• HABARI MPYA

    Sunday, May 24, 2015

    MABADILIKO YA BENCHI LA UFUNDI TAIFA STARS KWA SASA HAYAKWEPEKI

    MJADALA mkubwa kwa sasa katika soka ya Tanzania ni kuhusu matokeo mabaya ya timu ya taifa chini ya kocha Mholanzi, Mart Nooij.
    Kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, mijadala imetawala na bahati mbaya sana wengine wanaleta mzaha, wengine hawana hoja za msingi zaidi ya kuwasilisha jazba zao tu chuki binafsi.
    Mmoja kati ya watu walionivutia kwa hoja zao wiki hii ni Nahodha wa Taifa Stars katika michuano ya Kombe la COSAFA, John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
    Adebayor amezungumzia matatizo ya soka ya Tanzania kwa ufahamu wake kwa ujumla, nirudie kusema; hoja zake zimenikuna.
    Zimetugusa wengi, tukiwemo Waandishi wa Habari kwamba kwa namna moja au nyingine, tunachangia matatizo ya soka yetu. Mfumo mbovu kwa ujumla, kuanzia kwenye soka na hata vyombo vya habari vya michezo.
    Ajenda na sera kubwa ya vyombo vya habari nchini ni biashara na ndiyo maana Wahariri wanaumiza vichwa kila siku kutafuta kichwa kizuri cha kuipamba habari ya Simba au Yanga tu.
    Timu zetu za magazetini, timu kongwe zinazopaswa kuwa mfano kimfumo katika soka ya Tanzania, tuanze sasa kuangalia mifumo yake, je ni ambayo ina tija kwa soka letu?
    Tutajadili mengi, lakini ustawi wa timu ya taifa kwanza unatokana na klabu bora, zenye mifumo mizuri na baadaye kuwa na Ligi Kuu bora, ya ushindani na ya haki bila mizengwe ya marefa.
    Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) halimiliki wachezaji, bali klabu na si jukumu la TFF kuwa na miradi ya kuzalisha vipaji, bali ni klabu.
    TFF inachukua wachezaji kutoka kwenye klabu kuanzia kujenga timu za vijana hadi wakubwa- sasa kama klabu hazina mifumo bora ya kuzalisha wachezaji bora na Vyombo vya Habari vinaendelea kusifia; “Simba balaa, Yanga noma” tutarajie nini?
    Sisi wa vyombo vya Habari lazima ufike wakati kalamu zetu ziache kuyumbishwa na mawimbi ya ushabiki wa Simba na Yanga na kuamua kusimamia kwenye ukweli, tuwaambie watu ukweli wa matatizo ya soka nchi hii bila woga, ili tujirekebishe. 
    Simba na Yanga zina miaka karibu 80, lakini hazina viwanja tu. Tafakari hizo ni timu mpira kweli au wababaishaji tu?
    Kwa muda ambao klabu zimekuwapo, zilipaswa kuwa mfano bora sana siyo tu Tanzania bali na Afrika nzima, lakini kwa sababu sisi wa vyombo vya Habari tumeshindwa kushinikiza mabadiliko, tutarajie hiyo Azam FC yenye miaka ‘miwili’ ndiyo ilete mabadiliko?
    Huko Azam kwenyewe hamkani si shwari- makocha hawakai, akademi ipo ipo tu. Gharama nyingi zimetumika kuwekeza, lakini huwezi kuona cha maana sana kinachofanyika pale, si hoja yangu hiyo leo, nitaitafutia siku yake.
    Bocco amefanya kitu ambacho tulipaswa kufanya sisi Waandishi wa Habari. Lazima tukubali bila kuona haya, huyu kijana ana upeo wa hali ya juu na moyo wa kizalendo pia.
    Pamoja na ukweli huo wa Bocco, lakini pia matatizo ya soka yetu ni sugu na yanajulikana. Wakubwa wameshindwa kuwa mfano na inavyoonekana hawawezi tena.
    Simba na Yanga ni vijiwe na sehemu za watu kutengeneza umaarufu wakafanikishe mambo yao mengine kwa urahisi. Si klabu za mpira. Tunajua.
    Pamoja na ukweli huo, lakini hatuwezi kuacha kucheza mpira. Tutaendelea na matatizo yetu hivyo hivyo.
    Na katika kuendelea kucheza mpira katika hali hiyo hiyo mbovu, hatuwezi kuwa watu tuliojikatia tamaa moja kwa moja.
    Ndiyo maana inapotokea mambo yanakwenda kinyume cha matarajio, wenye nchi lazima tuwe wakali. Hatupo katika kiwango kikubwa, lakini hatupo katika kiwango cha chini kama hiki ambacho tumekishuhdia siku za karibuni chini ya Mart Nooij.
    Mart Nooij alianza vizuri kwa sababu aliikuta timu iliyoachwa na Mdenmark Kim Poulsen, lakini baada ya muda, ile ladha imeanza kutoweka na sasa tuko ovyo.
    Kile kikosi kilichokwenda COSAFA, chini ya mwalimu mwingine kingeweza kufanya vizuri hata kufika Nusu Fainali, lakini kwa sababu hakukuwa na kocha mzuri matokeo yake ndiyo yale tumefungwa mechi zote za Kundi B na kurudi nyumbani mikono mitupu.
    Mfumo wetu mbovu unaweza kutunyima nafasi ya kwenda AFCON au Kombe la Dunia, lakini si kufanya vizuri kwenye mashindano kama ya CECAFA, COSAFA na kutoa ushindani kwenye mechi za kufuzu za AFCON na Kombe la Dunia. 
    TFF wanatuambia hawawezi kumfuta kazi Nooij kwa sababu amebakiza mwaka mzima katika Mkataba wake hivyo watapaswa kumlipa. Hawana fedha.
    TFF haikukosea kumuondoa Kim Poulsen, uwezo wake ulifikia mwisho na kama itakumbukwa tulifikia kufungwa nyumbani na ugenini na Uganda kufuzu CHAN.
    Lakini kwa huyu mwalimu aliyemfuatia Kim, yaani Nooij hapa TFF imechemka na kielelezo ni takwimu na kiwango cha timu. 
    Na mbaya zaidi, hata benchi lake la Ufundi ni dhaifu pia. Salum Mayanga ni mwalimu anayeinukia vizuri, lakini bora angeanza kukomazwa katika timu za vijana. Huku juu bado.
    Timu kubwa zina ambo mengi, kwanza kuweza kuwamudu wachezaji  ‘wakubwa’. Timu ya taifa inahitaji kocha ambaye ataheshimiwa na wachezaji. Na tunafahamu wachezaji wetu wengi wao wana nidhamu mbovu.
    Lakini pia kocha Msaidizi wa timu taifa, lazima awe yule ambaye amekwishafanya kazi na makocha wengi wa kigeni, ili aweze kuona tofauti ya mtu anayefanya naye kazi katika wakati uliopo na uliopita. Kwa Mayanga pekee kuwa chini ya Nooij, benchi la Taifa Stars ni dhaifu.
    Tunafahamu Kamati ya Utendaji ya TFF inakutana leo kujadili mwenendo wa timu za taifa, basi waingie mkutanoni wakijua kwamba, mabadiliko ya benchi la Ufundi la Taifa Stars hayakwepeki kwa wakati huu. Siku njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MABADILIKO YA BENCHI LA UFUNDI TAIFA STARS KWA SASA HAYAKWEPEKI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top