• HABARI MPYA

    Wednesday, November 06, 2013

    MAREFA WALIKUWA CHANZO CHA MAAFA YA TAIFA OKTOBA 31

    RAIS wa Sirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Sepp Blatter aliwahi kusema soka na vurugu ni chanda na pete- na ninakumbuka kiongozi huyo wa dunia wa mpira wa miguu alisema hayo baada ya kutokea maafa uwanjani nchini Ivory Coast.
    Blatter alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa muongo uliopita na tangu hapo mamia wameendelea kufa viwanjani kutokana na vurugu zinazoibuka na kila siku ulinzi umekuwa ukiimarishwa nchi nyingi tu duniani.

    Soka ni mchezo wa watu ambao wanaongozwa na hisia. Watu ambao wanapenda furaha kupitia timu zao, watu ambao hawapendi kuona timu zao zinaonewa na inapotokea hivyo hakika inakuwa balaa si hapa Tanzania tu, popote duniani.
    Oktoba 31, mwaka huu kauli ya Blatter kwamba soka na vurugu ni chanda na pete ilichukua nafasi yake Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya Polisi kupambana na mashabiki wa Simba SC iliyokuwa ikimenyanana na Kagera Sugar ya Bukoba.
    Baada ya Kagera kusawazisha bao dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimia kwa dakika 90 na kupata sare ya 1-1, Uwanja wa Taifa, uligeuka eneo la vita baina ya Polisi mashabiki wa Simba SC.
    Baada ya Salum Kanoni kukwamisha nyavuni mkwaju wake wa penalti, mashabiki wa Simba waliokuwa viti vya Rangi ya Bluu na Chungwa, walianza kung’oa viti na kuvitupia uwanjani.
    Wazi chanzo cha vurugu ni marefa wabovu, ambao walifanya makosa mengi na mbaya zaidi mengi yalikuwa yakiwaumiza Simba SC.
    Mchezaji aliyesababisha penalti ya Kagera alionekana wazi akiuingiza mpira kwa mkono katika eneo la hatari na akajiangusha- lakini refa akatoa penalti. Na katika mchezo huo huo refa huyo huyo aliwanyima penalti Simba SC baada ya beki wa Kagera kuushika mpira wazi wazi kwenye eneo la hatari.
    Matukio yote haya mawili yalitokea katika lango moja la Kaskazini, Simba kunyimwa penalti halali kipindi cha kwanza na Kagera kupewa penalti haramu kipindi cha pili, hivyo mashabiki waliokuwa upande huo uzalendo uliwashinda wakafanya waliyoyafanya. Wamefanya kosa, hakuna ubishi.
    Lakini chanzo cha kosa lenyewe ni marefa wabovu na maana yake sasa, marefa wa aina hii wataendelea kuleta maafa katika viwanja vyetu, kwa sababu Blatter mwenyewe alikwishasema soka na vurugu ni chanda na pete- huwezi kuzuia hisia za mashabiki.    
    Mimi nawapenda Waingereza, wameweka sheria nyingi sana ambazo zinamfanya shabiki asiwe na wasiwasi hata kama timu yake itaonewa uwanjani, akijua kesho haki itatendeka.
    Moja ya sheria hizo ni kurudiwa kutazamwa kwa tukio katika picha na kutolewa maamuzi mapya yaliyo sahihi iwapo refa hataona uwanjani wakati anaongoza mchezo.
    Lakini huku kwetu jambo likitendeka, ndio imetoka haturudi nyuma hata kama ushahidi wa picha utaonyesha kosa lilitendeka. Mawili, Bodi ya Ligi Kuu iukubali udhaifu wa marefa wake na ipitishe kanuni kama za Waingereza, kukubali kutumia teknolojia kurekebisha makosa yaliyotokea uwanjani. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAREFA WALIKUWA CHANZO CHA MAAFA YA TAIFA OKTOBA 31 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top