• HABARI MPYA

  Tuesday, December 13, 2016

  SIMBA YAMSAJILI STRAIKA ALIYEIFUNGA YANGA IKIPIGWA 1-0 NA STAND UNITED

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imemsajili, mshambuliaji chipukizi Pastory Athanas aliyefunga bao pekee la Stand United katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  ‘Dogo’ huyo wa umri wa miaka 22, aliipasua ngome ya Yanga Septemba 25 mwaka huu Uwanja wa Kambarage Shinyanga iliyokuwa chini ya Mtogo Vincent Bossou na kumtungua kipa Ally Mustafa ‘Bafrthez’ dakika ya 58. 
  Huo ulikuwa mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Yanga kupoteza msimu huu kabla ya kwenda kufungwa na Mbeya City pia wiki mbili baadaye.
  Athanas amesaini leo ofisini kwa Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva katikati ya Jiji la Dar es Salaam. 
  Na anakuwa mchezaji wa pili kusaini Simba katika dirisha dogo baada ya kipa Mghana, Daniel Agyei kutoka Medeama SC ya kwao, wote wakisaini mkataba wa miaka miwili.
  Na mchezaji huyo mwenye kasi, uwezo wa kumiliki mpira na maarifa ya kimchezo, anasaini siku moja baada ya Simba kufungwa 2-1 na Mtibwa Sugar katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Anasaini zikiwa zimebaki siku tatu kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Simba itafungua dimba na Ndanda FC mjini Mtwara.
  Ikumbukwe Simba SC ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa inaongoza kwa pointi zake 35, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Yanga. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA YAMSAJILI STRAIKA ALIYEIFUNGA YANGA IKIPIGWA 1-0 NA STAND UNITED Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top