• HABARI MPYA

    Saturday, April 19, 2014

    LIGI KUU BARA YAFIKIA TAMATI LEO, AZAM BINGWA, ASHANTI, RHINO NA OLJORO ZAAGA

    Na Saada Akida na Zaituni Kibwana, Dar es Salaam
    PAZIA la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara limefungwa rasmi leo kwa Azam FC kutimiza ndoto za kumaliza ligi hiyo bila kupoteza mechi baada ya ushindi wa 1-0 jioni hii Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Mganda, Brian Umony ndiye aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 78 na kwa matokeo hayo, Azam FC inamaliza na pointi 62 na wametawazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Bara, wakiipokonya taji Yanga SC iliyomaliza katika nafasi ya pili na pointi 56 baada ya sare ya 1-1 jioni hii na watani wao, Simba SC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Nahodha wa Azam FC akiwa ameinua cheti cha kutambuliwa na FIFA kama mabingwa wapya wa Bara baada ya kukabidhiwa na Jamal Malinzi leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

    Azam ilijihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Jumapili iliyopita, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kufikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo zisingeweza kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho leo.
    Licha ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Aprili 13, mwaka huu, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo
    Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.
    Mechi ya leo ilihudhuria na Wakurugenzi wa Azam, Abubakar, Omar na Yussuf, watoto wa Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa ambao waliketi jukwaa kuu pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi.
    Malinzi alimkabidhi Kombe la ubingwa Nahodha wa Azam, John Bocco baada ya mechi hiyo pamoja na cheti maalum kutoka FIFA, ambacho kinatolewa kwa mara ya kwanza mwaka huu na Azam inakuwa timu ya kwanza kupata.
    Wachezaji wote walivalishwa Medali baada ya mechi na baada ya hapo sherehe za ubingwa zilichukua nafasi yake Uwanja wa Azam Complex.
    Taifa; Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mechi ya watani wa jadi ilimalizika kwa sare ya kufungana bao 1-1, Simba wakitangulia kupata bao dakika ya 77 kupitia kwa Haroun Chanongo, kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Yanga SC dakika ya 86.
    Uwanja wa Jamhuri, Morogoro Ashanti United iliendeleza rekodi yake ya kushuka msimu ule ule waliopanda Ligi Kuu, baada ya kufungwa 1-0 na Prisons ya Mbeya- bao pekee la Peter Michael dakika ya 54, wakati JKT Oljoro na Mtibwa Sugar zimetoka sare ya 1-1 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, na Mbeya City wameilaza 1-0 Mgambo JKT, bao la Saad Kipanga dakika ya 75.
    Coastal Union pia imemaliza ligi na kipigo cha 1-0 kutoka kwa Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, bao pekee la Themi Felix dakika ya 50, wakati Ruvu Shooting imeshinda mabao 2-0 dhidi ya Rhino Rangers.
    Ashanti United ya Ilala, Dar es Salaam inayomaliza ligi na pointi 25, inaungana na JKT Oljoro ya Arusha iliyomaliza na pointi 19 na Rhino Rangers ya Tabora pointi 16 kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na nafasi zao zinachukuliwa na Ndanda FC ya Mtwara, Polisi ya Morogoro na Stand United ya Shinyanga zilizopanda kwa ajili ya msimu ujao. 
    Mbali na Azam kumaliza kileleni na pointi 62, Yanga SC pointi 56 nafasi ya pili, Mbeya City ya Mbeya imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake 49, Simba SC ya nne pointi 38, Kagera Sugar ya tano pointi 38 pia, Ruvu Shooting ya sita pointi 38, Mtibwa Sugar ya saba pointi 31, JKT Ruvu ya nane pointi 31 Coastal Union ya tisa pointi 29, Prisons ya 10 pointi  28 na JKT Mgambo ya 11 pointi 26.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LIGI KUU BARA YAFIKIA TAMATI LEO, AZAM BINGWA, ASHANTI, RHINO NA OLJORO ZAAGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top