyu Twite walio katika timu ya taifa ya Rwanda, wakati Hamisi Kiiza aliye na Uganda, amemaliza mkataba wake na mustakabali wake bado haujawekwa wazi katika klabu hiyo. 
    Kiiza alishindwa kufikia makubaliano na uongozi wa Yanga kuhusu mkataba mpya na akaondoka bila kusaini wiki iliyopita.
    Kutokana na kutokuwepo kwa Brandts, mazoezi ya Yanga leo yaliongozwa na Msaidizi wake, Freddy Felix Minziro aliongoza mazoezi.
    Majukumu ya kwanza ya Yanga katika msimu mpya ni kwenda kutetea taji lao la Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame, nchini Sudan kuanzia Juni 18 mwaka huu.
    Yanga ambao ni mabingwa mara mbili mfululizo wa Kagame, wamepangwa Kundi C katika michuano hiyo pamoja na Ports ya Djibouti, Express ya Uganda na Vital 'O' ya Burundi, wakati wapinzani wao wa jadi, Simba SC wamepangwa Kundi A pamoja na wenyeji El-Mereikh, Elman  ya Somalia na APR ya Rwanda
    Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Juni 18 hadi Julai 2, mwaka huu mjini Khartoum, Sudan, mabingwa wa Kenya, Tusker wamepangwa Kundi B pamoja na wenyeji wengine, Al-Hilal, Falcons ya Zanzibar, Al Ahly Shandy ya Sudan na Al-Nasir Juba ya Sudan Kusini.
    Mabingwa watetezi, Yanga wataanza kampeni zao za kutetea taji hilo Juni 20 kwa kumenyana na Express, wakati Simba SC itashuka dimbani Juni 21 kufungua dimba na El-Mereikh, na mechi zote zitachezwa Elfashar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: KOCHA YANGA AKWAMA ULAYA, TIMU YAANZA KUJIFUA CHINI YA MINZIRO MABIBO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top