• HABARI MPYA

  Sunday, July 01, 2018

  ONYESHO LA CHRISTIAN BELLA USIKU WA UTAMADUNI WA MSWAHILI NCHINI MAREKANI LAFANA

  Na Mahmoud Zubeiry, MARYLAND
  ONYESHO la mwanamuziki maarufu kutoka nchini Tanzania, Christian Bella mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) limefana usiku huu kwenye ukumbi wa Hampton Inn, eneo la Baltimore Avanue mjini Maryland nchini Marekani.
  Katika onyesho hilo lililoandaliwa na Mtangazaji maarufu wa zamani wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), tangu enzi za Radio Tanzania (RTD), Steven Mgaza ambaye pia kwa hapa Marekani ametangazia kwa muda mrefu Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA), Bella alivutia zaidi kwa wimbo wake Nani Kama Mama.

  Christian Bella akitumbuiza leo kwenye ukumbi wa Hampton Inn, eneo la Baltimore Avanue mjini Maryland nchini Marekani

  Muongoza shughuli (MC), Sunday Shomari wa VoA, alipomtambulisha Bella kwa ajili ya kuingia kutumbuiza, mwanamuziki huyo kipenzi cha wapenzi wa muziki wa dansi na kwa ujumla na muziki wa kizazi kipya Afrika Mashariki alianza na wimbo Nani Kama Mama.
  Bahati mbaya kidogo mwanzoni mitambo ya muziki ilikorofisha na Bella aliyekuwa akiimba kwa kutumia CD na si kupigiwa ala jukwaani akaendelea kuwaburudisha wapenzi wake waliojitokeza ukumbini kwa sauti yake tamu.
  Nyimbo nyingine alizotumbuiza Bella usiku huu ni pamoja na Yako Wapi Mapenzi, Ameondoka, Amerudi Analia na nyinginezo.
  Mwandaaji wa onyesho hilo lililopewa jina Usiku wa Utamaduni wa Mswahili, Mgaza alifungua kwa kumkaribisha Mkurugenzi wa VoA, Mwamoyo Hamza aliyeelezea kwa muhtasari historia ya Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika na Kiswahili nchini Marekani. 
  Watu wapatao 100 waliojitokeza kwenye onyesho hilo, wengine wakiwa na familia zao pamoja na watoto waliburudika na wakapiga picha na Bella wakati na baada ya onyesho.  
  Bella aliahidi wakati mwingine akialikwa nchini Marekani atahakikisha anakwenda na bendi yake ya Malaika ili awape wapenzi wake burudani ya live.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ONYESHO LA CHRISTIAN BELLA USIKU WA UTAMADUNI WA MSWAHILI NCHINI MAREKANI LAFANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top