• HABARI MPYA

    Saturday, November 09, 2013

    ALIYEMSAJILI TENGA YANGA SASA HATEMBEI TENA, NI MSHINDO MKEYENGE MTANGAZAJI MAARUFU WA RTD ENZI HIZO

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    YAWEZA kuwa unajua Leodegar Chilla Tenga alichezea Yanga SC kabla ya kwenda kuwa mmoja wa waasisi wa Pan African pale Mtaa wa Swahili, Kariakoo, Dar es Salaam.
    Lakini unajua alifikaje fikaje Jangwani yalipo makao makuu ya Yanga SC? BIN ZUBEIRY leo atakupa hadithi tamu ya beki huyo kutua Yanga.
    Jana katika sherehe za tuzo za Wanasoka Bora za gazeti la Mwanaspoti ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, Mtangazaji maarufu wa zamani wa mpira kituo cha Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Tido Mhando alisimulia kisa hicho.
    Hii ndiyo hali ya Mzee Mshindo Mkeyenge kwa sasa, ana mguu moja

    Tido ambaye kwa sasa ni Mtendaji Mkuu wa kampuni ya MCL, wachapishaji wa gazeti la Mwanaspoti, alisimulia kisa hicho wakati alipopewa fursa ya kwenda kutoa tuzo ya heshima kwa mtangazaji nguli na mstaafu wa mpira nchini, Mshindo Mkeyenge.
    Tido mwenye sauti ambayo utaipenda a kusikitika kwa nini hatangazi tena, alianza kwa kumuelezea Mzee Mkeyenge kabla ya kumuita kumkabidhi tuzo yake ya heshima.
    Alisema alipoingia RTD miongoni mwa watu aliowakuta pale alikuwa ni Mzee Mkeyenge na alimpokea vizuri hadi akawa mtu wa karibu kwake kwenye kazi.
    “Mshindo ndiye alikuwa mtu wa kwanza kunipa safari ya nje ya nchi, ilikuwa kwenye Kombe la Challenge Uganda, alinichukua tukaenda wote.
    Tenga katika picha ya pamoja na Mkeyenge kushoto na mke wa mzee huyo kulia 

    Lakini mwaka 1972 au 1973 kama sikosei tukaenda naye kwenye Kombe la Taifa, michuano ilifanyika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza. Katika ile michuano, Mkoa wa Pwani ulikuja na wachezaji kadhaa wanafunzi.
    Mmojwapo alikuwa mwanafunzi wa sekondari ya Kibaha, beki Leodegar Tenga, ambaye alikuwa akicheza vizuri sana. Sasa wakati tunatangaza mpira, Mshindo akawa ananiuliza, unamuonaje huyu kijana, mimi ninamuambia mzuri,”.
    “Mimi sikufuatilia sana nikajua mambo ya kazi tu, lakini nikaja kushitukia Tenga amejiunga na Yanga na wakati huo Mshindo alikuwa Katibu Mwenezi wa Yanga,”.
    Kijana aliyembeba Mzee Mkeyenge kwenda kupokea tuzo yake

    “Baadaye nikaja kugundua, ni Mshindo ndiye aliyempeleka Tenga Yanga na Tenga alipofika Dar es Salaam, katika siku zake za mwanzo za maisha alifikia kwa Mshindo alikuwa anaishi pale,” alisema Tido Mhando na akaomba sasa Mshindo ajitokeze kuchukua tuzo yake.
    Wakati wote wa stori hiyo, watu waliokuwamo ndani ya ukumbi wa Mlimani City walikuwa wanafurahia sana- lakini ulipowadia wakati wa Mshindo mwenyewe kuja kupokea tuzo yake, hali ilibadilika ukumbini.
    Hawa wote amewatangaza wakicheza; Mzee Mkeyenge akizungumza mbele ya wachezaji wa zamani wa Taifa Stars, kutoka kulia Nicholaus Akwitende, John Lyino, Mbwana Abushiri, Omar Zimbwe na Said George jana Mlimani City 


    Tido Mhando kulia na Naibu Waziri wa TEKNOHAMA, Januari Makamba kushoto wakimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya Sh. Milioni 1 Mzee Mkeyenge baada ya kupewa tuzo

    Mshindo akiwa Mwenyekiti wa zamani wa Yanga SC, Imani Madega kulia

    Ishara za masikitiko na huruma zilitawala, kwani mtangazaji huyo aliyekuwa kipenzi cha wasikilizaji wa mpira nchini, aliwasili jukwaani akiwa amebebwa na kijana kwa kuwa kwa sasa hawezi kutembea tena.
    Hawezi kutembea kwa sababu amekatwa mguu wa kushoto kutokana na maradhi ya kupooza. Hakika iliwasononesha wengi.
    Lakini Mshindo amekatwa mguu tu, hajakatwa sauti yake iliyokuwa ikivutia wasikilizaji wa mpira na aliweza kutumia fursa hiyo kuzungumza na kukumbusha mambo kadha wa kadhaa enzi zake.
    Kwanza, alisema alipopatia kipaji cha utangazaji; “Wakati nasoma Dodoma, wenzangu walipokuwa wanakwenda kucheza mpira, mimi napanda juu ya miti nachukua jaliboshi la sigara nalikunja (kama kipaza sauti) naanza kutangaza mpira. Huko ndipo nilipopatia kipaji changu hicho, basi nikaendelea hadi kuwa mtangazaji mzuri,”alisema.
    Mzee Mshindo pia alikumbushia baadhi ya mambo wakati wake anatangaza na kwa ujumla aliwasisimua watu na baada ya kukabidhiwa tuzo zake, alibebwa tena kurejeshwa katika nafasi yake.
    Shughuli ilipoisha, Tenga ambaye wakati wote Tido anasimulia alikuwa anatabasamu tu, alikwenda kumsabahi na kuzungumza naye Mzee Mshindo Mkeyenge. Naam, bila shaka umejua kuhusu Tenga namna alivyojiunga na Yanga SC, zilikuwa jitihada za Mkeyenge. Tumuombee afya njema mzee huyu aliye katika wakati mgumu hivi sasa. Inshaallah, amin.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ALIYEMSAJILI TENGA YANGA SASA HATEMBEI TENA, NI MSHINDO MKEYENGE MTANGAZAJI MAARUFU WA RTD ENZI HIZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top