• HABARI MPYA

    Friday, December 18, 2020

    WAZIRI MPYA WA MICHEZO, BASHUNGWA ASEMA WANATAKA KUIIMARISHA BMT ILI IVISIMAMIE VYEMA VYAMA VYA SEKTA HIYO

    Na Shamimu Nyaki – WHUSM
    WAZIRI mpya wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema kwamba atahakikisha analiimarisha Baraza la Michezo la Taifa (BMT) katika kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuendeleza michezo nchini ikiwemo kuvisimamia vyema Vyama vya Michezo.
    Mhe. Bashungwa ameyasema hayo Desemba 18, 2020 Jijini Dar es Salaaam wakati alipofanya ziara pamoja na Naibu wake Mhe. Abdallah Ulega katika Baraza hilo ambapo amesema Sheria zote ambazo zinahitaji kufanyiwa maboresho zitawasilishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa maboresho yanayohitajika.
    “BMT lazima msimamie ustawi wa timu zetu za Taifa, ni lazima turudi katika misingi ya Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISETA ambayo yanaibua vipaji vingi, nasisitiza timizeni wajibu wenu mliopewa kisheria bila kumuonea mtu”, alisema Mhe.Bashungwa.


    Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashugwa akizungumza na Watendaji wa BMT alipofanya ziara katika Baraza hilo 

    Kwa upande wake Mhe. Naibu wa Waziri wa wizara hiyo Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa BMT lazima ifanye mapinduzi katika kuendeleza michezo yote kwakua michezo inaleta ajira, inakuza uchumi na kuimarisha afya, huku akimuagiza Msajili wa Vyama vya Michezo kuhakikisha anatimiza wajibu wake kwa weledi na viwango katika kusimia vyama hivyo.
    “BMT lazima mkae mguu sawa katika kutekeleza majuku yenu, ni jukumu lenu kuonyesha mafanikio kutokana na mafungu mbalimbali mnayopokea ya kuendesha michezo kwa uwazi na ukweli”, alisema Mhe.Ulega.
     Mhe.  Naibu Waziri Ulega ameongeza kuwa suala ya Tuzo kwa wanamichezo ni jambo jema ambalo linatakiwa kutekelezwa haraka ili kutambua mchango wa wanamichezo nchini.
    Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo Bw.Yusuph singo amesema kuwa sekta hiyo imepata mafaniko mengi ikiwemo timu za wanawake za mpira wa miguu kutwaa makombe mbalimbali Afrika, Timu ya vijana chini ya miaka 17 kushiriki AFCON 2019 yaliyofanyika hapa nchini na timu ya vijana chini ya miaka 20 kufuzu AFCON 2021.
    Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza hilo Bi. Neema Msita amesema kuwa miongoni mwa mafanikio ya Baraza hilo ni kuboresha baadhi ya Kanuni ambazo zimeleta mafaniko ikiwemo kutambulika kwa michezo ya ridhaa na ya kulipwa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WAZIRI MPYA WA MICHEZO, BASHUNGWA ASEMA WANATAKA KUIIMARISHA BMT ILI IVISIMAMIE VYEMA VYAMA VYA SEKTA HIYO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top