• HABARI MPYA

    Tuesday, April 30, 2013

    AZAM FC WAJIFUA NA KUIFANYIA UKACHERO RABAT, STEWART ASEMA WAARABU WATAANGUA KILIO CHA MACHOZI YA DAMU JUMAMOSI

    Kocha Stewart Hall, akiwaongoza wachezaji wake mazoezini jioni ya leo viwanja vya Maamora

    Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
    AZAM FC leo imefanya mazoezi yake ya kwanza tangu iwasili nchini Morocco jana kwa ajili ya mchezo wa marudiano, Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya wenyeji AS FAR ya Rabat Jumamosi mjini hapa.
    Kikosi cha Azam, kimefanya mazoezi ya saa mbili kuanzia saa 9:00 Alasiri kwa saa za hapa sawa na saa 11:00 jioni kwa saa za Dar es Salaam kwenye viwanja vya michezo vya Maamora.
    Wachezaji walionekana wachangamfu na kufurahia Uwanja wa nyasi halisi waliofanyia mazoezi, katika kituo hicho chenye viwanja zaidi ya vitano vizuri, vikiwemo vyenye nyasi bandia.
    Baada ya mazoezi, Kocha Muingereza, Stewart Hall alisema amefurahia mazingira ya Uwanja na ukarimu wa wenyeji kwa ujumla.
    “Sina malalamiko, mazingira mazuri kila kitu safi. Mambo yanakwenda vizuri, nafurahi,”alisema Stewart. 
    Salum Abubakar 'Sure Boy' akimtoka Kali Ongala mazoezini

    Seif Abdallah akimtoka Humphrey Mieno. Kulia ni Waziri Salum

    Kali Ongala akiwatoka Sure Boy na Brian Umony

    Kipre Tchetche akimtoka Malika Ndeule

    John Bocco 'Adebayor' akitafuta mbinu za kumtoka Omar Mtaki. Kulia Uhuru Suleiman

    Uwanja safi, mazoezi yananoga

    Kwenye baridi watu hawachoki
    Baada ya mazoezi, wachezaji walirejea kwenye hoteli waliyofikia, Golden Tulip, wakati Stewart na Msaidizi wake, Kali Ongala pamoja na viongozi, Katibu Nassor Idirsa, Meneja Patrick Kahemele, Msaidizi wake, Jemadari Said walikwenda Uwanja wa Prince Moulay Abdallah, ambako wapinzani wao, FAR Rabat walikuwa wanamenyana na Widad Fez katika mechi ya Ligi Kuu ya kwao.
    Rabat ilishinda 1-0, bao pekee la El Mahdi Naghmi dakika ya 90 kwa tik tak, baada ya kutokea piga nikupige langoni mwa Fez.
    Ushindi huo, umewafanya wazidi kuikaribia Raja Casablanca kileleni, kwa kufikisha pointi 53, baada ya kucheza mechi 25, ikizidiwa tatu na vinara hao wa ligi hiyo, waliocheza mechi moja zaidi dhidi yao katika ligi ya timu 16. 
    Akiwa uwanjani hapo, Stewart aliwatazama kwa makini wapinzani wake, ambao hawakucheza soka ya kuvutia sana kulinganisha na wapinzani wao, Fez huku akionekana kuandika kwenye kitabu chake mambo fulani kwa ajili ya kuyatumia kuwaelekeza wachezaji wake kuelekea mchezo huo.
    Stewart akimuonyesha kitu uwanjani Kali


    Stewart akiandika kwenye kitabu chake

    Mashabiki wa Rabat

    Hicham El Fathi wa Rabat akimzuia mchezaji wa Widad Fez

    Stewart kwa makini zadi, huku akikuna kichwa...na Kali kama unavyomuona

    Baada ya mechi hiyo, Stewart alisema; “Nimewaona, kwa kweli bado sioni kama ni timu ya kutisha kwetu. Sisi ni bora kuliko wao na nina matumaini ya kufanya vizuri dhidi yao,”.
    Wakati wa mchezo, japokuwa hawakuwapo watu wengi uwanjani, lakini FAR Rabat ilionekana kushangiliwa zaidi. Mashabiki wake wanajua kuhamasisha, wakiimba nyimbo nzuri na kushangilia muda wote.
    Lakini pia, wanaonekana ni watu wa vurugu timu yao inapofanya vibaya. BIN ZUBEIRY ilizungumza na baadhi ya mashabiki wa Rabat, wakasema baadhi ya mashabiki wao, zaidi ya 500 wanatafutwa na Polisi baada ya kufanya vurugu wiki iliyopita walipokwenda kucheza mechi Casabalanca na ndiyo sababu leo hawakuwa wengi uwanjani.
    “Wanaogopa wakionekana tu, watakamatwa na Polisi, ndiyo maana si wengi leo, ila huwa wanajaa pote pale,”alisema shabiki mmoja akionyesha eneo wanaloketi mashabiki hao, upande wa ubao wa kuonyesha matokeo.
    Azam itaendelea na mazoezi kesho na Stewart amesema watafanya awamu mbili, asubuhi na jioni.
    Viongozi; Kutoka kulia Jemadari, Nassor na Kahemele


    Mweusi anavutia; Bin Zubeiry akiwa katikati ya mashabiki wa Rabat na bendera yao

    Raha ya bao; Mashabiki wa Rabat wakishangilia bao la dakika ya mwisho

    Wanaondoka; Kutoka kulia Bin Zubeiry, Kahemele na Nassor

    Azam iliwasili hapa jana baada ya safari ndefu ya takriban saa 14 angani na saa mbili na ushei barabarani- saa tano kutoka Dar es Salaam hadi Dubai na saa tisa kutoka Dubai hadi Cassablanca- kisha saa mbili kwa barabara hadi Rabat.  
    Iliondoka Dar es Salaam Jumapili saa 11:00 jioni na kufika Dubai saa 6:00 ambako ililala hadi asubuhi ya jana ilipoondoka kuja Morocco na wachezaji walifika wamechoka kwa uchovu wa safari ndefu.
    Ikumbukwe, Azam inayoshiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya Afrika, inahitaji sare yoyote ya mabao au kushinda, ili kusonga mbele, baada ya awali katika mchezo wa Dar es Salaa kulazimishwa sare ya bila kufungana.
    Mechi hiyo itachezwa kwenye Uwanja huo huo wa Prince Moulay Abdallah hapa Rabat, wenye uwezo wa kukusanya mashabiki 52,000 kuanzia saa 11:00 kwa saa za hapa, sawa na saa 1:00 kwa saa za nyumbani, Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM FC WAJIFUA NA KUIFANYIA UKACHERO RABAT, STEWART ASEMA WAARABU WATAANGUA KILIO CHA MACHOZI YA DAMU JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top