• HABARI MPYA

  Friday, July 20, 2018

  YONDAN KUREJEA MAZOEZINI YANGA SC JUMATAU BAADA YA KUFIKIA MAKUBALIANO YA MKATABA MPYA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa Yanga, Kelvin Patrick Yondan anatarajiwa kuanza mazoezi Jumatatu baada ya mgomo wa takriabn mwezi mmoja akishinikiza kupatiwa mkataba mpya. 
  Yondan amemaliza mkataba wake Yanga SC Juni mwaka huu, lakini kwa kipindi chote ameshindwa kufikia makubaliano ya mkataba mpya na klabu.
  Juzi mchezaji huyo wa zamani wa Simba SC na Toto Africans ya Mwanza, alikuwa ana mazungumzo na wadau maalum wa klabu hiyo waliojitolea kuhakikisha suala lake linamalizwa na anasaini mkataba mpya.
  Kelvin Yondan (katikati) akiwa na Mwenyekiti 
  wa zamani wa klabu hiyo, Tarimba Abbas (kushoto)   


  Mazungumzo hayo yaliyoongozwa na Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, Tarimba Abbas yamefikia pazuri na Yondan amekubali kurudi mazoezini huku taratibu nyingine za mkataba mpya zikikamilishwa. 
  Wadau hao baada ya kumaliza suala la Yondan, sasa wanamgeukia beki mwingine, Hassan Ramadhani Kessy ambaye naye yupo kwenye mgomo wa kudai mkataba mpya pia ili naye wambakize Jangwani.
  Yondani na Kessy hawakuwepo kwenye kikosi cha Yanga SC kilichopigwa mabao 4-0 na wenyeji, Gor Mahia katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika usiku wa Jumatano Uwanja wa Moi Kasarani mjini Nairobi.
  Huo ulikuwa mwendelezo wa Yanga kuvurunda katika michuano hiyo, ikikamalisha mechi tatu za mzunguko wa kwanza bila ushindi, ikifungwa mbili zote 4-0, ya kwanza dhidi ya MC Alger nchini Algeria Mei 6 na sare ya 0-0 na Rayon Sport mjini Dar es Salaam Mei 16. 
  Yanga wataikaribisha Gor Mahia Julai 29 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano kabla ya kurudiana na USM Alger Agosti 19 na kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YONDAN KUREJEA MAZOEZINI YANGA SC JUMATAU BAADA YA KUFIKIA MAKUBALIANO YA MKATABA MPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top