• HABARI MPYA

    Saturday, July 14, 2018

    YANGA SC YATANGAZA KUWAREJESHA RASMI NGASSA NA KASEKE HUKU YONDAN NA KESSY WAKIGOMA KUSHINIKIZA MIKATABA MIPYA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    HATIMAYE klabu ya Yanga SC ya Dar es Salaam imetangaza rasmi kuwarejesha viungo wake, Deus Kaseke na Mrisho Ngassa ili kuimarisha kikosi chake kuelekea mechi zilizosalia za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika.
    Sasa mashabiki wa Yanga wanasubiri kusikia mshambuliaji Heritier Makambo kutoka DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye inaelezwa jina lakde limetumwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) pamoja na Ngassa na Kaseke kwa ya kucheza Kombe la Shirikisho.
    Ngassa na Kaseke wanafanya idadi ya wachezaji wapya waliosajiliwa rasmi Yanga kufika wanne, baada ya viungo wengine, Feisal Salum kutoka JKU ya Zanzibar na Jaffar Mohammed kutoka Maji Maji ya Songea iliyoshuka Daraja.
    Meneja wa Yanga SC, Hafidh Saleh (kushoto) akimkabidhi jezi ya klabu hiyo, kiungo Mrisho Ngassa (kulia) baada ya kusaini mkataba wa kurejea Jangwani
    Deus Kaseke (kulia) akiwa na Mrisho Ngassa (kushoto) baada ya kusaini mikataba ya kurejea rasmi Yanga

    Mrisho Ngassa (kushoto) aktia dole gumba katika fomu za mkataba wa Yanga pembeni ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Hussein Nyika

    Lakini uongozi wa Yanga unakabiliwa na mtihani juu ya wachezaji waliogoma, kipa Benno Kakolanya, mabeki Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’, Hassan Kessy na Kelvin Yondan ambao wamemaliza mikataba wanataka wasaini mipya.
    Wachezaji wote hao wamesusa mazoezi wakishinikiza kupewa mikataba mipya na angalau Kakolanya, Abdul na Dante walifanya mazoezi kwa siku kadhaa kabla ya leo kuungana na Kessy na Yondan kususa kabisa kufuatia kuona viongozi hawatimizi ahadi.
    Yanga SC inatarajiwa kuteremka uwanjani Jumatano ya Julai 18, mwaka huu mjini Nairobi nchini Kenya kumenyana na wenyeji, Gor Mahia nchini Kenya katika mchezo wa Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika, kabla ya timu hizo kurudi Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano Julai 29.
    Yanga SC haijashinda mechi hata moja kati ya mbili za awali za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa 4-0 na USM Alger nchini Algeria Mei 6 na kutoa sare ya 0-0 na Rayon Sports ya Rwanda mjini Dar es Salaam Mei 16.
    Baada ya hapo, Yanga SC itacheza tena nyumbani, Uwanja wa Taifa ikiwakaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
    Timu mbili za juu katika kundi hilo zitaungana na washindi sita wa makundi mengine manne kwa mechi za nyumbani na ugenini za Robo Fainali na zitakazofuzu zitasonga mbele, Nusu Fainali na baadaye Fainali.
    Bingwa wa Kombe la Shirikisho atapata zawadi ya dola za Kimarekani, 1 250, 000, mshindi wa pili dola 432, 000 wakati timu zitakazoshika nafasi za pili kwenye kila kundi zitapata dola 239, 000 kila moja, nafasio ya tatu dola  239, 000 na za nne dola 150, 000.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC YATANGAZA KUWAREJESHA RASMI NGASSA NA KASEKE HUKU YONDAN NA KESSY WAKIGOMA KUSHINIKIZA MIKATABA MIPYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top