• HABARI MPYA

    Thursday, April 24, 2014

    BIN SLUM: NIMETUMIA ZAIDI YA MILIONI 300 COASTAL UNION, MALIPO YAKE KASHFA NA MASIMANGO

    Na Dina Ismail, Dar es Salaam
    MKURUGENZI Mkuu wa kampuni ya Bin Slum Tyres, Nassor Bin Slum amesema kwamba ametumia zaidi ya Sh. Milioni 300 kwa ajili ya Coastal Union ya Tanga ndani ya kipindi cha miaka minne, lakini ajabu malipo yake kukashifiwa.
    Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Bin Slum amesema; “Nimepokea kwa masikitiko makubwa habari zilizotolewa na uongozi wa Coastal Union kupitia Mwenyekiti wake, Ahmed Aurora katika gazeti la Mwananchi la tarehe 23/04/2014 kwamba kwa kipindi cha miaka minne ambacho jina la kampuni yangu limekuwa likihusishwa na jezi za Coastal Union, sijatoa kiasi chochote cha pesa kulipia tangazo hilo.
    Shukrani ya punda, mateke; Nassor Bin Slum amesema wema alioifanyia Coastal Union malipo yake ni kashfa na masimango

    Ukweli ni kwamba, ingawa hakukuwa na mkataba wowote wa maandishi baina ya Binslum Tyres Limited, lakini mchango wangu kipesa katika klabu ya Coastal umekuwa mkubwa na wa gharama kubwa kuliko kama ningeingia mkataba na Coastal Union.
    Niliigharamia Coastal Union kama Mwanachama, mnazi na shabiki wa klabu hii bila ya kujali misingi ya kiudhamini kwa kipindi cha miaka minne. Nimetumia zaidi ya shilingi 300 milioni kwa shughuli mbalimbali za klabu hii na mashabiki wa timu hii na viongozi wanaoweza kusutwa na nafsi zao ni mashahidi wakubwa katika hili.
    Nimetumia zaidi ya shilingi 200 milioni kwa ajili ya kusajili wachezaji pekee. Wachezaji hawa ni wale wenye majina makubwa na madogo ambao wakati mwingine nililazimika mwenyewe kusafiri kwenda kuwanunua nchini jirani kama Jerry Santo na Crispian Odula ambao nililazimika kusafiri mpaka Kenya kwenda kuwanunua.
    Nimetumia zaidi ya shilingi 100 milioni kwa ajili ya kugharamia mishahara, posho na bonasi za wachezaji, mshahara wa kocha kama Hemed Morocco kwa mwaka mzima, na baadhi ya maofisa wa timu. nimeandaa kambi zote za timu tangu ilipopanda Ligi Kuu pamoja na kugharamia safari za timu katika mikoa mbalimbali.
    Sijawahi kuwa na nia ya kuvitaja vitu hivi hadharani, lakini inapofika mahali ambapo mtu mzito katika klabu kama Mwenyekiti anaongea na vyombo vya habari kupotosha ukweli huu, nalazimika kulinda heshima yangu binafsi, heshima ya familia, na heshima ya kampuni ambayo nimeihasisi kwa jasho kubwa kwa msaada wote wa Mwenyezi Mungu.
    Lengo langu halijawahi kuitangaza Kampuni yangu kupitia jezi za Coastal Union. Lengo langu lilikuwa kuipa hadhi jezi ya Coastal na kuongeza ushindani kwa makampuni kuwania kutangaza bidhaa zao kupitia jezi za Coastal.
    Kama ningeamua kuitangaza kampuni ya Binslum katika jezi ya Coastal kibiashara, ningeweza kutumia hata shilingi milioni 50 tu ndani ya kipindi cha miaka minne kwa sababu nina uhakika wasingekataa. Kwa sasa Coastal bado haipo katika hadhi ya kudhaminiwa kwa mabilioni ya pesa kama Simba na Yanga.
    Vinginevyo ningeweza kuzidhamini klabu za Simba, Yanga, Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons, JKT Ruvu na nyingine ambazo ziliendelea kuwepo Ligi Kuu ya Tanzania Bara hata wakati Coastal ikiwa madaraja ya chini.
    Niliamua kuingiza pesa nyingi Coastal Union kama shabiki, mnazi na mkereketwa na sitarajii pesa hizo kurudi katika faida ya kampuni kwa sababu Coastal Union sio njia kuu ya utangazaji wa bidhaa za Binslum kuliko Magazeti, Televisheni na redio na matangazo ya barabarani.
    Ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya Bwana Aurora, ingawa nitaendelea kuwa shabiki na mwanachama mkubwa wa Coastal Union ambayo nimeishabikia tangu utotoni.
    Nimeamua kuweka bayana ukweli huu na kwa sababu Mungu ameyaona yote niliyoyatenda Coastal Union, yeye ndiye atakayekuwa shahidi wangu katika hili,”imemalizia taarifa hiyo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BIN SLUM: NIMETUMIA ZAIDI YA MILIONI 300 COASTAL UNION, MALIPO YAKE KASHFA NA MASIMANGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top