• HABARI MPYA

  Wednesday, July 18, 2018

  YALIYOWAKUTA YANGA KENYA LEO AIBU TUPU ‘WALLAHI’…WAPIGWA 4-0 NA GOR MAHIA KAMA HAWAPO UWANJANI

  Na Mwandishi Wetu, NAIROBI
  YANGA SC imeendelea kuvurunda baada ya kuchapwa mabao 4-0 na wenyeji, Gor Mahia katika mchezo wa Kundi Kombe la Shirikisho Afrika Kombe la Shirikisho Afrika usiku huu Uwanja wa Moi Kasarani mjini Nairobi.
  Yanga sasa inakamalisha mechi zake tatu za mzunguko wa kwanza bila ushindi, ikifungwa mbili zote 4-0, ya kwanza dhidi ya MC Alger nchini Algeria Mei 6 na sare ya 0-0 na Rayon Sport mjini Dar es Salaam Mei 16. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa kutoka Somalia ambao ni Hassan Mohamed Hagi aliyepuliza kipyenga akisaidiwa na Hamza Hagi Abdi na Bashir Sh. Abdi Suleiman, hadi mapumziko tayari Yanga walikuwa wamekwishachapwa 2-0.

  Alianza mshambuliaji wa kimataifa wa Rwanda, Jacques Tuyisenge kutumia makosa ya safu mbofu ya ulinzi ya Yanga kuwahi kutokea miaka karibuni kufunga bao la kwanza dakika ya 21 akimalizia krosi ya Samuel Onyango.
  Yanga walifungwa bao hilo wakitoka kulishambulia lango la Gor Mahia kwa kona mbili mfululizo baada ya wenyeji kuanza kwa kuutawala mchezo kwa takriban dakika zote 10 za mwanzo.  
  Mshambuliaji Muivory Coast, Ephrem Guikan akamalizika pasi ya kiungo Mkenya, Francis Kahata kuifungia Gor Mahia bao la pili dakika ya 44. 
  Kipindi cha pili Yanga SC walikianza kwa kusukuma mashambulizi langoni mwa Gor Mahia kusaka mabao ya kusawazisha, lakini hiyo ikawapa nafasi wapinzani wao kuona njia za kuwafikia kuwaongeza mabao.
  Beki wa pembeni, Mwinyi Hajji Mngwali aliyekuwa anacheza kiungo leo akajifunga dakika ya 65 katika harakati za kuokoa kabla ya Guikan kukamilisha shangwe za mabao Gor Mahia dakika ya 86.
  Baada ya leo, Yanga wataikaribisha Gor Mahia Julai 29 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano kabla ya kurudiana na USM Alger Agosti 19 na kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
  Kikosi cha Gor Mahia kilikuwa; Shaaban Odhoji, Philemon Otieno, Haron Shakava, Charles Momanyi, Godfrey Walusimbi, Humphrey Mieno, Samuel Onyango/ Wellington Ochieng dk90, Ephrem Guikan, Francis Kahata/ Cercidy Okeyo Lumumba dk81, Benard Ondiek na Jacques Tuyisenge/ Francis Mustafa dk52.
  Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul, Andrew Vincent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Gardiel Michael, Mwinyi Mngwali/Amissi Tambwe dk80, Papy Kambamba Tshishimbi, Ibrahim Ajib/Emmanuel Martin dk77, Juma Mahadhi, Yohana Mkomola/Said ‘Ronaldo’ Mussa dk53 na Pius Buswita.


  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YALIYOWAKUTA YANGA KENYA LEO AIBU TUPU ‘WALLAHI’…WAPIGWA 4-0 NA GOR MAHIA KAMA HAWAPO UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top