• HABARI MPYA

    Friday, November 08, 2013

    STEWART HALL ANGEFUKUZWA SIKU YOYOTE AZAM FC, NA ATAENDELEA KUFUKUZWA

    Na Mahmoud Zubeiry, aliyekuwa Chamazi
    MAKOCHA wanaajiriwa ili wafukuzwe, huo ni msemo maarufu sasa na wakati fulani, kocha maarufu duniani, Jose Mourinho alisema; “So I know all about the ups and downs of football, I know that one day I will be sacked,”.
    Mourinho alikuwa anamaanisha anaifahamu kwa undani soka na anafahamu iko siku atafukuzwa.
    Huwezi kustaajabu, Stewart Hall amefukuzwa tena Azam FC, baada ya kurejeshwa Desemba mwaka jana na fahamu iko siku Jose Mourinho atafukuzwa tena Chelsea kama hataondoka mwenyewe.
    Hayo ndiyo maisha ya makocha, kuajiriwa na kufukuzwa. Jana, Muingereza, Stewart John Hall aliwaaga wachezaji na benchi la Ufundi mara tu baada ya mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baina ya timu hiyo na Mbeya City ulioisha kwa sare ya kufungana mabao 3-3 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    “Ni kweli nimewaaga wachezaji na wenzangu katika benchi la Ufundi, nimewaambia imebidi niondoke kwa sababu nimepata kazi sehemu nyingine. Lakini pia wamiliki wa timu wameridhia niondoke na ninaondoka vizuri, nawatakia kila heri,”alisema Stewart alipozungumza na BIN ZUBEIRY jioni ya jana.
    Hii inakuwa mara ya pili, Stewart kuondoka Azam, baada ya awali Agosti mwaka jana kuondolewa kiasi cha mwaka mmoja tu tangu aajiriwe akitoka kufundisha timu ya taifa ya Zanzibar.
    Stewart alifukuzwa baada ya kuiwezesha Azam kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu na Kombe la Kagame, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pamoja na kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi na nafasi yake ikachukuliwa na Mserbia, Boris Bunjak.
    Hata hivyo, baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Stewart aliyehamia Sofapaka ya Kenya, alirejeshwa Azam kufuatia kutimuliwa kwa Mserbia, Bunjak.
    Stewart akarudia kuipa nafasi ya pili Azam katika Ligi Kuu na kuipa Kombe la Mapinduzi pamoja na kuiwezesha kutwaa taji la Ngao ya Hisani, michuano iliyofanyika mjini Kinshasa, DRC, Desemba mwaka jana. 
    Bado haijajulikana sasa Azam itaangukia mikononi mwa kocha gani, ikiwa sasa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu umemalizika na wachezaji wanakwenda mapumzikoni.
    Stewart ni kocha wa nne kuondolewa Azam tangu ianze kucheza Ligi Kuu msimu wa 2007/2008 baada ya Wabrazil Neider dos Santos na Itamar Amorin na Mserbia Bunjak.
    Stewart Hall ameaga Azam jana

