• HABARI MPYA

    Friday, December 11, 2020

    WAZIRI MPYA WA MICHEZO, BASHUNGWA AAHIDI KUENDELEZA MAZURI YOTE YA DK. MWAKYEMBE

    Na Shamimu Nyaki – WHUSM, DODOMA
    WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema kwamba mambo yote mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake, Dk. Harrison Mwakyembe katika sekta anazozisimamia atayaendeleza ili matarajio ya kuundwa kwa kwa Wizara hiyo yafikiwe.
    Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 11, 2020 wakati akipokea Ofisi kutoka kwa Waziri mstaafu Dkt. Harrison Mwakyembe ambapo ameeleza kuwa ataendelea kushauriana na naye katika masuala mbalimbali ya wizara hiyo kutokana na uzoefu aliyonao, huku akisitiza kuwa mahusiano mazuri na watu katika maeneo mbalimbali ya kazi na jamii ni muhimu kwa sababu manufaa mengi.
    “Tulishirikiana na wewe katika kuhamisha Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara kuja wizara hii,nimatumaini yangu tutaendelea kushirikiana katika sekta zote za wizara hii”, alisema Mhe. Bashungwa.
    Akiendelea kuzungumza Waziri Bashungwa alisema kuwa tayari ameaviagiza Vyama vya Michezo kuwasilisha mpango mkakati wa namna ya kuendesha michezo nchini, huku akisisitiza suala la Makampuni ya Michezo ya Kubahatisha kuchangia katika ustawi wa Timu za Taifa.


