• HABARI MPYA

    Friday, April 26, 2013

    SIMBA SC YAIPA MANENO YA UKWELI TFF, RAGE AMPOKEA KWA MIKONO MIWLI HANS POPPE

    Nakupokea kwa mikono miwili; Rage amempokea Hans Poppe

    Na Ezekiel Kamwaga
    UONGOZI wa Simba umekubaliana na hatua ya serikali kuzuia kuchezwa kwa mchezo uliopangwa kuchezwa leo wa Ligi Kuu ya Tanzania baina ya Wekundu wa Msimbazi na Ruvu Shooting Stars.
    Hata hivyo, uongozi wa Simba haujafurahishwa na namna uzuiaji huo ulivyofanyika, taarifa ikitolewa jana kwenye siku ya mechi yenyewe wakati maandalizi yote yakiwa yamefanyika na hivyo kusababisha matatizo katika sehemu kubwa tatu.
    Mosi, uongozi wa Simba umeingia gharama kubwa ya kuweka timu kambini na kujiandaa na mechi. Pili, benchi la ufundi na wachezaji walikuwa tayari wamejiandaa na mechi kimwili na kiakili na kuahirishwa huku kwa mechi kumesaidia tu kuvuruga programu. Tatu, wapenzi na washabiki wa Simba wamepata usumbufu wa kwenda uwanjani na kukuta hakuna mechi.
    Uongozi wa Simba umewaomba radhi wapenzi na wanachama wake ambao walifika Uwanja wa Taifa jana kutazama mechi ambayo haikuwapo.
    “Washabiki ndiyo wanaoifanya Simba na mchezo wa mpira wa miguu nchini uwe na umaarufu ulionao na bila wao ligi yetu inaweza kupoteza nguvu na ushindani ilionao,”imesema taarifa ya Simba SC.
    Simba SC inashauri kuwe na utaratibu unaojulikana wa kuahirisha mechi kwa walau saa 48 kabla ya siku ya mechi, ikiamini hiyo itasaidia pande zote zinazohusika. 
    “Kama mechi imeshindikana kwa sababu za nje ya uwezo wa kibinadamau (Force de Majeure) kama vile mafuriko, tetemeko la ardhi na vimbunga, mechi inaweza kuahirishwa ghafla lakini si kwa mechi ambayo uwepo wake ulifahamika miezi kadhaa nyuma,”imesema taarifa ya Simba SC.
    Simba pia imeshauri kuwe siku maalum za mechi za Ligi Kuu na kila siku mechi zinachezwa, wakitolea mfano wao walikuwa na mechi wikiendi iliyopita na Ruvu ilikuwa na mechi Mbeya zaidi ya wiki moja iliyopita na hivyo mechi hii ingeweza kuchezwa hata juzi (Jumatano) ambayo ni siku ya kawaida kwa mechi kuchezwa badala ya jana Alhamisi.
    “Ni matumaini yetu kwamba kuahirishwa kwa mechi hii kutakuwa fundisho kubwa katika upangaji wa ratiba na uahirishaji wa mechi ambao una faida kwa pande zote husika,”imesema taarifa hiyo.
    Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, amemshukuru aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu, Zacharia Hans Poppe, kwa kukubali kurejea kushikilia nyadhifa zake zote.
    Poppe alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake za uongozi ndani ya Simba Machi 7 mwaka huu, kutokana na hali ya migogoro iliyokuwapo wakati huo.
    Hata hivyo, Rage alikataa kujiuzulu huko kwa Poppe na akasema atamshawishi abadili maamuzi kwa manufaa ya Simba.
    “Napenda kutumia nafasi hii kuwaarifu wana Simba popote walipo kwamba Poppe amerejea na yuko tayari kuitumikia Simba kama Mjumbe wa Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba,” alisema Rage.
    Kwa upande wake, Poppe alisema amerejea Simba kutokana na utulivu ulioanza kujitokeza klabuni na kwamba nia yake ni kuhakikisha klabu inafanya usajili mzuri na wa kiwango kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC YAIPA MANENO YA UKWELI TFF, RAGE AMPOKEA KWA MIKONO MIWLI HANS POPPE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top