• HABARI MPYA

    Saturday, April 26, 2014

    KOCHA MPYA STARS ATUA DAR NA KUSEMA; “NIMEKUJA KUWAPA KILE MLICHOKIKOSA KWA MUDA MREFU”

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    KOCHA mpya wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Martinus Ignatius ‘Mart’ Nooij amewasili usiku huu mjini Dar es Salaam tayari kuanza kazi, akirithi mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen.
    Nooij alitua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) majira ya Saa 8:20 usiku kwa ndege ya shirika la Ethiopia na moja kwa moja kupelekwea kupumzika katika hoteli ya Protea, katikati ya Jiji.
    Karibu sana mzee; Mshauri wa Ufundi wa Rais wa TFF, Pelegrinius Rutayuga kulia akimlaki kocha mpya wa taifa Stars, Mart Nooij usiku huu JNIA

    Nooij alilakiwa na Mshauri wa Ufundi wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Pelegrinius Rutayuga pamoja na Ofisa Itifaki wa shirikisho hilo, Raphael Matola aliyeshughulikia taratibu zake za Idara ya Uhamiaji kuweza kuruhusiwa kuingia nchini. 
    Mara baada ya kuwasili JNIA, Nooij aliiambia BIN ZUBEIRY, chombo pekee cha habari kilichokuwapo wakati anawasili na cha kwanza kuandika juu ya uteuzi wake, amekuja Tanzania kuwapa wananchi wake kile ambacho wamekikosa kwa muda mrefu.
    “Naifahamu Tanzania, najua wananchi wake wanapenda soka, wanapenda raha ambayo wameikosa kwa muda mrefu, naamini kwa ushirikiano na wananchi wa hapa, wakiwemo viongozi, wachezaji na vyombo vya habari, nitawapa kile ambacho wamekikosa kwa muda mrefu,”alisema Mholanzi huyo.
    Rais wa TFF, Jamal Emil Malinzi atamtambulisha rasmi mchana wa leo (Aprili 26, 2014) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya mchezo wa kirariki wa kimataifa baina ya Tanzania na Burundi.
    Raphael Matola akimpokea Nooij

    Tayari Nooij ambaye ametokea klabu ya St George ya Ethiopia amekwishasaini Mkataba wa miaka miwili na TFF baada ya mchakato makini, uliohusisha wataalamu na washauri wa kimataifa juu ya masuala ya ufundi uliomuidhinisha mwalimu huyo wa Kidachi aliyezaliwa Julai 3, mwaka 1954 mjini Beverwijk, Uholanzi.
    Nooij amewahi kuwa mwalimu maalum katika programu za maendeleo ya soka katika Chama cha Soka Uholanzi (DFA) na pia amewahi kufundisha timu ya EVC 1913 ya Marekani na baadaye Kazakhstan.
    Alikuwa kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 ya Burkina Faso katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2003 na mwaka 2004 alikuwa kocha wa muda wa klabu ya FC Volendam ya Uholanzi.
    Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa kocha wa Msumbiji na akaiwezesha kufuzu kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza Mambas wanashiriki AFCON baada ya msoto wa miaka 12. 
    Hata hivyo, katika fainali hizo, Msumbiji ilishika mkia katika kundi lake baada ya kuambulia sare moja na kufungwa mechi mbili. Baada ya kukosa tiketi ya  AFCON 2012, Nooij akajiuzulu Septemba mwaka 2011 na nafasi yake kuchukuliwa na Mjerumani, Gert Engels.
    Katikati ni Abel Mtweve, mdau aliyejitokeza kumpokea mwalimu huyo pia

    Aprili 19 mwaka 2012, aliajiriwa na klabu ya Santos ya Afrika Kusini, ambako hata hivyo alifukuzwa Desemba 18, mwaka 2012 na kunyakuliwa na St George ya Ethiopia.
    Nooij ataishuhudia Taifa Stars ikimenyana na  Int’hamba Murugamba baadaye chini ya Msaidizi wake, Salum Mayanga na baada ya hapo ataanza kasi rasmi.
    Mechi hiyo ya kirafiki ambayo ni sehemu ya maadhimisho ya sherehe za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar itachezeshwa na refa Anthony Ogwayo kutoka Kenya na itaanza saa 10:00 jioni. Ogwayo atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Oliver Odhiambo wote pia kutoka Kenya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel Mujuni wa Tanzania wakati Kamishna ni Charles Ndagala.
    Viingilio katika mechi hiyo ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA MPYA STARS ATUA DAR NA KUSEMA; “NIMEKUJA KUWAPA KILE MLICHOKIKOSA KWA MUDA MREFU” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top