• HABARI MPYA

    Thursday, April 16, 2015

    MALINZI ‘AWAPANDISHA MZUKA’ YANGA SC WACHINJE WAARABU TAIFA JUMAMOSI

    Na Baraka Kizuguto, DAR ES SALAAM
    RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amewataka Yanga SC kupambana kuhakikisha wanaota ushindi mzuri dhidi ya Etoile du Sahel ya Tunisia Jumamosi  Uwanja wa Taifa jijini Dar  es Salaam.
    Katika salamu zake kwa klabu ya Yanga SC, Malinzi amewaambia wawakilishi pekee wa Tanzania katika michuano ya Afrika wahakikishe wanapata ushindi katika mchezo huo wa kwanza Raundi ya Pili Kombe la Shirikisho Afrika.
    Yanga imefika katika hatua ya 16 bora Kombe la Shirikisho baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).

    Ikifanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel, Yanga SC itacheza na moja ya timu nane zitakazotolewa 16 bora ya Ligi ya Mabingwa kuwania kupangwa kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho.
    Wapinzani wao, Etoile du Sahel wanatarajiwa kuwasili Saa 9:30 usiku kwa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair   bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56.
    Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tunisia  (FTF), Krifa Jalel ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa klabu ya Etoile du Sahel (ESS), Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10.
    Timu ya Etoile du Sahel itafikia katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi, na kesho jioni ijumaa wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
    Waamuzi wa mchezo huo ni Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na wanatarajiwa kuwasili leo mchana, huku kamisaa wa mchezo huo Salah Ahmed Mohamed kutokea nchini Sudan akitarajiwa kuwasili leo jioni na wote watafikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MALINZI ‘AWAPANDISHA MZUKA’ YANGA SC WACHINJE WAARABU TAIFA JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top