• HABARI MPYA

  Thursday, July 19, 2018

  ULIMWENGU AFUNGA LA PILI EL HILAL YATOKA SARE 2-2 NA WAMAKONDE KOMBE LA SHIRIKISHO

  Na Mwandishi Wetu, OMDURAN
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu usiku wa jana ameifungia bao la pili El HIlal ikitoka sare ya 2-2 na Songo ya Msumbiji katika mchezo wa Kundi B Kombe la Shirikisho Afrika Uwanja wa Al-Hilal mjini Omdurman.
  Ulimwengu alifunga bao hilo dakika ya 36 akimalizia pasi ya Mohamed Bashir, aliyefunga bao la kwanza dakika ya pili tu ya mchezo kwa pasi ya Sharaf Eldin Ali. 
  Dakika mbili kabla ya mapumziko, Songo ikafanikiwa kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na kiungo Mmalawi, Frank Banda dakika ya 43 akimalizia pasi ya beki, Pascoal Amorim kabla ya mshambuliaji mkongwe Helder Pelembe kuisawazishia timu hiyo dakika ya 87.
  EL Hilal imekamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza bila ushindi, baada ya sare ya pili jana na mechi moja ya kufungwa na sasa inafikisha pointi mbili tu.
  Ulimwengu amejiunga na El Hilal mwishoni mwa mwezi Mei baada ya kuachana na AFC Eskilstuna ya Sweden ambayo alishindwa kuitumikia vyema kutokana na kuandamwa na maumivu ya goti yaliyomlazimu kufanyiwa upasuaji katika hospitali ya Taasisi ya Sayansi ya Michezo mjini Cape Town, Afrika Kusini mwaka jana na kupitia kipindi kirefu cha mazoezi ya kujiweka fiti.
  Ulimwengu alikwenda kwa watalaamu nchini Italia kufanyishwa mazoezi maalum ya kumuweka fiti haraka arejee uwanjani, ambayo hakika yamemsaidia hadi kuanza vyema na vigogo wa Sudan.
  Maumivu ya goti yalikuwa yakimsakama Ulimwengu tangu alipojiunga na Eskilstuna Januari mwaka jana akitokea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kiasi cha kushindwa kucheza. 
  Ulimwengu aliyezaliwa Juni 14, mwaka 1993 aliibukia katika taasisi ya soka Tanzania (TSA) mwaka 2008, kabla ya mwaka 2009 kwenda kuanza kukomazwa Ligi Kuu katika klabu ya Moro United alikokuwa akicheza kwa mkopo hadi mwaka 2010 alipokwenda akademi ya AFC Eskilstuna ya Sweden, alikocheza hadi mwaka 2011  alipochukuliwa na timu ya vijana ya Mazembe.
  Alicheza U-20 ya Mazembe kwa msimu moja kabla ya kupandishwa rasmi timu ya wakubwa mwaka 2012 na moja kwa moja kuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza hadi anamaliza Mkataba wake Oktoba mwaka jana.
  Ulimwengu alihamia Ulaya baada ya kushinda mataji makubwa akiwa na Mazembe kama Ligi ya Mabingwa Afrika, Super Cup ya Afrika na pamoja na kucheza Klabu Bingwa ya Dunia.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: ULIMWENGU AFUNGA LA PILI EL HILAL YATOKA SARE 2-2 NA WAMAKONDE KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top