    Azam imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, ikiwa katika nafasi ya pili kwa pointi zake 27 sawa na Mbeya City, nyuma ya mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 28.  
    Wakati fulani katikati ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, baada ya Azam kulazimishwa sare ya 1-1 na Ashanti United, wachezaji waliambiwa hawajitumi na wakakaripiwa na uongozi- baada ya hapo kweli wakaongeza juhudi na kuanza kuiwezesha timu kushinda mfululizo.
    Azam ikazifunga zote Simba na Yanga na kuendelea kushinda hadi ilipokuja kukwama kwa sare ya 3-3 na Mbeya City jana, timu ambayo haijafungwa mechi yoyote msimu huu. Azam haijapoteza mechi msimu huu na kama si sare ya kizembe mbele ya Ashanti, leo ingemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa kileleni.
    Unaweza kujua tatizo la Azam liko wapi hadi kocha anaondolewa? Haichezi soka ya kuvutia, hilo moja linatajwa, wachezaji chipukizi hawapewi nafasi, hilo lingine.
    Watanzania wameingiwa na maradhi ya kupenda pasi nyingi, soka ya Barcelona. Zikigongwa pasi wanashangilia sana. Katika mchezo dhidi ya Ruvu Shooting, Azam walishinda 3-0 lakini wapinzani wao walipiga pasi nyingi sana. Mfumo wa Stewart unaweza kuuona ni wa kushambulia moja kwa moja kwa sababu ina watu wenye kasi pembeni na mbele na ndiyo maana imevuna mabao mengi.
    Hilo suala la kupandisha vijana, hayo mambo yanakwenda kwa utaratibu na kocha yeyote hawezi kuthubutu kumjaribu mchezaji katika Ligi- labda itokee dharula kama iliyotokea Stewart akawapandisha Joseph Kimwaga na Farid Mussa.
    Mapema wakati wa usajili wa msimu huu, Stewart alisema hatasajili mchezaji mpya, kwa sababu anapandisha vijana wa akademi na kama kuongeza mtu mpya ni hadi Januari akiona udhaifu kwenye timu.
    Mwanzoni tu mwa msimu alianza kumpanga kwenye kikosi cha kwanza kipa kutoka akademi, Aishi Manula na akampa mechi zaidi kwa kupokezana na Mwadini Ally.
    Stewart ametambulisha vipaji vipya ndani ya Azam na watu wameona wachezaji kama Khamis Mcha ‘Vialli’, Himid Mao, Waziri Salum ukiachilia mbali Aishi, Kimwaga na Farid na amekuwa na misimamo ya kukumbatia wachezaji chipukizi.
    Huyu Salum Abubakar ‘Sure Boy’ alianza kuwa mchezaji wa uhakika kwenye kikosi cha kwanza Azam baada ya Stewart kufika Chamazi- kabla ya hapo alikuwa anacheza kwa nadra.    
    Mourinho aliondolewa Chelsea mara ya kwanza si kwa sababu ya matokeo, bali aliambiwa timu haichezi soka ya kuvutia na aliporejeshwa safari hii akaahidi itachezwa kandanda ya ‘Kibarcelona’ Stamford Bridge, maana yake anabadilisha falsafa.
    Stewart ameridhika kuondoka na falsafa zake zisizokubalika Azam, lakini anaiachaia klabu kumbukumbu nzuri ya mataji matatu, mawili ya Mapinduzi, moja Ngao ya Hisani michuano iliyofanyika DRC na Medali za Fedha mbili za Ligi Kuu, moja ya Kombe la Kagame.
    Ikishiriki kwa mara ya kwanza michuano ya Afrika mwaka jana, Stewart aliifikisha Azam 16 bora ya Kombe la Shirikisho na ilibakia kidogo iingie kwenye mechi za mchujo kuwania kucheza hatua ya makundi kama si John Bocco kukosa penalti dakika nane kabla ya filimbi ya mwisho dhidi ya AS FAR Rabat nchini Morocco.  
    Anaiacha timu katika nafasi nzuri kwenye Ligi Kuu, ya pili ikizidiwa pointi moja tu (28-27) na mabingwa watetezi, Yanga SC walio kileleni. Anaiacha timu haijapoteza hata mechi moja hadi sasa katika ligi. Kwangu Stewart anabakia katika orodha ya makocha wazuri waliowahi kufanya kazi Tanzania siku za karibuni. Kocha asiye mbinafsi, anayewapa nafasi wasaidizi wake na kuwaamini. Anayejua kuishi na wachezaji. Mchapakazi.
    Kubwa ni kocha aliyepandisha hadhi ya Azam ndani ya muda mfupi tu. Nenda Stewart, usingefukuzwa jana, ungefukuzwa siku yoyote na popote uendako utaendelea kufukuzwa. Na atakayekuja Azam badala yako, naye atafukuzwa pia. Hayo ndiyo maisha ya makocha, wanaajiriwa ili wafukuzwe.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STEWART HALL ANGEFUKUZWA SIKU YOYOTE AZAM FC, NA ATAENDELEA KUFUKUZWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top