• HABARI MPYA

    Thursday, May 23, 2019

    SEVILLA YATOKA NYUMA NA KUIPIGA SIMBA SC 5-4 UWANJA WA TAIFA, BOCCO MCHEZAJI BORA WA MECHI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya Sevilla ya Hispania imefanikiwa kutwaa Kombe la SportPesaChallenge baada ya kuwafunga wenyeji, Simba SC mabao 5-4 katika mchezo maalum wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam usiku wa leo.
    Lakini haukuwa ushindi mwepesi, kwani Sevilla waliomaliza nafasi ya sita kwenye La Liga msimu walilazimika kutoka nyuma kwa mabao 3-1 hadi mapumziko ili kushinda 5-4.
    Nahodha wa klabu, John Raphael Bocco alianza kuifungia Simba SC dakika ya nane kabla ya mshambuliaji mwenzake, Mnyarwanda Meddie Kagere kufunga la pili dakika ya 14.
    Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe akiwakabidhi Kombe Sevilla
    Wachezaji wa Sevilla wakifurahia na kombe lao baada ya mechi
    Nahodha wa Simba SC, John Bocco akikabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi

    Sevilla ikazinduka na kupata bao lake la kwanza dakika ya 24 kupitia kwa Jesus Escudero, lakini mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya 32.
    Sevilla ikakianza vyema kipindi cha pili baada ya kufanikiwa kupata bao la pili kupitia kwa Bryan Gil dakika ya 48, lakini kiungo Mzambia, Clatous Chama akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 61.
    Sevilla wakacharuka kuanzia dakika ya 85 wakipata mabao matatu na kuibuka na ushindi huo, kabla ya kukabidhiwa Kombe na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe.
    Alianza winga Mholanzi, Quincy Promes kufunga mabao mawili dakika ya 85 na 89 kabla ya Manuel Agudo Durán maarufu kama Nolito kufunga la ushindi dakika ya tano ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90.
    Pamoja na kuchapwa, Simba SC ikajifariji baada ya Nahodha wake, John Bocco kukabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi hiyo.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manila/Deogratius Munishi ‘Dida’ dk46, Zana Coulibaly/Nicolas Gyan dk46, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’/Rashid Juma dk79, Pascal Wawa/Yussuf Mlipili dk46, Jonas Mkude/Muzamil Yassin dk65, Emmanuel Okwi/James Kotei dk46, Clatous Chama/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk79, John Bocco/Adam Salamba dk79 na Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga dk65. 
    Sevilla: Juan Soriano, Jesus Navas, Sergio Escudero, Simon Kuaer/Franco Vasquez, Ever Banega, Sergi Gomez,Quincy Promes/Bryan Gil dk65, Roque Sema, Wissam Ben Yedder, Manuel Agudo Nolito na Franco Vazquez.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SEVILLA YATOKA NYUMA NA KUIPIGA SIMBA SC 5-4 UWANJA WA TAIFA, BOCCO MCHEZAJI BORA WA MECHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top