• HABARI MPYA

  Sunday, July 15, 2018

  MAWAZO YA WATU WALIOCHOKA KIFIKRA HAYAWEZI KUENDELEA KUONGOZA SOKA YA TANZANIA

  KUANZIA msimu ujao wa 2018-2019 klabu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara zitaruhusiwa kusajili hadi wachezaji 10 wa kigeni, likiwa ni ongezeko la wachezaji watatu kutoka saba wa msimu uliopita.
  Hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kilichofanyika Julai 12, mwaka huu makao makuu ya shirikisho hilo, Uwanja wa Karume Ilala mjini Dar es Salaam.
  Na kikao hicho kilichoongozwa na Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia kiliridhia klabu kutumia hata wachezaji 10 wote wa wakati mmoja uwanjani kwa mashindano yote.

  Akitangaza maamuzi hayo wiki hii, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema; “Uamuzi huo umelenga katika kuboresha na kuleta ushindani zaidi kwenye Ligi pamoja na kupandisha viwango vya wachezaji wazawa,”.
  Maamuzi haya yanamaanisha Tanzania inazidi kuvunja rekodi yake ya matumizi ya wachezaji wengi wa kigeni miongoni mwa nchi za Afrika, kwani hata hao saba tayari ilikuwa idadi kubwa zaidi barani.
  Nchi pekee iliyobaki ambayo ilikuwa haina utaratibu mzuri wa matumizi ya wachezaji wa kigeni, ilikuwa ni Rwanda ambayo nayo sasa imeamua kuweka sheria na udhibiti wa hali ya juu kuhakikisha inatoa nafasi pana kwa wachezaji wa nyumbani kucheza ligi yao.
  Nchi zote kubwa Afrika, zikiwemo zile zinazotawala mashindano ya klabu barani zina sharia ya matumizi ya wachezaji wachache wa kigeni katika Ligi zao.
  Nchi nyingi za Kaskazini mwa Afrika zikiwemo Morocco, Tunisia na Misri kila timu inaruhusiwa kusajili wachezaji wanne tu wa kigeni.
  Mwaka 2016 Algeria ilizuia kabisa wachezaji wa kigeni katika Ligi yao, kabla ya kuruhusu tena mwaka jana, tena wachezaji wawili tu na ambao hawazidi umri wa miaka 30.
  Afrika Kusini ni moja ya nchi zenye kuruhusu idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, nao ni watano tu kusajili na kuchezesha kwa wakati mmoja.
  Tunisia imeweka sheria ngumu ya kusajili wachezaji wa kigeni, ambayo ni kwanza awe na umri kuanzia miaka 19 na awe amechezea timu za taifa za vijana za nchi yake, kikosi cha pili cha timu ya taifa ya nchi yake na kwa ujumla awe amecheza mechi zisizopungua 10 za timu ya taifa.
  Nchi ya Kaskazini ambayo bado haijawa na sheria kali ya udhibiti wa wachezaji wa kigeni ni Libya ambako nako hakuna timu ya wachezaji zaidi ya sita.  
  Lakini hata Afrika Magharibi kuna sharia ya udhibiti wa wachezaji wa kigeni, kuhakikisha wachezaji wazawa wanapewa nafasi zaidi.
  Lengo na kutoa uwanja mpana kwa wachezaji wazawa ni kuwapa frusa ya kucheza na kukuza viwango vyao, ili baadaye waje kuzisaidia timu zao za taifa.
  Na ili uwe na mchezaji timamu wa kukusaidia kushindana kuwania tiketi ya fainali kama CHAN na AFCON lazima awe ana uzoefu wa kucheza michuano ya Afrika.
  Tanzania ina nafasi mbili za kucheza michuano hiyo, ikiingiza timu moja Ligi ya Mabingwa na moja nyingine Kombe la Shirikisho, ambako mara nyingi timu zetu zimekuwa zikitolewa katika hatua za mwanzoni.
  Na kwa sheria mpya ya kusajili wachezaji 10 wa kigeni na kutumia wote kwa wakati mmoja, tarajia klabu kubwa na Azam, Simba na Yanga ambazo mara nyingi ndiyo hucheza mashindano ya Afrika vikosi vyao vitakidhi matakwa ya kanuni, yaani kuwa na wachezaji 10 katika usajili na uwanjani wakati wa mechi.
  Timu yetu ya taifa kwa sasa imekuwa ikiundwa na wachezaji wengi kutoka Azam, Simba na Yanga timu ambazo zinashiriki mashindano mengi na maana yake zinakua wachezaji wa kiwango bora zaidi kwa timu ya taifa.
  Sasa kama Azam, Simba na Yanga zitakuwa na wachezaji 10 wa kigeni na ambao zinaweza kuwatumia wote kwa wakati mmoja – tutarajie wachezaji wa timu ya taifa watatoka timu ambazo hazichezi mashindano makubwa. 
  Na kama tulikuwa tukifungwa mabao saba na Algeria tukiwa na timu yenye wachezaji wenye uzoefu wa mechi kubwa, siku tutakapoanza kuwa na timu ya taifa ya wachezaji wa timu zinazopigania kuepuka kushuka daraja hali itakuwaje?  
  Bado sijapata majibu mwafaka TFF wamefikiria nini kuongeza idadi ya wachezaji 10 wa kigeni katika matarajio ya kupunguza japo hadi watano – kwa sababu zilizoelezwa hazina mashiko. 
  Hoja zinazotolewa ni eti wachezaji wazawa waliopo timu kubwa hawajitumi, hivyo suluhisho na kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni – lakini ukirejea nyuma klabu zetu zilifikia mafanikio makubwa bila wachezaji wa kigeni.
  Yanga walicheza Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika 1969, 1970 na 1998 ulipoanza kutumika mfumo wa makundi na Simba walifika Nusu Fainali ya Klabu Bingwa mwaka 1974 na fainali ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kama vikosini kulikuwa kuna wageni ni wale waliokuja nchini kama wakimbizi kutoka Kongo na Burundi. 
  Timu zinawalalamikia wachezaji wazawa wakati hata hao wa kigeni wakisajiliwa wanachuja baada ya muda mfupi, mfano Laudit Mavugo wa Burundi kutokana tu kutokuwa na utaratibu mzuri wa kuwalea wachezaji – ikiwemo kutokuwa na Uwanja wa mazoezi. 
  Na badala ya kujikita kwenye tatizo la msingi kama CAF inayoaelekeza katika Club Licensing, timu zewe na Uwanja rasmi wa mazoezi, tunakimbilia kuongeza idadi ya wachezaji wa kigeni.
  TFF ilipaswa kusimamia mambo ya msingi kwanza, kama kuhakikisha sheria ya Club Licensing inatekelezwa kikamilifu – badala yake wanataka kutumia njia ya mkato kuwa na ligi ya ushindani kwa kujaza wageni pasipo kuzingatia maslahi ya soka ya nchi kwa ujumla. 
  China kwenyewe sasa hivi timu zinaruhusiwa kusajili wachezaji watano tu wa kigeni na kutumia watatu tu uwanjani kwa wakati mmoja, ujasiri huu Rais wa TFF, Karia na wenzake katika Kamati ya Utendaji wameupata wapi?
  Siwezi kuingia kwenye mawazo ya viongozi wa TFF, lakini ninachokiona ni mawazo yanayofanana na watu waliochoka kifikra na ambao hawastahili kupewa muda zaidi wa kuendelea kuongoza soka ya Tanzania. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAWAZO YA WATU WALIOCHOKA KIFIKRA HAYAWEZI KUENDELEA KUONGOZA SOKA YA TANZANIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top