• HABARI MPYA

    Sunday, July 01, 2018

    YANGA WASIPOAMKA SASA WATALIA ZAIDI MSIMU UJAO

    WIKI hii Simba SC imetambulisha wachezaji wake watatu wapya, ambao ni kipa Deogratius Munishi ‘Dida’, beki Muivory Coast, Serge Wawa Pascal na mshambuliaji Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, Meddie Kagere.
    Kufuatia usajili huo, kilio kikafuata kwa mahasimu wao wa jadi, Yanga wakilalamika kwamba Simba wameingilia mipango yao, kwani ni wao ndiyo waliokuwa wanataka kuwasajili wachezaji hao.
    Wanadai eti, wao walikuwa kwenye mipango ya kuwasajili wachezaji hao lakini ajabu mahasimu wao wa jadi, wameingilia kati na kuwasajili.

    Na Yanga wanasema kwamba kwa mara nyingingine Simba SC wameingilia usajili wao kama walivyofanya kwa mshambuliaji Adam Salamba kutoka Lipuli.
    Hii inakuwa mwendelezo wa desturi ya Yanga kulalamika kuporwa wachezaji, baada ya awali kuitupia lawama Singida United eti ili iliingilia usajili wao wa wachezaji kadhaa, akiwemo John Tibar.
    Yanga wanasahau kwamba usajili si maneno bali ni vitendo, unapomtaka mchezaji unakwenda kuzungumza naye na kumsainisha mkataba – je, wao walifanya hivyo kwa nani kati ya Salamba, Dida, Wawa na Kagere?
    Jibu ni hapana, Yanga wanaweza kuwa walikuwa wanawataka tu wachezaji hao lakini wakajikuta hawana uwezo wa kuwasajili hadi wakawahiwa na wapinzani.
    Lakini kama ni hivyo pia, kwa nini Yanga wawe wanawaona wachezaji wanaoamini ni wazuri, lakini wanashindwa kumalizana nao hadi wanachukuliwa na wapinzani? Kuna tatizo.
    Katika mkutano wa Juni 10, mwaka huu Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu hiyo, Tarimba Abbas na Makamu wake, Saidy Meckysadik, kusimamia usajili na mambo mengine muhimu ya klabu kwa sasa.
    Wajumbe walioteuliwa na Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, Hamad Islam, Makaga Yanga, Ridhiwani Kikwete, Majjid Suleiman na Hussein Ndama.   
    Lakini siku chache baadaye, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Clement Sanga akasema kwamba Kamati ya Tarimba ambayo iliundwa na wanachama yenyewe itasaidia tu ushauri na upatikanaji wa fedha, lakini usajili utaendelea kufanywa na Kamati iliyokuwapo.
    Ina maana Kamati ambayo imeshindwa, imefeli. Imeifikisha klabu kukosa michuano ya Afrika mwakani, kuonekana klabu ya ujanja ujanja isiyojiweza kwa chochote. Ajabu Tarimba alikubaliana na hilo, wakati maazimio ya wanachama Juni 10 yalikuwa tofauti. Wanachama waliipa majukumu kamili Kamati ya Tarimba kuisimamia klabu katika wakati huu mgumu.
    Na hiyo ni baada ya wanachama hao kukubaliana kwa kauli moja kumrejesha madarakani, Mwenyekiti wao Yussuf Mehboob Manji katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harison Mwakyembe, aliyeagiza kufanyika kwa uchaguzi wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu ndani ya miezi miwili.
    Idadi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga imepungua kutoka uongozi uliochaguliwa Juni mwaka 2016 chini ya Mwenyekiti Manji, baada ya kujizulu pia kwa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe watatu, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala na Hussein Nyika.
    Pamoja na Waziri Mwakyembe, Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Huruma Mkuchika ambao walianza kwa kikao cha faragha na uongozi wa Yanga chini ya Kaimu Mwenyekiti, Clement Sanga.
    Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Michezo, Yusuph Singo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya, Jaji John Mkwawa na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya klabu pamoja na Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa.
    Kitu ambacho wanachama wa Yanga wanajua ni; walimpa madaraka kamili Tarimba na Kamati yake kusimamia timu wakati huu mgumu wakisubiri majibu ya Manji kama atakubali kurejea au la.
    Tarimba aliibuka mara moja, wiki iliyopita na akasema wanafanya mambo yao kwa siri ili kuepuka kuwapa faida wapinzani wao na watakapokamilika wataweka hadharani.
    Kwa sasa kinachoendelea Yanga ni vigumu kuelelewa kwa sababu wakati Tarimba amesema wanafanya mambo yao kwa siri, wenzake wanalia kwamba wachezaji wao ndiyo wanaochukuliwa na Simba.
    Watu wengi walikuwa wana matumaini na uteuzi wa Kamati ya Tarimba, kwamba ingetatua matatizo ya klabu kwa haraka, lakini kinachoonekana ni kama Kamati hiyo haijapewa majukumu. Inaitwa Kamati ya ushauri tu na si usimamizi tena wa klabu.
    Maana yake mkutano wa Juni 10 ulikuwa kiini macho tu, kuwahadaa wana Yanga, lakini kila kitu kinabaki kama kilivyo, Yanga ni ya Sanga ni rafiki zake akina Omar Kaaya, Hussein Nyika, Samuel Lukumay na Katibu wao, Charles Boniface Mkwasa.   
    Yanga wapo bado wapo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ambayo itarejea baada ya fainali za Kombe la Dunia na Julai 18 watakuwa wageni wa Gor Mahia nchini Kenya.
    Wakati timu iliyoonekana dhaifu baada ya msimu imeshindwa kuongezewa nguvu kwa usajili wa wachezaji wapya, bado hata wachezaji waliokuwapo waliokuwa wanaibeba Yanga kipindi hicho nao wanaondoka mfano Mzambia, Obrey Chirwa.
    Bado watu wanataka kuwahadaa wanachama eti kila mchezaji wanayemtaka Simba na Singida United wanawachukua, wakati inaonekana kabisa watu pale Jangwani wapo kwa maslahi yao mengine binafsi na si ya klabu.
    Sasa kuna propaganda zinaenezwa eti Manji anataka kufanya kazi na uongozi wa Sanga na ndiyo maana mabadiliko yoyote hayapewi nafasi Yanga, iwe Kamati ya Tarimba au agizo la uchaguzi la Serikali.
    Huu ni wakati sasa wanachama wa Yanga waamke na kuanza kuhoji mambo ya msingi kuhusu klabu yao, vinginevyo watakuwa na msimu mbaya zaidi ujao. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WASIPOAMKA SASA WATALIA ZAIDI MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top