• HABARI MPYA

    Sunday, April 21, 2013

    HAYA YA ZANZIBAR, IKO WAPI TOFAUTI YA DHAMBI YA KUUA NA USHOGA?



    NISEME ukweli, napenda sana visiwa vya Zanzibar. Napenda sana mchezo wa soka. Napenda sana muziki. Watu wengi hawafahamu lakini ninapokwenda nje ya Tanzania, huwa nauliza zilipo sehemu tatu tu; wapi ninapoweza kutazama mpira wa Ulaya, wapi kwenye internet café na wapi kwenye Karaoke.
    Kwa ambao nimewaacha kidogo kuhusu karaoke, ni burudani ambayo mtu huimba nyimbo unayopenda kwa kupigiwa ala na wewe kuimba. Si kwamba napenda kuimba pekee au kusikiliza muziki; la hasha, nimewahi pia kujiandikisha katika darasa la kucheza muziki wa Salsa nchini Uganda mwaka 2008.
    Kwa ufupi, sinema na muziki ndiyo maisha yangu. Lakini, kama napata vitu hivyo na halafu nikiwa katika visiwa vya Zanzibar inakuwa nzuri, nzuri sana. 
    Safu hii ya leo ni zawadi kwa Zanzibar na Wazanzibari (na Wazanzibara).