    Aidha,Mhe.Bashungwa ameiagiza Bodi ya Filamu Tanzania kuona namna ya kuanzisha mfumo ambao utatumika kuuza kazi za filamu kwa mfumo wa kidigitali kama ilivyo ‘Netflix’ kwani itasaidia wasanii kusambaza kazi zao kwa urahisi na pia kuchangia katika pato la taifa ambapo alisisitiza kuwa “Msanii kiwanda chake ni kichwa chake”.
    Naye Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega alisema kuwa jambo la kuwa na Shule za Michezo (Sports Academy) ni jambo la msingi ambalo uongozi wao utalifanyia kazi na kuweka mkazo katika michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA ili timu ya taifa itokane na vijana hao.
    “Tumejipanga kuhakikisha tunalinda Utamaduni wa Taifa Letu, vijana tunaowajibu wa kuhakikisha tunu za nchi pamoja na maadili ya nchi yetu tunayalinda, na katika sekta ya Sanaa tunatambua Sanaa ni ajira hivyo tutasaidia kuikuza”,alisema Mhe.Ulega.
    Awali akiwakaribisha viongozi hao Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi alisema kuwa katika kipindi cha uongozi wa Dkt. Mwakyembe kumekuwepo na mafanikio mengi ikiwemo ongezeko la Bajeti pamoja na utatuzi wa changamoto mbalimbali zilizokuwepo katika wizara hiyo.
    Katika ufafanuzi wake Dkt. Abbasi alisistiza kuwa Dkt.Mwakyembe alisimamia vyema sekta ya Habari ambapo alihakikisha Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016, inafuatwa pamoja na Kanuni zake ambapo alisisitiza kuwa sekta ya habari ni taaluma na vyombo vya habari vina haki na wajibu.
    “Katika uongozi wako Dkt.Mwakyembe ulifanya mambo mengi, ulitatua mgogogo kati ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na Kampuni ya Startimes ambao uliyokuwa umedumu kwa muda mrefu, umeongoza kuanzishwa kwa Tanzania Safari Chaneli, umefanya maboresho makubwa katika shirika hilo ikiwemo kuanzishwa kwa kipindi cha Aridhio, umesimamia sekta ya michezo kwa kutunga Kanuni za Baraza la Michezo la Taifa pamoja na kuunda Kamati ya Kusimamia Haki za Wasanii”,alisema Dkt.Abbasi.
    Kwa upande Waziri huyo aliyemaliza muda wake Dkt.Harrison Mwakyembe amewashauri viongozi hao kutambua umuhimu wa kuundwa kwa Wizara hiyo tangu enzi za Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere ambapo lengo lilikuwa ni kulinda historia ya nchi.
    Dkt. Mwakyembe amesema kuwa wizara hiyo ina Sekta ya Utamaduni ambayo ni kiini na roho ya taifa kwa kuwa inaeleza mambo mbalimbali ya taifa ikiwemo lugha ya Kiswahili, umuhimu wa Wimbo wa Taifa ambapo ni lazima kuimbwa shuleni kila siku na kwenye  shughuli mbalimbali za kitaifa ambapo Sera ya Utamaduni ya Mwaka 1997 imeeleza kuwa ni  jambo hilo ni la lazima.
    Vilevile Dkt.Mwakyembe amesema kuwa sekta ya habari inatambulika katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa, wananchi wana haki ya kupata taarifa na habari sahihi na sekta ya michezo na Sanaa zinatoa fursa kwa vijana ikiwemo kujiajiri hivyo ni muhimu zikaendelea kuendelezwa.
    Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa amesema Wizara hiyo ni msingi wa kulinda historia, mila na desturi za nchi pamoja na kuhakikisha sekta zake zinachangia katika kukuza pato la taifa, ambapo amesisitiza kuwa sekta ya Michezo ina wajibu wa kuhakikisha inafanya vizuri ndani na nje ya nchi hivyo amewataka wataalamu wa Sekta hizo kuongeza ubunifu katika kutekeleza majukumu yao.
    Bashungwa ameyasema hayo leo Desemba 10,2020 katika kikao na Menejimenti ambayo ilijumuisha Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi  zilizo chini ya wizara hiyo ambapo amesema ni jukumu la kila Idara na Taasisi kuwa na mtazamo chanya na kubuni njia mbalimbali za kitaalamu zitakazosaidia kutatua changamoto zilizopo katika sekta zao lengo likiwa ni kukidhi maatarajio ya kuundwa kwa Wizara hiyo.
    "Ni lazima tuangalie namna ya kuchangia katika pato la taifa, pamoja na kuboresha makusanyo ya Mirabaha, Sekta ya Michezo leteni suluhisho la changamoto ambazo nyinyi wataalamu mnaona zitasaidia kuboresha sekta hii" alisema Bashungwa.
    Mhe.Bashungwa ameongeza kuwa mkakati wa Serikali ni kuhakikisha Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) linasikika nchi nzima, hivyo fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha usikivu zitumike ipasavyo, huku akisisitiza Chama cha Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kuendelea kutatua kero za wadau wake ili wanufaike na kazi zao.
     Naye Naibu Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amewaagiza wajumbe hao wa menejiment ya Wizara na Wakuu wa Taasisi kuangalia Sera zote zilizopo kama zinaendana na wakati uliopo na zinakidhi matakwa ya wadau wao na nchi katika kuendeleza sekta hizo.
    Mhe.Ulega amesisitiza viongozi hao kuwa katika kulinda na kuendeleza maadili ya Kitanzania, mila na desturi za jamii  ni vyema kuwatumia viongozi wa dini ambao wanahudumia jamii kiimani, kimaadili na kielimu, Huku akihimiza Sekta ya michezo kuwa ina wajibu wa kutumia michezo ya UMITASHUMTA na UMISETA kuibua vipaji  vitavyosaidia kuzalisha wanamichezo nchini.
    Kwa upande wake Katibu Mkuu Wa Wizara na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa Miondombinu ya michezo inaendelea kuboreshwa huku akieleza kuwa Uwanja wa Dodoma umefikia hatua nzuri ambapo hatua ya awali ikiwemo mchoro kwa ajili ya ujenzi wa uwanja huo imekamilika.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZIRI MPYA WA MICHEZO, BASHUNGWA AAHIDI KUENDELEZA MAZURI YOTE YA DK. MWAKYEMBE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top