• HABARI MPYA

  Wednesday, July 04, 2018

  YANGA YAONGEZA WATATU KOMBE LA SHIRIKISHO, NI NGASSA, KASEKE NA MSHAMBULIAJI MKONGO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeimarisha kikosi chake kwa ajili ya mechi nne zijazo za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika kwa kusajili wachezaji watatu wapya, ambao ni viungo wazawa Deus Kaseke, Mrisho Ngassa na mshambuliaji Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
  Habari ambazo Bin Zubeiry Sports – Online imezipata kutoka Yanga SC wachezaji hao ambao wote ni huru baada ya kumaliza mikataba na klabu zao, Makambo kutoka DC Motema Pembe ya Lubumbashi, Kaseke kutoka Singida United na Ngassa kutoka Ndanda FC majina yao yametumwa makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  Wakati Makambo ni mchezaji ambaye ameletwa na kocha mpya wa Yanga, Mkongo Mwinyi Zahera, Kaseke na Ngassa wote wanarejea nyumbani baada ya kuwa wameitumikia awali klabu hiyo.

  Amerudi nyumbani; Mrisho Ngassa akiwatoka wachezaji wa Simba SC katika mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita 

  Yanga SC haijashinda mechi hata moja kati ya mbili za awali za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kufungwa 4-0 na USM Alger nchini Algeria Mei 6 na kutoa sare ya 0-0 na Rayon Sports ya Rwanda mjini Dar es Salaam Mei 16.
  Itateremka tena uwanjani Jumatano ya Julai 18, mwaka huu mjini Nairobi nchini Kenya kumenyana na wenyeji, Gor Mahia nchini Kenya kabla ya timu hizo kurudi Dar es Salaam kwa mchezo wa marudiano Julai 29.
  Baada ya hapo, Yanga SC itacheza tena nyumbani, Uwanja wa Taifa ikiwakaribisha USM Alger Agosti 19 kabla ya kwenda kukamilisha mechi zake za kundi hilo kwa kumenyana na wenyeji, Rayon Sport Agosti 28.
  Timu mbili za juu katika kundi hilo zitaungana na washindi sita wa makundi mengine manne kwa mechi za nyumbani na ugenini za Robo Fainali na zitakazofuzu zitasonga mbele, Nusu Fainali na baadaye Fainali.
  Bingwa wa Kombe la Shirikisho atapata zawadi ya dola za Kimarekani, 1 250, 000, mshindi wa pili dola 432, 000 wakati timu zitakazoshika nafasi za pili kwenye kila kundi zitapata dola 239, 000 kila moja, nafasio ya tatu dola  239, 000 na za nne dola 150, 000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA YAONGEZA WATATU KOMBE LA SHIRIKISHO, NI NGASSA, KASEKE NA MSHAMBULIAJI MKONGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top