    MIAKA michache iliyopita, taasisi ya 02 ilifanya utafiti wake nchini Marekani na barani Ulaya ambapo swali lilikuwa moja tu - kama kutakuwa na bendi ya watu wanne unayoihitaji, yenye mwimbaji, mpiga gitaa, mpiga ngoma na mpiga piano, ungetamani iundwe na wanamuziki gani?
    Kwa kura nyingi, jibu lilikuwa moja; gitaa apige Jimi Hendrix, ngoma apige Phil Collins, piano apige Elton John na kipaza sauti ashike Freddie Mercury.
    Sikushangaa wengine lakini jina la Mercury lilinishangaza. Mbele ya Michael Jackson, Elvis Presley, John Lennon na Paul McCartney, ilikuaje Mercury akashinda? Jibu nikalitafuta na nikalipata.
    Huyu bwana alikuwa anajua kuimba nyimbo kali. Alikuwa anajua kucheza na jukwaa. Ndiyo maana shoo aliyoitoa mwaka 1985 katika Uwanja wa Wembley kwenye shughuli ya Live Aid inatajwa kuwa ndiyo shoo bora zaidi kuwahi kufanyika hapa duniani.
    Vibao vyake kama Rock You, We are the Champions na kile maarufu cha Bohemian Rhapsody, viliwapagawisha washabiki na ni shoo ambayo inakumbukwa hadi leo.
    Wapo wanaoamini kwamba dunia haijawahi kutoa mburudishaji mahiri jukwani kama Freddie Mercury…. Kwamba pengine huyu bwana ndiye mwanamuziki mwimbaji bora zaidi kuwahi kutokea duniani. Alifariki mwaka 1991
    Lakini Freddie alizaliwa Zanzibar. Akakulia Zanzibar na yeye na familia yake wakahama Zanzibar baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 kutokana na mapinduzi yaliyotokea.
    Enzi hizo akiitwa Farrokh Bulsara. Hili jina la Freddie Mercury ni la jukwaani tu. Maana yake nini hii? Maana yake ni kwamba Tanzania imewahi kutoa mwanamuziki bora zaidi kuwahi kutokea duniani hata kama siasa zimesababisha hata watu wasijue kama huyu bwana alizaliwa kwetu.
    Nenda Zanzibar leo na hakuna ukumbusho wowote wa maana wa Freddie Mercury. Hakuna sanamu. Hakuna picha. Hakuna kumbukumbu yoyote ya maana. Uingereza ambako alihamia ukubwani, wana kumbukumbu zake zote.
    Kitu kibaya zaidi ni kwamba mwaka 2006, wakati baadhi ya watu (hususani kutoka Ulaya na Marekani)  walipotaka kufanya maadhimisho ya miaka 60 ya kuzaliwa kwake, shughuli hiyo ikafutwa.
    Kisa? Makundi ya kidini yalipinga kwa sababu Freddie aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa Ukimwi alikuwa amejitangaza kuwa ni shoga. Kwamba kumtukuza Freddie ni sawa na kuutukuza ushoga na tabia mbaya !
    Na hapa ndipo kwenye msingi wa safu yangu hii ya leo; kwanini tunawahukumu watu kwa mambo yasiyoendana na kila tunachowajulia au wanachokifanya?
    Watu wanataka kumkumbuka na kumheshimu Freddie kama mwanamuziki wa kipekee, wanakataliwa kwa sababu ya ushoga wake ! Lakini huyu bwana hakufahamika kwa ushoga wake bali kwa muziki wake. Na wanachotaka kumkumbukia watu ni kipaji chake na si ushoga wake.
    Unakuta mtu ana uwezo mkubwa wa kucheza soka lakini watu wanamhukumu kwa kunywa kwake pombe. Au mtu ni mchoraji mzuri sana lakini anapenda sana wanawake na watu wanataka achukiwe kwa sababu hiyo.
    Sisi ambao tunahukumu, hatujawahi kumsakama Julius Nyerere kwa kuwa kiongozi mzuri lakini asiye na kipaji cha soka. Tunamkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuongoza lakini hatumlaumu kwa yale ambayo hakujaaliwa.
    Pointi yangu kubwa leo hapa ni kwamba tukiamua kumpa mtu heshima yake, ni lazima tutofautishe kipaji chake na mapungufu yake. Tusimhukumu mtu kwa mambo yake ya pembeni.
    Sijawahi kusikia watu wakiwasema viongozi wa dini kwa kutokuwa na vipaji vingine kama vile kuimba au kuchora. Tunawaheshimu na kuwathamini kwa kazi zao za kueneza dini. Tunawaheshimu madereva kwa kazi yao.
    Tatizo linakuja tunapoanza kuwajadili wanamichezo na wasanii…. Tunataka wawe na vipaji na halafu tunataka pia wawe watakatifu!!!! Hii si haki. Kama tunataka kuwapa heshima au kuwahukumu, basi tuwatazame katika kazi zao.
    Tumwache Mwenyezi Mungu atoe hukumu yake ya haki siku itakapofika lakini wengine tuache kuhukumu.
    Kama serikali ingetumia fedha kidogo kukarabati nyumba aliyokuwa akiishi na kuifanya makumbusho na kufanya tamasha la kila mwaka kumkumbuka Freddie, Tanzania ingeongeza fedha nyingi za kigeni na tungepata wageni ambao wangeweza kupromoti wanamuziki na muziki wetu.
    Lakini hatuingizi chochote, tunapoteza historia kwa sababu ya mambo ambayo hayana faida. Nchi yetu hiihii inakumbuka kila mwaka watu ambao wanajulikana waliua mamia ya watu bila hatia lakini inakataa kumuenzi mtu eti kwa vile alikuwa shoga.
    Kuna tofauti gani kati ya dhambi ya kuua na ushoga? 
    Na kwanini tuwahukumu wanamuziki na wanamichezo kama mapadri na mashekhe wakati hatuwapi viongozi wa dini presha ya kuwa wachezaji au wasanii?
    LEO nimekumbuka sana Zanzibar kwa sababu ya msiba wa bibi yetu mpendwa Fatma Binti Baraka almaarufu Bi Kidude. Yeye, Sinti Binti Saad na Freddie pengine ndiyo wanamuziki mahiri zaidi kuwahi kutokea visiwani humo. 
    Zanzibar imetoa wasomi na wanazuoni wa kutosha. Mwanasiasa wa kwanza nchini aliyekuwa na mrengo wa kushoto wa ukweli kabisa alikuwa ni Dk. Abdulrahmn Babu, kutoka Zanzibar.
    Sijaoni mcheza mpira wa kikapu hapa nchini mwenye kipaji cha Abdallah Ramadhani “Dullah,”  naye Mzanzibari.
    Naamini Zanzibar ina vipaji vingi kuliko sote tunavyodhani. Hata hivyo, sidhani kama kuna mtu anataka kuwa kama hao kwa sababu hakuna lolote la maana la kuwaenzi magwiji hao watatu lililofanyika. 
    Hili ni jambo ambalo tunahitaji kulitazama vizuri….. Baadaye utakuja kusikia kwamba Bi. Kidude ni mtu mbaya kwa sababu alikuwa anavuta sigara. Tabia mbaya !
    Sipendi kusema hili neno lakini lina ukweli ndani yake; Si kila mtu anataka kwenda mbinguni…. Wengine mbingu yao ipo hapa hapa duniani. Tusihukumiane kwa mambo yaliyo nje ya tunachokifanya. Tukianzia hapa, tunaweza kufaidi matunda baadaye.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HAYA YA ZANZIBAR, IKO WAPI TOFAUTI YA DHAMBI YA KUUA NA USHOGA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top