• HABARI MPYA

    Thursday, July 19, 2018

    SIMBA SC YAMTAMBULISHA RASMI MBELGIJI KUWA KOCHA MPYA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KLABU ya Simba SC imemtambulisha rasmi beki wa zamani wa kimataifa wa Ubelgiji, Patrick Winand J. Aussems kuwa kocha wake mpya akichukua nafasi ya Mfaransa, Pierre Lechantre aluyeondoka Mei.
    Aussems aliyezaliwa Februari 6, mwaka 1965 mjini Moelingen, Ubelgiji ametambulishwa mchana wa leo hoteli ya Serena mjini Dar es Salaam na rais wa klabu hiyo, Salim Abdallag 'Try Again' akitokea timu ya taifa ya Nepal.
    Salim amesema kwamba wana imani kubwa na Aussems kwamba atailetea mafanikio klabu yao kutokana na rekodi yake nzuri.
    Kocha huyo ana uzoefu wa kufundisha timu kadhaa Asia na Ulaya – lakini amewahi kufundisha KSA ya Cameroon na AC Leopards ya Dolisie nchini Kongo, hizo zikiwa timu pekee za Afrika.
    Aussems alikuwa jukwaani Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam jana wakati wa mchezo wa mwisho wa Kundi C Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kati ya Simba na Singida United timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1.

    Patrick Aussems (kushoto) akisaini mikataba na Kaimu Rais wa, Salim Abdallah 'Try Again  

    WASIFU WA PATRICK WINAND J. AUSSEMS:  

    Jina Kamili; Patrick Winand J. Aussems
    Kuzaliwa; Februari 6, 1965
    Alipozaliwa; Moelingen, Ubelgiji
    Timu alizochezea
    Mwaka             Timu 
    1974–1981 RCS Visé
    1981–1988 Standard Liege
    1988–1989 K.A.A. Gent
    1989–1990 R.F.C. Seraing
    1990–1993 ES Troyes AC
    Timu alizofundisha
    1992 ES Troyes AC
    1995–1999 SS Saint-Louisienne
    1999–2001 Capricorne Saint-Pierre
    2002–2003 Stade Beaucairois
    2003–2004 Stade de Reims
    2004–2005 KSA Cameroon
    2005–2006 SCO Angers
    2009–2010 Evian Thonon Gaillard F.C.
    2011–2012 Shenzhen Ruby
    2012–2013 Chengdu Blades
    2013–15 AC Léopards
    2015–16 Nepal


    Baada ya hapo akaondoka uwanjani akiongozana na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba SC, Jasmin Costa na inaelezwa leo ndiyo ilikuwa siku ya mazungumzo ambayo kama yatakwenda vizuri yatafuatia na kusaini mkataba.   
    Aussems alianza kama mchezaji wa kwao, akichezea klabu za RCS Vise (1974–1981), Standard Liege (1981–1988), K.A.A. Gent (1988–1989), R.F.C. Seraing (1989–1990) na ES Troyes AC ya Ufaransa kuanzia mwaka 1990 hadi 1993, ambayo ilikuwa timu yake ya kwanza kufundisha akianza kama kocha mchezaji mwaka 1992.
    Mwaka 1995 alienda kufundisha SS Saint-Louisienne hadi 1999 alipohamia Capricorne Saint-Pierre hadi 2002 alipokwenda Stade Beaucairois hadi 2003 alipojiunga na Stade de Reims zote za Ufaransa hadi mwaka 2004 alipokuja Afrika kufundisha KSA ya Cameroon hadi mwaka 2006 aliporejea Ufaransa kufundisha SCO Angers.
    Timu nyingine alizofundisha ni Evian Thonon Gaillard F.C. ya Ufaransa pia kuanzia 2009 hadi 2011 alikwenda China kufundisha Shenzhen Ruby (2011) na Chengdu Blades kuanzia 2012 hadi 2013 aliporudi Afrika kufundisha AC Leopards hadi mwaka 2015 alipokwenda kufundisha timu ya taifa ya Nepal.
    Kwa upande wake, Lechantre aliyekuja na msaidizi wake binafasi Simba, Mtunisia Aymen Hbibi Mohammed aliondokea nchini Kenya mwezi uliopita timu ilipokuwa kwenye michuano ya SportPesa Super Cup, baada ya kutofautiana na uongozi.
    Lechantre aliyeanza kazi Januari 18 tu, mwaka huu ghafla alisusa kazi nchini Kenya baada ya mechi moja dhidi ya Kariobangi Sharks na akapanda jukwaani wakati Simba SC ikimenyana na Kakamega Homeboyz katika Nusu Fainali ya SportPesa Super Cup na kuibuka na ushindi wa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Afraha pia.

    Msemaji wa klabu ya Simba, Hajji Manara (kushoto) akimkabidhi jezi ya klabu hiyo, kocha Patrick J. Aussems leo

    Timu iliongozwa na Kocha Msaidizi, Mrundi Masoud Juma aliyekaa benchi na kocha wa makipa, Muharami Mohammed ‘Shilton’ na jukwaani alikuwepo Kaimu Rais wa klabu, Salim Abdallah ‘Try Again’.
    Dalili za Simba SC kutodumu na kocha huyo zilianza kuonekana mapema tu baada ya Lechantre kuomba kazi ya kuifundisha timu ya taifa ya Cameroon Aprili mwaka huu.
    Na baada ya Ligi Kuu kumalizika, Simba SC ikitwaa ubingwa wa kwanza tangu mwaka 2012, iliibuka minong’ono Simba SC haiwezi kuendelea na Mfaransa huyo kwa sababu ya mshahara mkubwa.
    Lakini pia minong’ono mingine ilikuwa inasema kwamba  viongozi wa Simba hawapendezewi na tabia ya ukali wa kupitiliza wa kocha huyo kiasi cha kutopenda hata kuzungumza wala kupokea ushauri.
    Lechantre alichukua nafasi ya Mcameroon Joseph Marius Omog na ameiongoza timu katika mechi 22 tu, ukiondoa mchezo huo ambao alikuwa jukwaani, ikishinda 14, sare saba na kufungwa moja.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAMTAMBULISHA RASMI MBELGIJI KUWA KOCHA MPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top