• HABARI MPYA

    Thursday, April 24, 2014

    MKENYA OGWAYO KUCHEZESHA STARS, BURUNDI

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    REFA Anthony Ogwayo mwenye beji ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kutoka Kenya ndiye atakayechezesha mechi kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Burundi (Intamba Mu Rugamba) itakayochezwa keshokutwa (Aprili 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ogwayo katika mechi hiyo ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar, atasaidiwa na Gilbert Cheruiyot na Oliver Odhiambo wote pia kutoka Kenya. Mwamuzi wa mezani atakuwa Israel Mujuni wa Tanzania.
    Kikosi cha sasa Taifa Stars

    Burundi inatarajia kuwasili nchini leo (Aprili 24 mwaka huu) saa 12 jioni kwa ndege ya Kenya Airways na itafanya mazoezi kesho (Aprili 25 mwaka huu) saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Taifa.
    Nayo Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ipo kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi hiyo ambayo itakuwa ya kwanza tangu kuanza kwa mpango wa maboresho wa timu hiyo.
    Makocha wa timu zote mbili pamoja na manahodha wao kesho (Aprili 25 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) watakuwa na mkutano na Waandishi wa habari kuzungumzia mechi hiyo.
    Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa VIP A kiingilio kitakuwa sh. 20,000 wakati VIP B na C ni sh. 10,000. 
    Wakati huo huo: Kocha Mkuu mpya wa Taifa Stars, Martinus Ignatius Maria maarufu kama Mart Nooij anatarajiwa kuwasili nchini Jumamosi alfajiri (Aprili 26 mwaka huu) tayari kwa ajili ya kuanza kazi ya kuinoa timu hiyo.
    Nooij (59) atawasili saa 7.20 usiku kwa ndege ya Ethiopia Airlines ambapo anatarajia kukutana na waandishi wa habari Jumamosi mchana, saa chache kabla ya kuanza mechi ya kirafiki kati ya Taifa Stars na Burundi itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MKENYA OGWAYO KUCHEZESHA STARS, BURUNDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top