• HABARI MPYA

    Tuesday, July 17, 2018

    SANGA NA TARIMBA WAMALIZA TOFAUTI ZAO, WAKUBALIANA KUFANYA KAZI PAMOJA KUISAIDIA YANGA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KAIMU Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga na aliyekuwa Menyekiti wa Kamati Maalum ya Kusimamia shughuli za Uendeshwaji wa klabu, Tarimba Abbas leo wamekubaliana kuzika tofauti zao.
    Makubaliano hayo yamefikiwa katika kikao kilichofanyika ofisini kwa Abbas Tarimba, Oysterbay mjini Dar es Salaam leo na pongezi kwa tawi la Viva Young (Yanga) International lililojitolea kuhakikihsa wawili hao wanazika tofauti zao.
    Habari kutoka kwenye kikao hicho zimesema kwamba tawi la Viva Young (Yanga) International lilifanya mawasiliano na kila mmoja miongoni mwa wawili hao kwa lengo la kuwakutanisha kumaliza tofauti zao.
    Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga (kushoto) akiwa na Mwenyekiti wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas (katikati) baada ya kikao cha usuluhishi leo. Kulia ni Omary Kimota. Picha ya chini mwingine kulia ni Deo Mutta 
    “Baada ya makubaliano, viongozi wetu hawa walikutana na kuzungumza leo na kwa kifupi wamegundua hakukuwa na tofauti kabisa miongoni mwao, isipokuwa kupelekewa au kupokea taarifa zisizo sahihi na kosa walilolifanya ni kutowasiliana baada ya taarifa hizo, kila mmoja akawa anachukua hatua hadi kufika ilipofikia,”kimsema chanzo.  
    Baada ya kikao hicho, Sanga na Tarimba wamekubaliana kuzika tofauti zao na kuunganisha nguvu zao katika kuhakikisha wanaisaidia Yanga kuanzia sasa.
    “Nafikiri nisiwe mzungumzaji wao, wala mzungumzaji wa klabu, wao watazungumza wenyewe, au klabu itatoa taarifa, ila kwa sasa nataka nikuhakikishie hakuna tena mgawanyiko ndani ya klabu na tofauti baina ya Mwenyekiti na Mwenyekiti wetu wa zamani (Tarimba) zimezikwa,”kimeongeza chanzo.
    Wiki iliyopita Tarimba alijiuzulu Uenyekiti wa Kamati Maalum ya Kusimamia shughuli za Uendeshwaji wa klabu baada ya kuarifiwa kwamba anapingwa na Mwenyekiti wa klabu, Sanga.
    Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga SC waliunda Kamati ya watu tisa chini ya Rais wa zamani wa klabu, Tarimba Abbas na wanachama wa Yanga Kusimamia Shughuli mbalimbali za klabu hiyo kufuatia kile kinachoonekana kuelemewa kwa uongozi uliopo madarakani sasa chini ya Kaimu Mwenyekiti, Sanga.
    Mwenyekiti Mteule wa Kamati hiyo ni Tarimba Abbas, Makamu wake, Saidy Meckysadik na Wajumbe wa Kamati hiyo ni Abdallah Bin Kleb, Hussein Nyika, Samuel Lukumay, Lucas Mashauri, Yusuphed Mhandeni, 
    Na hiyo ni kutokana na kupwaya kwa Kamati ya Utendaji kutoka uongozi uliochaguliwa Juni mwaka 2016 imepungua mno baada ya kujiuzulu kwa Mwenyekiti mwenyewe, Yussuf Manji na Wajumbe wa Omary Said Amir, Salum Mkemi, Ayoub Nyenzi na Hashim Abdallah.  
    Waliobaki katika Kamati ya Utendaji pamoja na Sanga ni Wajumbe wanne, Siza Augustino Lymo, Tobias Lingalangala, Samuel Lukumay na Hussein Nyika.
    Ilidaiwa jana Sanga alikutana na viongozi wa Matawi na kuiponda Kamati ya Tarimba huku akisema kwamba Mwenyekiti wa klabu, Yussuf Manji ameomba miezi mitatu kabla ya kurejea kuendelea na majukumu yake klabuni.
    Juni 10, mwaka huu katika Bwalo la Maafisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam, wanachama wa Yanga SC pamoja na kuunda Kamati ya Tarimba, pia waligomea ombi la Mei mwaka jana la Mwenyekiti wao, Manji kujiuzulu na kusema bado wanamtambua kama kiongozi wao mkuu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SANGA NA TARIMBA WAMALIZA TOFAUTI ZAO, WAKUBALIANA KUFANYA KAZI PAMOJA KUISAIDIA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top