• HABARI MPYA

    Tuesday, May 19, 2015

    SAMATTA, ULIMWENGU SASA WABEBA MATUMAINI YA NOOIJ TAIFA STARS

    Mshambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana Samatta kwa pamoja na mwenzake, Thomas Ulimwengu sasa ndiyo wamebeba matumaini ya kocha Mart Nooij mechi za kufuzu AFCON Taifa Stars

    RATIBA YA MECHI ZA KUNDI G

    Jumamosi Juni 13, 2015
    Nigeria v Chad
    Misri v Tanzania
    Jumamosi Sept 5, 2015
    Tanzania v Nigeria
    Chad v Misri
    Ijumaa Machi 25, 2016
    Chad v Tanzania
    Nigeria v Misri
    Jumatatu Machi 28, 2016
    Tanzania v Chad
    Misri v Nigeria
    Jumamosi Juni 4, 2016
    Chad v Nigeria
    Tanzania v Misri
    Jumamosi Sept 3, 2016
    Nigeria v Tanzania
    Misri v Chad
    Na Mwandishi Wetu, RUSTENBURG
    KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mholanzi, Mart Nooij amesema kwamba anatarajia washambuliaji wa TP Mazembe ya DRC, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu watakiongezea kikosi chake kwa ajili ya mechi za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
    Nooij anasema hayo baada ya Stars jana kupoteza mchezo wake wa kwanza wa Kombe la COSAFA dhidi ya Swaziland.
    Amesema anashukuru kwa kupata mwaliko wa kushiriki COSAFA, kwani kwake anatumia michuano hii kama sehemu ya maandalizi ya kuwania kufuzu AFCON na CHAN Juni.
    Amesema anaamini wachezaji aliowaacha majeruhi nyumbani pamoja na nyota hao wa TP Mazembe, watakiongeza nguvu katika kikosi chake kitakaporejea Tanzania.
    Amesema amepoteza mchezo wa kwanza COSAFA ambao alitarajia kushinda, lakini vijana walicheza vizuri kipindi cha kwanza, kabla bao la wapinzani kuwapoteza mchezoni.
    “Presha ya mchezo ilikua kubwa hasa kipindi cha pili, kutokana na vijana wangu kucheza kwa kusaka bao, huku Swaziland wakimiliki zaidi mpira na kukuta mipango yetu kutokua na madhara” alisema Nooij.
    Nooij ameiongoza Stars katika mechi ya 14 jana tangu awasili mwishoni mwa Aprili kuchukua mikoba ya Mdenmark, Kim Poulsen na timu hiyo imefungwa bao 1-0 na Swaziland katika mchezo wa kwanza wa Kundi B Kombe la COSAFA Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini hapa.
    Katika mechi 14 ambazo Nooij ameiongoza Stars, imeshinda tatu tu, ikifungwa tano na kutoa sare mara sita, tena mechi nyingi ikicheza nyumbani.
    Matokeo hayo yanaiweka Stars katika mazingira magumu ya kwenda Robo Fainali- baada ya Madagascar kuifunga 2-1 Lesotho katika mchezo wa kwanza.
    Stars sasa lazima ishinde mechi zake mbili zijazo dhidi ya Lesotho na Madagascar ili kuangalia uwezekano wa kwenda Robo Fainali.
    Mart Nooij ameshinda mechi tatu tu kati ya 14 tangu aanze kufundisha Taifa Stars Aprili mwaka jana

    Swaziland ambayo bao lake pekee lilifungwa na  Sifiso Mabila kwa shuti kali dakika ya 42 baada ya kutanguliziwa pasi kwenye njia na Xolani Sibandze aliyemtoka Oscar Joshua upande wa kushoto, waliizidi ufundi uwanjani Stars jana.
    Taifa Stars itatupa kete yake ya pili kesho Saa 11:00 jioni kwa saa za Afrika kusini, sawa na Saa 12:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki dhidi ya Madagascar katika Uwanja wa Royal Bafokeng. Madagascar walishinda mabao 2-1 dhidi ya Lesotho katika mchezo wa kwanza jana.
    Baada ya COSAFA, Taifa Stars inatarajiwa kwenda kuweka kambi Addis Ababa, Ethiopia mwezi ujao kujiandaa na mchezo wa kwanza wa Kundi G dhidi ya Misri, kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2017 nchini Gabon.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA, ULIMWENGU SASA WABEBA MATUMAINI YA NOOIJ TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top