• HABARI MPYA

  Wednesday, July 18, 2018

  GWIJI WA YANGA SC, CHARLES BONIFACE MKWASA KUJIUZULU UKATIBU MKUU KWA SABABU ZA KIAFYA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KAIMU Katibu Mkuu wa Yanga SC na gwiji wa klabu, Charles Boniface Mkwasa amekabidhi barua ya kujiuzulu kwa sababu za kiafya.
  Mkwasa aliyeanza kuitumikia Yanga SC kama mchezaji miaka ya 1980, baadaye kocha kuanzia miaka ya 1999 kabla ya kuingia kwenye uongozi miaka miwili iliyopita, ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba hali yake kiafaya si nzuri.
  “Hospitali nimeshauriwa kupumzika. Hata hivi ninaongea na wewe kwa simu basi tu, nimeambiwa nipunguze hata kuongea kwa simu kutokana na matatizo yangu,”amesema.  
  Mkwasa ni kiungo hodari wa zamani wa kimataifa nchini na mume wa mwandishi wa habari na mtangazaji wa zamani wa Redio na Televisheni nchini, Betty Chalamila Mkwasa aliyeng’ara RTD na baadaye Redio One na ITV, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya wa zamani.
  Charles Boniface Mkwasa atakabidhi barua ya kujiuzulu, wakati wowote kwa sababu za kiafya.

