• HABARI MPYA

    Monday, April 28, 2014

    SIMBA SC: ANAYEMTAKA TAMBWE AJE MEZANI

    Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
    SIKU moja baada ya mshambuliaji Amisi Tambwe kutangaza nia ya kujiunga na Azam FC na Yanga, uongozi wa Simba umesema hautamzuia nyota huyo kuiacha klabu hiyo ya Msimbazi.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu leo mchana akiwa mjini Kigali, Rwanda, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Pope, amesema wako tayari kumwachia nyota huyo kujiunga na timu yoyote atakayotaka.
    "Sera ya Simba iko wazi, hatuzuii mchezaji yeyote kujiunga na timu anayoitaka, kama Tambwe akipata timu itakayompa maslahi mazuri zaidi, sisi hatuna pingamizi, tutamwachia lakini wafuate tu taratibu zote za kuvunja mkataba maana bado ana mkataba na Simba," amesema Hans Pope.
    Mkali wa mabao; Simba SC imesema anayemtaka Tambwe aende kuzungumza nao
    Mwishoni mwa wiki Tambwe, mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2013/14, alisema jijini Dar es Salaam kuwa yuko tayari kuondoka Simba na kujiunga na timu yoyote itakayompa 'mpunga' mwingi.
    "Bado nina mkataba wa mwaka mmoja na Simba lakini timu nyingine ikija na dau kubwa niko tayari kujiunga nayo," alisema Tambwe katika mahoajiano na BIN ZUBEIRY jijini mwishoni mwa wiki.
    "Kwa sasa ni mapenzi na klabu ya Simba, lakini nikisajiliwa na Azam au Yanga, nazo nitazipenda tu," alisema zaidi raia huyo wa Burundi.
    Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Burundi na michuano ya Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati -- Tambwe, alijiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili Agosti mwaka jana akitokea klabu ya Vital'O ya kwao Burundi.
    Mkali huyo wa kufumania nyavu ameichezea Simba mechi 23 za Ligi Kuu msimu wa 2013/14 na kuifungia magoli 19 akikosa mechi tatu walizotoka sare ya 2-2 na Rhino Rangers mjini Tabora Agosti 24 mwaka jana baada ya yeye na Mrundi mwenzake Gilbert Kaze kukosa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
    Tambwe pia alikosa mechi ya mzunguko wa kwanza waliyolala 2-1 dhidi ya wasiofungiika Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Oktoba 28 mwaka jana baada ya kuumia katika mechi ya iliyotangulia waliyotoka suluhu na mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union Oktoba 23.
    Tambwe pia hakuwamo kwenye msafara wa kikosi cha Mcroatia Zdravko Logarusic kilichosafiri kwenda mjini Bukoba, Kagera kumenyana na Kagera Sugar katika mechi ya sare ya bao moja Aprili 5.
    Wakati Tambwe akikaribisha ofa, tayari kocha wa Azam FC, Mcameroon Joseph Omog ameshaweka wazi kwamba atasajili viungo na washambualiaji kutoka timu za Yanga, Simba na Mbeya City.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC: ANAYEMTAKA TAMBWE AJE MEZANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top