• HABARI MPYA

  Wednesday, July 04, 2018

  SIMBA SC NA SINGIDA UNITED ZATOA SARE 1-1 NA ZOTE KUFUZU ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME

  Na Sada Salmin, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imemaliza kama kinara wa Kundi C michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya sare ya 1-1 na Singida United jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
  Kwa sare hiyo, Simba SC inamaliza na pointi saba, sawa na Singida United, lakini Wekundu wa Msimbazi wanamalizia juu kutokana na wastani wao mzuri wa mabao.
  Katika mchezo wa leo, Simba walitangulia kupata bao dakika ya 15, mfungaji mshambuliaji mpya, Meddia Kagere Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda, akimalizia kazi nzuri ya kiungo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia, Jamal Mwambeleko.
  Salum Chuku wa Singida United (kushoto) akipiga mpira mbele ya Meddie Kagere wa Simba leo Uwanja wa Taifa

  Singida United walisawazisha bao hilo dakika ya 35 kupitia kwa mshambuliaji mpya pia, Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman ambaye aliiadhibu timu yake ya zamani akimalizia kazi nzuri ya mchezaji mwingine mpya, John Tibar.
  Mechi nyingine za leo za Kombe la Kagame, APR ya Rwanda imeichapa mabao 4-1 Dakadaha ya Somalia na kumaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi C kwa pointi zake tatu, baada ya kupoteza mechi zake mbele ya Simba na Singida United.
  Kikosi cha Simba SC leo kilikuwa: Deo Munishi, Mwinyi Kazimoto, Nicholas Gyan, Muzamil Yassin, Pascal Wawa, Jamal Mwambeleko/Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ dk85, Said Ndemla, Meddie Kagere, Moses Kitandu/ Marcel Kaheza dk66, Mohammed Rashid/Adam Salamba dk46 na James Kotei. 
  Singida: Peter Manyika, Kennedy Juma, Boniface Maganga, Salum Chuku, Salum Kipaga, Yussuf Kagoma, Danny Lyanga, Kenny Ali/ Nizar Khalfan dk87, Elivter Mpepo/ Benedict Junior Aymerick dk60, Habib Kyombo na John Tibar/ Amara Diaby dk69.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC NA SINGIDA UNITED ZATOA SARE 1-1 NA ZOTE KUFUZU ROBO FAINALI KOMBE LA KAGAME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top