• HABARI MPYA

    Wednesday, May 20, 2015

    KOCHA ALIYEIPA YANGA ‘NDOO’ YA TANO KAGAME APEWA JUKUMU LA KUWAFUNDISHA AKINA ADEBAYOR

    KOCHA aliyewapa Yanga SC Kombe la tano la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kagame, Mbelgiji Tom Saintfiet anatarajiwa kusaini Mkataba wa miaka miwili kuinoa timu ya taifa ya Togo.
    Anatarajiwa kusaini Mkataba huo Juni 1, kiasi cha wiki moja kabla ya The Hawks kumenyana na Ghana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa.
    Togo itaanza kampeni zake za kuwania kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017 nyumbani dhidi ya Liberia Juni 13.
    Saintfiet tayari ametaja kikosi chake cha awali cha wachezaji 30, akimjumuisha mshambuliaji wa Tottenham Hotspur ya England, Emmanuel Adebayor kwa ajili ya mechi zijazo.
    Tom Saintfiet (kulia) sasa kocha wa Togo ya akina Adebayor

    Kocha huyo wa zamani wa Ethiopia, Namibia na Malawi atasaidiwa na Nahodha wa zamani wa Togo, Abalo Dosseh.
    Saintfiet alikuwa kocha wa muda wa Togo katika mchezo wa kirafiki wakitoa sare na Mauritius mwezi Machi.
    “Tumeamua kwa pamoja na Wizara ya Michezo kurejesha imani yetu kwa Tom Saintfiet,” amesema Antoine Folly, Ofisa wa Shirikisho la Soka Togo.
    “Pia tumeamua kwa mara ya kwanza katika historia ya soka ya nchi hii kusaini Mikataba na benchi zima la Ufundi, Kocha Mkuu na Msaidizi wake,”amesema na kuongeza; “Nyuma tulikuwa tunampa Mkataba Kocha Mkuu tu. Sasa tumeamua kuboresha mazingira,”.
    Togo imekuwa bila kocha tangu Tchakala Tchanile amalize Mkataba mwaka jana The Hawks ikishindwa kufuzu AFCON ya 2015.
    Saintfiet mara ya mwisho alikuwa kocha wa klabu ya Free State Stars ya Afrika Kusini kabla ya kutupiwa virago Novemba mwaka jana.
    Mwaka 2012 aliifundisha kwa muda mfupi, Yanga SC akiipa Kombe la Kagame mjini Dar es Salaam, kabla ya kutofautiana na Mwenyekiti, Yussuf Manji na kuvunjiwa Mkataba 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA ALIYEIPA YANGA ‘NDOO’ YA TANO KAGAME APEWA JUKUMU LA KUWAFUNDISHA AKINA ADEBAYOR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top