  Charles alizaliwa Aprili 10 mwaka 1955 mjini Morogoro, ambako alipata elimu yake ya Msingi na sekondari na kisoka aliibukia katika timu ya Mseto FC ya Morogoro mwaka 1973 kama beki wa kati na kiungo hodari ambayo aliiwezesha kuwa timu ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania mwaka 1975.
  1976 akahamia Tumbaku pia ya Morogoro aliyoichezea hadi mwaka 1979 alipotua Yanga SC, wakati huo ikiwa imepoteza makali yake kufuatia mgogoro mkubwa wa mwaka 1976 ulioigawa timu hiyo na kuzaliwa Pan Africans.
  Baada ya nyota wengi wa Yanga SC kukimbilia Nyota ya Morogoro na baadaye kwenda kuasisi Pan Africans, timu hiyo ya Jangwani ikaanza kujiumba upya kwa kusajili nyota wengine, Mkwasa akiwa miongoni mwao.
  Akiwa na chipukizi wenzake wa wakati huo kama Ahmad Amasha, Juma Mkambi ‘Jenerali’, Mkwasa waliiwezesha Yanga SC kurejesha makali na kutwaa tena ubingwa wa Tanzania mwaka 1981 tangu walipotwaa mara ya mwisho 1974.
  Alidumu Yanga SC hadi mwaka 1989 alipoamua kutungika daluga zake za kuwa kocha mchezaji wa timu ya Super Stars ya Dar es Salaam. Lakini tayari mwaka 1988 alikwishaanza kupata mafunzo ya ukocha.
  Baada ya kozi tatu za awali za ukocha Tanzania, mwaka 1991 Mkwasa alikwenda Brazil alipochukua Diploma na aliporejea akajiunga na Yanga SC kama Msaidizi wa Syllersaid Mziray (sasa marehemu).
  Mkwasa ambaye mwaka 2000 alikwenda kusomea tena ukocha Ujerumani na kupata Diploma nyingine, kwa sasa ana leseni A ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) aliyoipata mwaka jana na pia ni Mkufunzi Daraja la Kwanza wa CAF tangu 2014.
  Mbali na kufundisha Super Star na Yanga SC kuanzia 1989 hadi 1993, Mkwasa alifundisha pia iliyokuwa timu ya Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), maarufu kama Sigara kuanzia 1994 hadi 1996 alipokwenda Al Khaboura ya Oman alikodumu hadi 1999.
  Alirejea nchini 1999 na kuwa Kocha Mkuu wa  Tanzania Prisons ya Mbeya, ambayo mwaka 1999 aliipa ubingwa wa iliyokuwa Ligi ya Muungano.
  Kwa mafanikio, Yanga SC wakamchukua kama kocha Mkuu mwaka 2001, akimrithi Raoul Jean Pierre Shungu kutoka DRC. Aliifikisha Yanga SC hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika ikatolewa na Mamelodi Sundwons ya Afrika Kusini baada ya kufungwa 3-2 ugenini na kutoa sare ya 3-3 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Mwaka 2002 akahamia Coastal Union, 2003 akarejea Prisons alikodumu hadi 2005 alipohamia Moro United, kabla ya 2006 kuhamia Miembeni ya Zanzibar aliyoipa ubingwa wa Zanzibar na ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mbele ya vigogo wa Bara, Mtibwa Sugar, Simba na Yanga SC.
  Mwaka 2008 akawa Kocha wa African Lyon kwa msimu mmoja kabla ya kuhamia Ruvu Shooting alikodumu hadi 2013 alipokwenda Yanga SC kama Msaidizi wa Mholanzi, Hans van der Pluijm.
  Mwaka 2013 baada ya msimu, akaondoka na Pluijm kwenda Al Shoolai ya Saudi Arabia, ambako hawakudumu, baada ya takriban miezi mitatu wakaacha kazi kufuatia kukerwa na kuingiliwa na uongozi wa timu juu ya masuala ya usajili.
  Desemba mwaka 2014 yeye na Pluim wakarejea Yanga SC kumpokea, Mbrazl Maximo na mwishoni mwa msimu wakaipa timu ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kuifikisha hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika walipotolewa na Etoile du Sahel baada ya sae ya 1-1 Dar es Salaam na kufungwa 1-0 Tunisia.
  Kwa mara ya kwanza kufundisha timu ya taifa ilikuwa ni mwaka 1993 alipoteuliwa kufundisha timu ya vijana chini ya umri wa miaka U17, kabla ya kuteuliwa kikosi cha pili Tanzania Bara, kilichopewa jina Kakakuona mwaka 1992, ambacho kiliwapiku ‘kaka zao’ Victoria 92 kwa kufika Fainali ya Kombe la Challenge, wakati huo akiwa Msaidizi wa Sunday Burton Kayuni.
  Mwaka 2001 alikuwa Msaidizi wa Mziray chini ya Mshauri wa Ufundi, Mjerumani Burkhad Pape katika kikosi Taifa Stars kilichotwaa ubingwa wa Kombe la mataifa manne, Castle Cup.  
  Mwaka 2002, yeye na Mziray waliifiksiha timu ya Bara fainali ya Kombe la Challenge na mwaka 2007 akapewa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kama Kocha Mkuu, lakini haikufanya vizuri baada ya kuambulia nafasi ya nne.
  Mwaka 2008 akapewa timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars kama Kocha Mkuu ambako huko alipata mafanikio makubwa, ikiwemo kuiwezesha kukata tiketi ya Fainali za Mataifa ya Afrika  mwaka 2010, Fainali za Michezo ya Afrika 2011 na kuwa washindi wa tatu Kombe la COSAFA pia mwaka huo.
  Mkwasa ni mshindi wa mataji ndani na nje ya Uwanja, akiwa anacheza alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara 1975 na Mseto, 1981, 1983, 1985, 1987 na 1989 na Yanga SC, Ligi ya Muungano 1983 na 1987, wakati pia walikuwa washindi wa pili wa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka 1986.
  Huyo ni Mchezaji Bora chipukizi wa Tanzania mwaka 1975 na Mchezaji Bora wa Tanzania mwaka 1981 ambaye akiwa kocha, ametwaa mataji ya Ligi Kuu ya Bara katika miaka ya 1991, 1992, 1993 na 2015 akiwa na Yanga SC, Ligi ya Muungano 1991 na ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati mwaka 1993 mjini Kampala, Uganda.
  Ametwaa pia Ngao ya Jamii mara mbili, mwaka 2001 na 2014 akiwa na Yanga SC- na amekuwa Kocha Bora Tanzania mwaka 1999 na 2005 kabla ya kuteuliwa kuwa Kaimu Katibu Mkuu Januari mwaka jana kufuatia Baraka Deusdedit kurejea kwenye Idara ya Fedha.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: GWIJI WA YANGA SC, CHARLES BONIFACE MKWASA KUJIUZULU UKATIBU MKUU KWA SABABU ZA KIAFYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top