• HABARI MPYA

  Wednesday, July 18, 2018

  MAHAKAMA YATOA SIKU SABA HANS POPPE, LAUWO KUONGEZWA KWENYE KESI YA AVEVA NA KABURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa siku saba kwa upande wa mashitaka wawe wamebadilisha hati ya mashitaka katika kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili, Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na makamu wake, Godfrey Nyange maarufu kama Kaburu.
  Aveva ambaye alikuwa hajafika mahakamani hapo kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa figo, jana alifika mahakamani hapo huku afya yake ikionekana bado haijatengemaa.
  Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba ametoa amri hiyo leo baada ya Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai kudai kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa na kwamba Mahakama ilitoa amri ya kubadilisha hati ya mashitaka na kuongeza washitakiwa ambao ni Mwenyekiti wa Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe na Franklin Lauwo.

  Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe (kulia) akiwa na Makamu wake, Kassim Dewji kushoto 

  Wakili Swai alidai kuwa jukumu la kubadilisha hati hiyo liliachwa kwa Wakili wa Serikali, Shadrack Kimaro na kwamba alisafiri kwenda Moshi na sasa amerudi kwa ajili ya kutekeleza amri hiyo hivyo wanaomba muda wa kukamilisha kaz hiyo.
  Alidai pia wanaomba siku saba kwa ajili ya kukamilisha mabadiliko ya hati ya mashitaka. Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko alidai kuwa hati ya mashitaka iliyotakiwa kufanyiwa mabadiliko ni ya watu wanne   na wenyewe wapo wawili  hivyo wanaomba wafanye haraka kubadilisha hati hiyo. Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 26, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
  Kwa pamoja, Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashitaka matano ya uhujumu uchumi, ikiwamo kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na utakatishaji wa fedha ambazo ni dola za Kimarekani 300,000, zaidi ya Sh. Milioni 600 za Tanzania.
  Aveva na Kaburu walipelekwa mahabusu, gereza la Keko, Dar es Salaam Juni 29, mwaka huu kufuatia kusomewa mashitaka matano Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
  Wawili hao walifikishwa mahakamani mapema asubuhi ya Juni 29, mwaka huu na kusomewa mashitaka hayo matano mchana wake, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodai kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni Rais Aveva na Makamu wake, Kaburu kiasi cha dola za Kimarekani 300,000.
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwenye benki ya CRDB tawi la Azikiwe mjini Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sharia, ambapo inadaiwa Rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka kwenye benki ya  Barclays tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu aliyemsadia Aveva kutakatisha fedha katika Barclays baada ya kughushi nyaraka.
  Na Aprili 30, mwaka huu Mahakama hiyo iliwaongeza Hans Poppe na mkandarasi wa uwanja wa klabu hiyo, Frank Peter Lauwo katika kesi hiyo na kuagiza wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayowakabili.
  Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba baada ya Swai kudai amewatafuta washitakiwa hao tangu Machi mwaka huu bila mafanikio na kuomba hati ya kuwakamata.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAHAKAMA YATOA SIKU SABA HANS POPPE, LAUWO KUONGEZWA KWENYE KESI YA AVEVA NA KABURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top