• HABARI MPYA

    Wednesday, June 05, 2013

    TBL YAMWAGA NYUZI MPYA SIMBA NA YANGA KWA AJILI YA KAGAME

    Meneja wa Kilimanjaro, George Kavishe akimkabidhi jezi  Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itangare 'Kinesi' kulia 
    Na Ibrahim Kyaruzi, IMEWEKWA JUNI 5, 2013 SAA 9:30 ALASIRI
    IKIWA ni sehemu ya udhamini wake, bia ya Kilimanjaro Premium Lager imewapa vifaa vya michezo Simba na Yanga kwa ajili ya michuano wa Kombe la Kagame iliyopangwa kufanyika kuanzia tarehe 18 Juni mwezi huu.
    Akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, George Kavishe alisema, ‘‘ Bila ubishi Simba na Yanga ndio klabu kubwa za mpira Tanzania na zote zimefika  katika fainali za mchuano wa Kombe la Kagame kwa mara ya  19 sasa, haya ni mafanikio makubwa kwa hizi timu, kama wadhamini wakuu wa timu hizi, Kilimanjaro Premium Lager  inaziunga mkono Simba na Yanga katika harakati zao kucheza tena fainali za michuano hii ya kusisimua na ya kihistoria.
    Kavishe akimkabidhi jezi Katibu wa Yanga SC, Lawrence Mwalusako
    Aliongeza kuwa  Kombe la Kagame ni mashindano makubwa Africa mashariki na kati, na ni jukwaa bora kwa wachezaji wetu kuonyesha vipaji vyao  dhidi ya wachezaji wa viwango vya juu katika kanda hii lakini pia ni jukwaa zuri kwa wale wanaounda timu za taifa kuchagua wachezaji.
    “Ushirikiano huu baina ya Bia ya Kilimanjaro na klabu hizi ni mizizi inayotokana na maadili katika kazi, kufanya kazi kama timu na ile kiu ya mafanikio.  Na mafanikio ya ushirikiano huu ni pamoja na kushuhudia  mara kwa mara timu hizi mbili zikitoa  wachezaji  kwa timu ya Taifa  (Taifa Stars) ambao  wamekuwa na matokeo mazuri chini ya udhamini wa Bia ya Kilimanjaro.
    Tutaendelea  kusaidia  timu hizi, na kuhakikisha tunapeleka mpira wa nchi hii kwenye kilele cha mafanikio.
    Meneja wa Bia ya Kilimanjaro pia aliwataka  Simba na Yanga kuhakikisha wanaiwakilisha nchi yetu vizuri  katika mchuano huu mkubwa wa vilabu katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati na kuwasihi kuchukua  ushindi na kurudi na kombe la 12 la Kagame kwa mashabiki wanaosubiria kwa hamu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TBL YAMWAGA NYUZI MPYA SIMBA NA YANGA KWA AJILI YA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top