• HABARI MPYA

    Saturday, April 26, 2014

    MUUNGANO MCHUNGU KWA STARS, YAPIGWA ‘SERIKALI TATU’ NA BURUNDI TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imewafanya wananchi wamalizie vibaya sherehe za miaka 50 za Muungano baada ya kufungwa mabao 3-0 na Burundi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa jioni hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Stars iliyotumia wachezaji wengi chipukizi waliopatikana kwa njia ya maboresho ya timu hiyo, leo ilionekana kuzidiwa katika idara na Burundi iliyotumia wachezaji wake wazoefu.
    Winga wa Taifa Stars, Simon Msuva akimtoka beki wa Burundi leo Taifa

    Mshambuliaji wa Yanga SC na Nahodha wa Int’hamba Murugamba, Didier Kavumbangu alifungua pati la mabao ya Burundi dakika ya 45 akifunga kwa ustafi akimalizia pasi nzuri ya Ndarusanze Claude aliyeingia dakika ya 32 kuchukua nafasi ya Paschal Hakizimana.
    Burundi walikwenda kupumzika wakiwa wanaongoza kwa bao hilo 1-0 na kipindi cha pili Stars ilidhoofika zaidi na kuongezwa mabao mawili ndani ya dakika nne.
    Alianza mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Bara, Amisi Tambwe anayechezea Simba SC dakika ya 56 aliyefumua shuti akiwa ndani ya eneo la hatari baada ya kutengewa mpira kwa kifua na Kavumbangu kufuatia koris ya Cedric Amisi.
    Amisi Cedric kushoto akimpongeza Amisi Tambwe baada ya kufunga bao la pili,kulia ni Kavumbangu na Msuva wa Stars aliyejishika kiuno
    Mashabiki watoto wa Stars wakiitani Stars imepigwa serikaloi tatu na Burundi siku ya miaka 50 ya Muungano
    Msuva akiwatoka wachezaji wa Burundi

    Yussuf Ndikumana alifunga bao la tatu dakika ya 60 kwa shuti la umbali wa mita 50 baada ya kukutana na mpira akiwa katikati ya Uwanja na kumtazama kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyekuwa ametoka langoni mwake na kumtungua kiulaini.
    Bao hilo liliamsha Stars na kutoka wote kushambulia kusaka japo bao la kufutia machozi na Simon Msuva alitengeneza nafasi tatu nzuri na zote wenzake wakashindwa kuzitumia vizuri.
    Nafasi nzuri zaidi ilikuja dakika ya 85 baada ya Msuva kuteleza kulia mwa Uwanja na kuingia hadi kwenye boksi akamkatia pande safi Ramadhani Singano ‘Messi’ ambaye alipiga nje.
    Mchezo wa leo umeonyesha Tanzania bado ina safari ndefu na ngumu kuweza kupata timu bora ya taifa.
    Kikosi cha Tanzania leo kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Omar Kindamba/Himid Mao, Edward Peter, Aggrey Morris, Said Mourad, Said Juma/Jonas Mkude, Simon Msuva, Frank Domayo, Ayoub Lipati/Omar Nyenje, Mohamed Seif/Haroun Chanongo na Ramadhani Singano ‘Messi’.
    Burundi; Arthur Arakaza/Biha Omar, Kiza Fataki, Rugonumugabo Stephane, Issa Hakizimana, Rashid Leon, Yusuf Ndikumana/Nahimana Chasil, Steve Nzigamasabo, Amisi Cedric, Didier Kavumbangu, Paschal Hakizimana/Ndarusanze Claude na Amisi Tambwe/Shaaban Hussein. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MUUNGANO MCHUNGU KWA STARS, YAPIGWA ‘SERIKALI TATU’ NA BURUNDI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top